Tafuta

Vatican News
Padre Raniero Cantalamessa: Tafakari za Kwaresima 2019: Kauli mbiu: Ingia ndani mwako! Padre Raniero Cantalamessa: Tafakari za Kwaresima 2019: Kauli mbiu: Ingia ndani mwako!  (ANSA)

Tafakari za Kipindi cha Kwaresima 2019: Ingia ndani mwako!

Tafakari za Kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2019 zinaongozwa na kauli mbiu “Ingia ndani mwako” sehemu ya maneno ya Mtakatifu Agostino, Askofu na Mwalimu wa Kanisa, anayewaalika waamini kuingia katika undani wa maisha yao ili kupata amani na utulivu wa ndani, kwa kugundua na kutambua uwepo endelevu wa Mungu ndani mwao na kati ya wale wanaowazunguka.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Padre Raniero Cantalamessa, Mhubiri wa Nyumba ya Kipapa anasema, tafakari za Kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2019 zinaongozwa na kauli mbiu "In te ipsum redi" yaani “Ingia ndani mwako” sehemu ya maneno ya Mtakatifu Agostino, Askofu na Mwalimu wa Kanisa, anayewaalika waamini kuingia katika undani wa maisha yao kwa kuondokana na mahangaiko na changamoto za maisha, ili hatimaye, kupata amani na utulivu wa ndani, kwa kugundua na kutambua uwepo endelevu wa Mungu katika undani wa maisha yao na Walatini wanasema "Coram Deo". Ukweli wa maisha umejikita katika undani wa mtu!

Hizi ni tafakari ambazo kwa kawaida zinahudhuriwa na Baba Mtakatifu Francisko, waandamizi wake kutoka Sekretarieti kuu ya Vatican pamoja na wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume wanaoishi na kufanya utume wao hapa mjini Roma! Kwa mwaka huu, kutakuwa na tafakari tano zinazoanza rasmi tarehe 15 Machi 2019 hadi tarehe 12 Aprili 2019. Mahubiri haya ni sehemu ya mchakato na mwaliko kwa walengwa kujitahidi kutoa nafasi kwa uwepo endelevu wa Mungu katika maisha yao, kwa kuondokana na ubinafsi, ili kweli Mwenyezi Mungu aweze kuzima kiu ya maisha na utume wao!

Hivi ndivyo ilivyokuwa kwa Waisraeli walipokuwa utumwani, kiasi cha kuwa na shauku ya Mungu “... Nafsi yangu inamwonea kiu Mungu” Zab. 42:1-2. Huu ni mwaliko kwa waamini kutambua uwepo endelevu wa Mungu katika maisha yao. Ikumbukwe kwamba, watu wanakutana na Mwenyezi Mungu katika: Biblia, Sakramenti za Kanisa na hasa zaidi Ekaristi Takatifu na kati ya jirani zao. Mtakatifu Agostino anawataka waamini kuingia ndani mwao, wenyewe, ili waweze kujifahamu jinsi walivyo pamoja na kutambua uwepo wa Mungu katika maisha na utume wao.

Kipindi cha Kwaresima ni wakati wa kuingia katika jangwa la maisha ya kiroho, ili kutafuta nafasi ya kuzungumza na Mungu kwa njia ya: Sala, Tafakari, Kufunga na Matendo ya huruma. Waamini wanaweza kujitengenezea nafasi ya kuingia ndani mwao, hata walau kwa muda mfupi tu, wakati wa mapumziko, wakiwa njiani kurejea nyumbani baada ya pilika pilika za mchana kutwa na hata pengine, kabla ya kulala. Waamini wajifunze kumsikiliza Mwenyezi Mungu anayezungumza nao kutoka katika undani wa maisha yao. Wajitahidi kushiriki kwa uelewa mpana zaidi wa maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa.

Padre Raniero Cantalamessa anasema, kuna haja ya kutafuta nafasi ya kuzungumza na Mungu kutoka katika undani wa maisha kwa kuondokana pia na miungu wadogo ambao: uchu wa mali na fedha; madaraka na tabia ya watu kupenda kujikweza sana! Kuna miungu ambao wanaendelea kusababisha majanga katika maisha ya watu: ngono, vita pamoja na ubinafsi ambao kimsingi ndio “ndama wa dhahabu” ambaye kila mwanadamu amembeba moyoni na kichwani pake! Padre Raniero Cantalamessa anasema, Msalaba ni muhtasari wa huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake! Ni kielelezo cha unyenyekevu wa Neno wa Mungu aliyefanyika mwili: Juu ya Msalaba, kumetundikwa hekima ya Mungu. Katika kipindi cha Kwaresima, Msalaba unabeba maana ya pekee sana katika maisha na utume wa waamini. Ni alama ya ufunuo wa upendo wa Mungu na sadaka ya hali ya juu kabisa, bila ya kujibakiza hata kidogo!

P. Cantalamessa
14 March 2019, 14:31