Tafuta

Vatican News
Wanawake wanapaswa kuwezeshwa kiuchumi ili kuchangia mapambano dhidi ya baa la njaa na uharibifu wa mazingira duniani! Wanawake wanapaswa kuwezeshwa kiuchumi ili kuchangia mapambano dhidi ya baa la njaa na uharibifu wa mazingira duniani!  (ANSA)

Wanawake: Mapambano na baa la njaa na uharibifu wa mazingira!

Wanawake wakiwezeshwa kikamilifu, wanaweza kuendelea kutoa mchango mkubwa zaidi hata katika mchakato wa mapambano dhidi ya baa la njaa na utapiamlo duniani sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote! Wanawake wajengewe nguvu ya kiuchumi na wapewe ujuzi na maarifa, ili kuweza kuwa na uhakika wa usalama wa usalama wa chakula duniani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani tarehe 8 Machi 2019, amekumbusha kwa kusema kwamba, wanawake wamekuwa na mchango mkubwa sana katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wengi duniani. Ni kundi ambalo limechangia sana kulinda na kuenzi uhai, kiasi hata cha kuthubutu kujisadaka. Wanawake ni walinzi wakuu wa amani duniani, inayobubujika kutoka katika maisha yao kama akina mama. Wanawake ni wenza wakuu wa maendeleo na wanabeba ndani mwao ile ndoto ya upendo!

Wanawake wanayo ndoto ya leo na kesho ya amani, kumbe, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, wanawake wanapewa nafasi ili kuchangia ustawi, maendeleo na mafao ya wengi! Wanawake wanayo fadhila ya huruma na mapendo inayobubujika kutoka kwenye asili yao ya umama. Wanawake wakiwezeshwa kikamilifu, wanaweza kuendelea kutoa mchango mkubwa zaidi hata katika mchakato wa mapambano dhidi ya baa la njaa na utapiamlo duniani sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote! Wanawake wanapaswa kuwezeshwa kiuchumi ili waweze kuwa na nguvu ya kiuchumi, ujuzi na maarifa, ili kuweza kuwa na uhakika wa usalama wa lishe na chakula duniani.

Kwa njia hii, wanawake wanaweza kuwa ni kiungo kikuu cha mshikamano katika mapambano dhidi ya baa la njaa duniani na kama sehemu ya utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu na Fungamani ifikapo mwaka 2030. Jambo jingine linalopaswa kupewa msukumo wa pekee na Jumuiya ya Kimataifa ni usawa, utu na heshima kwa wanawake. Wanawake wapewe fursa ya kushiriki katika vikao vyote vinavyopanga, amua na kutekeleza mambo msingi katika jamii, ili hata wao waweze kuchangia mawazo yao tangu awali!

Monsinyo Fernando Chica Arellano, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye: Shirika la Kilimo na Chakula la Umoja wa Mataifa, FAO, Mfuko wa Maendeleo ya Kilimo wa Umoja wa Mataifa, IFAD pamoja na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani, WFP., anasema, kuwekeza kwa wanawake kama sehemu ya mchakato wa kilimo endelevu ni ufunguo wa maendeleo ya jamii. Wanawake ndio wanao ratibu kwa kiasi kikubwa uchumi wa nyumbani na kwa namna ya pekee vijijini ambako ni wadau wakuu katika sekta ya kilimo. Hawa ni nguvu kazi ya sekta ya kilimo sehemu mbali mbali za dunia.

Kumbe, wanawake wanapaswa kupewa ujuzi na maarifa ili waweze kuwa mstari wa mbele katika utunzaji wa mazingira nyumba ya wote. Uharibifu wa mazingira umekuwa ni kati ya vyanzo vikuu vinavyoendelea kuwatumbukiza watu wengi katika maafa, magonjwa, umaskini na ujinga. Baba Mtakatifu Francisko angependa kuona wanawake wakiheshimiwa na kuthaminiwa kwa kuondokana na tabia ya mfumo dume, unaoendelea kuwadhalilisha na kuwakandamiza wanawake. Ni muhimu ikiwa kama Jumuiya ya Kimataifa itawekeza katika elimu, malezi na makuzi ya kiutu, ili kujenga na kudumisha utandawazi wa mshikamano wa kidugu unaosimikwa katika kanuni ya auni. Inasikitisha kuona kwamba, ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia unaendelea kujenga utamaduni wa kutoguswa na shida pamoja na mahangaiko ya watu wengine.

Monsinyo Fernando Chica Arellano anaendelea kufafanua kwamba, takwimu zilizotolewa na FAO pamoja Umoja wa Afrika kwa mwaka 2018 zinaonesha kwamba, mchango wa wanawake katika sekta ya kilimo bado haujapewa msukumo wa pekee ili kuchangia zaidi katika mchakato wa uzalishaji katika sekta ya kilimo. Matokeo yake, wanawake wengi maeneo ya vijijini wamebakizwa nyuma katika masuala ya uzalishaji, usimamizi wa rasilimali pamoja mambo ya lishe. Ikumbukwe kwamba, wanawake ni sawa na asilimia 48% ya nguvu kazi katika kilimo.Wanawake wakiwezeshwa kikamilifu, baa la njaa, utapiamlo wa kutisha pamoja na umaskini vinaweza kupewa kisogo na Jumuiya ya Kimataifa.

Na kwa njia hii, anasema Monsinyo Arellano, utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu na fungamani ya binadamu yanaweza kufikiwa. Kumbe, maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, yalenge zaidi katika mchakato wa kuwawezesha wanawake katika medani mbali mbali za maisha, ili kweli waweze kushiriki katika mapambano ya baa la njaa duniani pamoja na uharibifu wa mazingira nyumba ya wote!

Wanawake Duniani
11 March 2019, 08:34