Vatican News
Kardinali Pietro Parolin, hivi karibuni ameweka jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Bikira Maria wa Shauri Jema, huko Tirana, Albania Kardinali Pietro Parolin, hivi karibuni ameweka jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Bikira Maria wa Shauri Jema huko Tirana, Albania. 

Kardinali Parolin: Jiwe la msingi la Hospitali Tirana, Albania!

Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, akiwa kwenye Chuo Kikuu cha Bikira Maria wa Shauri Jema, kinachoongozwa na Shirika la Mabinti wa Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, mahali ambapo panajengwa Hospitali ya Bikira Maria wa Shauri Jema, ameweka jiwe la msingi la Hospitali pamoja na Kitivo cha Tiba, ili kuweza kuboresha huduma ya afya kwa wananchi wa Albania.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican hivi karibuni amefanya ziara ya kitume mjini Tirana, nchini Albania ambako amebariki jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Bikira Maria wa Shauri Jema. Nchini Albania, Kardinali Parolin amelakiwa na Kardinali Ernest Simon aliyekuwa ameambatana na Askofu mkuu Charles J. Brown, Balozi wa Vatican nchini Albania pamoja na Monsinyo Romanus Mbena, mkuu wa itifaki ubalozini hapo! Akiwa nchini Albania, Kardinali Parolin amepata fursa ya kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu na Baraza la Maaskofu Katoliki Albania. Katika mahubiri yake, amekazia zaidi kuhusu hekima ya Kikristo na Fadhila za kimungu na hasa Imani, ili iweze kuwasaidia kuwa imara katika maisha na utume wao kwa watu wa Mungu nchini Albania.

Fadhila ya imani, iwawezeshe viongozi wa Kanisa kutambua na kuambata mapenzi ya Mungu katika maisha yao, ili waweze kuishi na kutenda kwa haki, daima wakijitahidi kuimwilisha katika vipaumbele vya maisha na utume wao. Maaskofu wakumbuke kwamba, wao ni wahudumu na mashuhuda wa imani kwa ajili ya wokovu wa walimwengu! Kardinali Parolin amegusia pia uhusiano kati ya Serikali na Kanisa na umuhimu wa Kanisa kuendelea kujizatiti katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Changamo, matatizo na fursa mbali mbali zinazopatikana nchini humo zinapaswa kujadiliwa na Maaskofu wote, ili hatimaye, kufikia uamuzi na utekelezaji wa pamoja.

Kardinali Parolin amewapongeza wakleri, watawa na wamisionari wanaoendelea kujisadaka kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili hata katika mazingira magumu na hatarishi kama ilivyo kwa sasa nchini Albania. Kardinali Parolin alipata nafasi pia ya kumtembelea na kuzungumza na Rais Ilir Meta wa Albania, mlezi wa Mfuko wa Bikira Maria wa Shauri Jema aliyetoa mwaliko kwa Kardinali ili kushuhudia tukio hili la huruma na upendo wa Mungu kwa maskini na wagonjwa. Viongozi hawa wawili katika mazungumzo yao, wameridhishwa na uhusiano wa muda mrefu kati ya Albania na Vatican; majadiliano ya kidini na kiekumene nchini humo na kwamba, umefika wakati wa kuanza utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa kati ya Albania na Vatican kunako mwaka 2002.

Wamezungumzia umuhimu wa kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu pamoja na kuhakikisha kwamba, changamoto zinazowakabili wananchi wa Albania zinasikilizwa na kupewa ufumbuzi wa kudumu. Viongozi wa Serikali ya Albania pamoja na Vatican wameahidi kuendeleza ushirikiano katika masuala ya utamaduni na elimu.

Kardinali Parolin, akiwa kwenye Chuo Kikuu cha Bikira Maria wa Shauri Jema, kinachoongozwa na Shirika la Mabinti wa Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, mahali ambapo panajengwa Hospitali ya Bikira Maria wa Shauri Jema, ameweka jiwe la msingi la Hospitali pamoja na Kitivo cha Tiba, ili kuweza kuboresha huduma ya afya kwa watu wa Mungu nchini Albania. Tukio hili limehudhuriwa na viongozi mbali mbali wa Serikali, Kanisa na Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume nchini Albania.

Wazo la ujenzi wa Hospitali ya Bikira Maria wa Shauri Jema lilianza kunako mwaka 1993, wakati ambapo Serikali ya Albania iliwekeana mkataba na Vatican, ili kuanzisha Hospitali ambayo ingemilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki. Lengo likiwa ni kutoa huduma bora za afya pasi na upendeleo kwa familia ya Mungu nchini Albania. Pili, Hospitali hii ililenga kutoa mafunzo kwa madaktari na wauguzi, ili kusaidia mchakato wa huduma ya afya nchini Albania, kwa kuwa na maabara bora zaidi ya uchunguzi wa magonjwa pamoja na tafiti ili kuendelea kupyaisha na kucharuka katika huduma ya tiba kwa binadamu.

Ujenzi wa Hospitali hii, unafanyika katika awamu kuu tatu. Kardinali Pietro Parolin katika hotuba yake, amewapatia salam na matashi mema kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko pamoja na kuwapongeza wale wote wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya huduma makini kwa wagonjwa, maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Amewashukuru wafadhili mbali mbali kwa wena na ukarimu wao ili kuliwezesha Kanisa kuendelea kutoa huduma ya afya na elimu kwa familia ya Mungu nchini Albania.

Kardinali Parolin ameipongeza Serikali ya Albania kwa kushirikiana kwa karibu sana na Kanisa katika huduma za kijamii na kwamba, huu ni mfano bora wa kuigwa katika kukuza na kudumisha ushirikiano kati ya Serikali na taasisi binafsi katika huduma. Amewakumbusha wafanyakazi katika sekta ya afya kwamba, wao ni wahudumu wa maisha ya binadamu, utu na heshima yake. Wanapaswa kutambua kwamba, binadamu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na maisha yake ni matakatifu, kumbe yanapaswa kulindwa, kuheshimiwa na kuendelezwa. Wafanyakazi wa sekta ya afya wanapaswa kuweka uwiano mzuri kati ya taaluma, weledi na utu wao ili kujenga na kuimarisha uhusiano kati ya madaktari na wagonjwa wanaowahudumia kwa imani, matumaini na mapendo!

Kardinali Parolin: Tirana
06 March 2019, 16:14