Tafuta

Vatican News
Makongamano ya Ekaristi Takatifu ni muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa. Makongamano ya Ekaristi Takatifu ni muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa.  (ANSA)

Makongamano ya Ekaristi Takatifu katika utume wa Kanisa!

Ekaristi takatifu ni shule ya upendo, ukarimu, umoja na mshikamano wa dhati. Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya Upendo; zawadi na sadaka ya Kristo Yesu Msalabani; kielelezo cha huduma inayomwilishwa na kuwasha mapendo kwa Mungu na jirani. Ni Sakramenti ya Altare, mahali pa kukutana mubashara na Kristo Yesu katika maumbo ya Mkate na Divai; Mwili na Damu yake Azizi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Makongamano ya Ekaristi Takatifu Kitaifa na Kimataifa ni katekesi endelevu na ya kina: kuhusu Fumbo la Ekaristi Takatifu, kiini na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Katika adhimisho la Fumbo la Ekaristi Takatifu kuna mkate na divai, ambavyo kwa maneno ya Kristo Yesu na kwa nguvu ya Roho Mtakatifu hugeuka kuwa Mwili na Damu ya Kristo, chakula cha kiroho na masurufu ya njiani. Ekaristi takatifu ni shule ya upendo, ukarimu, umoja na mshikamano wa dhati kati ya watu wa Mungu. Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya Upendo; zawadi na sadaka ya Kristo Yesu Msalabani; kielelezo cha huduma inayomwilishwa na kuwasha mapendo kwa Mungu na jirani.

Ni Sakramenti ya Altare, mahali pa kukutana mubashara na Kristo Yesu katika maumbo ya Mkate na Divai; Mwili na Damu yake Azizi. Ekaristi Takatifu ni Fumbo na muhtasari wa imani ya Kanisa. Hii ni zawadi ya upendo inayobubujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu kwa kumwonesha Kristo Yesu kuwa kweli ni Mwanakondoo wa Mungu na sadaka hai inayotolewa kwa ajili ya maondoleo ya dhambi na maisha ya uzima wa milele! Ekaristi Takatifu ni kielelezo cha Kristo anayejitoa mwenyewe kwa ajili ya ujenzi wa Fumbo la Mwili wake, yaani Kanisa pamoja na utendaji wake. Hii ni Sakramenti ya umoja wa Kanisa, inayoimarisha na kudumisha upatanisho kati ya Mungu na jirani.

Mababa wa Kanisa wanasema, Ekaristi Takatifu ni Fumbo linalopaswa kuadhimishwa kwa Ibada, Uchaji wa Mungu na Uaminifu, ili kuonja: uzuri, ukuu na utakatifu wa Sakramenti hii ya ajabu, inayoonesha Mwili na Damu Azizi ya Kristo Yesu kama anavyofafanuliwa na Mtakatifu Thoma wa Akwino! Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu, kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa, tarehe 1 Machi 2019 amehitimisha Kongamano la IV la Ekaristi Takatifu Kitaifa kwa kuwahimiza waamini kujikita katika ushiriki mkamilifu wa maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi takatifu ili waweze kujichotea neema, nguvu na ari ya kuweza kutekeleza dhamana ya kimisionari kwa kutangaza na kushuhudia upendo na huruma ya Mungu inayobubujika kutoka katika Fumbo la Ekaristi Takatifu.

Kongamano hili ni tukio ambalo limewakusanya waamini kutoka Majimbo mbali mbali nchini Taiwan, ili kushiriki katika katekesi na tafakari ya kina kuhusu Fumbo la Ekaristi Takatifu, kumbu kumbu endelevu ya uwepo wa Kristo Yesu kati ya watu wake katika maumbo ya Mkate na Divai; Mwili na Damu yake Azizi! Hii ni Sakramenti ya umoja, upendo na inayozima kiu ya maisha ya kiroho, tayari kutoka kifua mbele kwenda kujisadaka na kujimega kwa ajili ya huduma kwa Mungu na jirani na hasa zaidi kwa maskini na wale wote wanaoteseka: kiroho na kimwili! Ekaristi Takatifu ni chachu ya toba na wongofu wa ndani kama ilivyokuwa kwa Zakayo Mtoza Ushuru, aliyekutana mubashara na Kristo Yesu, akatubu na kumwongokea Mungu na akawa kweli ni chombo cha huruma ya Mungu kwa watu wake!

Ni wakati kwa waamini kujenga na kuimarisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia; kwa kusaidiana, kupokeana, kukamilishana na kutakatifuzana. Huu ni muda wa kuimarisha dhamana na wajibu wa wazazi kwa watoto wao katika masuala ya elimu, malezi na makuzi mintarafu maelekezo ya Kanisa, Mama na Mwalimu! Ekaristi Takatifu ijenge na kuimarisha umoja na mshikamano katika mapambano ya umaskini, ujinga na umaskini; kwa kulinda na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo, utu, heshima na haki msingi za binadamu!

Wajumbe wa Kongamano la IV la Ekaristi Takatifu Kitaifa nchini Taiwan kwa Mwaka 2019  wanakiri kwamba, wameguswa kwa namna ya pekee na maadhimisho ya Kongamano la Ekaristi Kitaifa na kwamba, wanayo changamoto kubwa mbele yao ya kuhakikisha kwamba, wanamwilisha na kuendeleza yale yaliyowagusa katika maisha na utume wao ndani ya Kanisa kwa njia ya ushuhuda wa imani tendaji, ili kweli waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya: Imani, Mapendo na Matumaini, kwa wale wote waliokata tamaa! Wanataka kuwa kweli ni mashuhuda wa furaha ya Injili kwa kukutana mubashara na Kristo Yesu katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu.

Sasa waamini walei, wanatumwa kuwa ni wamisionari wa furaha ya Injili ndani na nje ya Taiwan. Waamini wakumbuke kwamba, wanashiriki kikamilifu: Ukuhani, Unabii na Ufalme wa Kristo, kumbe kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, wanaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia kweli za Injili. Waamini walei wawe mstari wa mbele kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Wao wanapaswa kuwa ni chumvi ya dunia na nuru ya ulimwengu! Wajenge na kuimarisha mshikamano wa umoja na udugu kati ya watu wa Mungu kama anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko kwa Mwaka 2019.

Ikumbukwe kwamba, “Udugu wa binadamu” ndiyo kauli mbiu inayoongoza maisha na utume wa Kanisa kwa mwaka huu wa 2019! Kumbe, Neno la Mungu, Ekaristi Takatifu, Umoja na Udugu ni mambo muhimu katika mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu ndani na nje ya Taiwan. Maadhimisho ya Kongamano la Ekaristi Takatifu Kitaifa imekuwa kama ni kipindi cha mafungo ya maisha ya kiroho, yaliyotawaliwa na ukimya, sala, tafakari na ushuhuda wa imani, matumaini na mapendo. Ni matumaini makubwa ya Kardinali Ferdinando Filoni kwamba, maadhimisho ya Kongamano la IV la Ekaristi Takatifu Kitaifa litaendelea kuwa ni chemchemi ya ushuhuda wa tunu msingi za Kiinjili na uaminifu wao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake!

Makongamano ya Ekaristi
04 March 2019, 15:07