Tafuta

Vatican News
Papa Francisko atuma msaada Kusini mwa Afrika kwa waathirika wa kimbunga cha Idai, ambacho kimesababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao! Papa Francisko atuma msaada Kusini mwa Afrika kwa waathirika wa kimbunga cha Idai, ambacho kimesababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao!  (IFRC)

Papa Francisko atoa msaada kwa waathirika Kusini mwa Afrika!

Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko limechangia kiasi cha Euro 150, 000 ili kusaidia kutoa huduma ya kwanza kwa waathirika. Fedha hii itawafikia walengwa kupitia kwa balozi za Vatican zilizoko katika nchi hizi. Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki kuendelea kuchangia ili waathirika wapate huduma!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kimbunga cha Idai kilichotokea hivi karibuni huko: Msumbiji, Malawi na Zimbabwe, kimesababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuonesha uwepo wake wa karibu kwa njia ya sala na sadaka yake, kwa watu wote walioguswa na kutikiswa na majanga haya asilia, kielelezo cha upendo na mshikamano wa Kanisa kwa watu wanaoteseka!

Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko limechangia kiasi cha Euro 150, 000 ili kusaidia kutoa huduma ya kwanza kwa waathirika. Fedha hii itawafikia walengwa kupitia kwa balozi za Vatican zilizoko katika nchi hizi. Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki kutoka sehemu mbali mbali za dunia, pamoja na watu wenye mapenzi mema, wanaendelea kuhamasishwa kuchangia, ili kusaidia wananchi waliokumbwa na maafa makubwa huko Msumbiji, Zimbabwe na Malawi.

Takwimu zinaonesha kwamba, zaidi ya watu 500 wamefariki dunia katika nchi hizi tatu; kuna watu milioni 1.7 ambao wameguswa na kutikiswa sana na kimbunga cha Idai wengi wao wakiwa ni watoto pamoja na maelfu ta watu wasiokuwa na makazi maalum kutokana na nyumba zao kukumbwa na mafuriko makubwa. Hatari iliyoko mbele ya waathirika hawa ni magonjwa ya mlipuko. Msaada wa dharura unaohitaji kwa wakati huu ni: ujenzi wa makazi ya muda, chakula, maji safi na salama; elimu, ili wanafunzi waendelee kusoma, vifaa tiba pamoja na dawa ni muhimu sana kwa wakati huu!

Maafa Afrika

 

 

23 March 2019, 15:43