Tafuta

Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia: Mambo msingi: Mchakato wa Kanisa katika uinjilishaji wa kina pamoja na ekolojia fungamani Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia: Mambo msingi: Mchakato wa Kanisa katika uinjilishaji wa kina pamoja na ekolojia fungamani 

Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia Oktoba, 2019

Kardinali Lorenzo Baldisseri anasema Sinodi ya Amazonia itajikita katika mambo makuu mawili: mchakato wa utume wa Kanisa katika uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji msingi ya binadamu: kiroho na kimwili pamoja na ekolojia fungamani. Hizi ni nyanja mbili tofauti, lakini zinategemeana kukamilishana katika uhalisia wa maisha ya watu ukanda wa Amazonia! Hili ni tukio la Kikanisa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kardinali Lorenzo Baldisseri, Katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu katika hotuba yake elekezi kwenye Jukwaa la XV la Kimataifa kuhusu Habari za Utunzaji Bora wa Mazingira, huko San Miniato, Pisa, Kaskazini mwa Italia, Jumamosi, tarehe 9 Machi 2019 amegusia sababu msingi zilizomsukuma Baba Mtakatifu Francisko kuitisha Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia, maana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa; maamuzi kuhusu Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia pamoja na Tema msingi zinazoibuliwa na Mama Kanisa kwa wakati huu, baada ya kusoma alama za nyakati, yaani wongofu wa kiekolojia.

Mshikamano, umoja na Ukatoliki wa Kanisa ni mambo msingi ambayo yameliwezesha Kanisa katika kipindi cha takribani miaka hamsini kuweza kutembea kwa pamoja, kusali na kutafakari kuhusu utume na maisha ya Kanisa la Kristo, huku likiwa limeungana na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Ni hija ngumu yenye changamoto nyingi, lakini mwishoni inaonesha matunda ya furaha, amani na utulivu. Maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu ni matunda ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, yaliyofanyiwa kazi na Mtakatifu Paulo VI kunako tarehe 15 Septemba 1965.

Tangu wakati huo, Kanisa limeendelea kufaidika kwa kiasi kikubwa na mwono huu wa kinabii, kwa Maaskofu kushikamana na Khalifa wa Mtakatifu Petro katika kupanga na kutekeleza mikakati ya shughuli za kichungaji kwa ajili ya Kanisa la Kristo sanjari na kusoma alama za nyakati. Maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu yanawawezesha Maaskofu na waamini walei kutembea kwa pamoja katika imani, matumaini na mapendo. Maadhimisho haya yameboreshwa zaidi na Katiba ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko “Episcopalis Communio” yaani “kuhusu Sinodi za Maaskofu” iliyochapishwa mwezi Septemba 2018. Hiki ni chombo cha uinjilishaji kinachofumbatwa katika ujenzi wa utamaduni wa kusikiliza, kuadhimisha na kutenda kwa umoja.

Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia yatafanyika mjini Vatican kuanzia tarehe 6-27 Oktoba 2019 kwa kuongozwa na kauli mbiu "Amazonia: njia mpya ya Kanisa na kwa ajili ya ekolojia fungamani". Hati ya maandalizi ya Sinodi ya Amazonia inakazia umuhimu wa: kuona, kung'amua na kutenda! Ni Sinodi itakayopembua tema mbali mbali:kuhusu: haki jamii, malezi awali na endelevu, katekesi, liturujia na utambulisho wa Kanisa katika Ukanda wa Amazonia unaoziunganisha nchi tisa ambazo ni: Bolivia, Brazil, Colombia, Equador, Perù, Venezuela, Suriname na Guyana. Hatua zote za maandalizi tayari zimekwisha kutekelezwa na kwamba, Hati ya Maandalizi ya Sinodi ya Maaskofu wa Amazonia iko tayari!

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya kitume huko Amerika ya Kusini hivi karibuni alisikitika kusema kwamba, ukoloni mamboleo unaojikita katika nguvu ya kiuchumi: kwa uchimbaji wa mafuta na gesi asilia; kilimo cha mashamba makubwa ili kukidhi mahitaji ya mali ghafi ya viwanda; ni mambo yanayotishia usalama, maisha, ustawi na maendeleo ya Ukanda wa Amazonia. Baba Mtakatifu anawataka Maaskofu kuwa karibu zaidi na wakleri wao; kukuza na kudumisha tunu msingi za maisha ya Kiinjili ili kupambana na saratani ya rushwa, ufisadi na kumong'onyoka kwa haki msingi, utu na heshima ya binadamu na kwamba, Maaskofu wathamini majadiliano katika ukweli na uwazi.

Haya ni mambo msingi kama sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu iliyoitishwa na Baba Mtakatifu Francisko. Kardinali Baldisseri anakaza kusema, lengo ni kuibua mbinu mkakati wa shughuli za kichungaji zitakazokidhi mahitaji ya uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili; utamadunisho kwa kuhakikisha kwamba, tunu msingi za kiinjili zinamwilishwa katika tamaduni, mila na desturi za watu wa Amazonia pamoja na kuzisafisha zile zinazosigana na kupingana na Habari Njema ya Wokovu! Ni Sinodi itakayojikita katika mchakato wa kukuza na kudumisha haki msingi za binadamu kama njia ya kuenzi utu na heshima ya binadamu!

Kumbe, Sinodi itajikita katika mambo makuu mawili: mchakato wa utume wa Kanisa katika uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji msingi ya binadamu: kiroho na kimwili pamoja na ekolojia fungamani. Hizi ni nyanja mbili tofauti, lakini zinategemeana kukamilishana katika uhalisia wa maisha ya watu! Sinodi hii ni mwendelezo wa tafakari ya kina inayotolewa na Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa Kitume“Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”. Huu ni wajibu fungamani kwani madhara yake yanawaathiri watu wote bila ubaguzi. Uchafuzi mkubwa wa mazingira Ukanda wa Amazonia unaendelea kuhatarisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi duniani.

Kuna uhusiano mkubwa kati ya maisha na utume wa Kanisa katika Ukanda wa Amazonia anasema Kardinali Baldisseri! Mkazo ni uinjilishaji wa kina ili kukuza na kudumisha misingi ya: umoja, udugu na mshikamano kwa kujikita katika Injili ya upendo, haki, amani, maridhiano pamoja na utunzaji wa mazingira nyumba ya wote. Huu ni mwaliko wa kusikiliza na kujibu kilio cha watu mahalia Ukanda wa Amazonia, ambao kwa miaka mingi wamenyonya na kunyanyaswa sana! Utunzaji bora wa mazingi, utu, heshima na haki msingi za binadamu ni mambo msingi katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu hapa duniani.

Itakumbukwa kwamba, maadhimisho ya Jukwaa XV la Kimataifa kuhusu Habari za Utunzaji Bora wa Mazingira, huko San Miniato, Pisa, Kaskazini mwa Italia, lilianza kutimua vumbi hapo tarehe 7 na kuhitimishwa rasmi tarehe 9 Machi 2019. Hili ni tukio ambalo limewashirikisha watetezi wa mazingira kutoka sehemu mbali mbali za dunia na Afrika imewakilishwa na Teresa Muthoni Maina Gitonga, kutoka Kenya, Jean Claude Mbede, kutoka Cameroon na Ugochi Oluigbo, Mwandishi wa habari za mazingira aliyepewa tuzo kutokana na juhudi za kuandaa vipindi vizuri vya Luninga ili kuhamasisha utunzaji bora wa mazingira, nyumba ya wote!

Sinodi ya Amazonia
09 March 2019, 16:03