Tafuta

Kardinali Leonardo Sandri anapembua kwa kina na mapana kuhusu: Uhuru wa kuabudu, uhuru wa kidini, haki na amani duniani! Kardinali Leonardo Sandri anapembua kwa kina na mapana kuhusu: Uhuru wa kuabudu, uhuru wa kidini, haki na amani duniani! 

Changamoto ya uhuru wa kuabudu, haki na amani duniani

Uhuru wa kidini unafumbatwa katika mambo makuu matatu: Umuhimu wa kujenga na kudumisha umoja na mshikamano miongoni mwa waamini wa dini mbali mbali; Pili, kulinda na kudumisha amani na utulivu kama chachu muhimu ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Tatu, majadiliano ya kidini katika ukweli na uwazi ni mbinu mkakati unaoweza kuleta suluhu ya migogoro mingi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, uhuru wa kidini ni kiini cha haki msingi za binadamu kinachompatia mwamini uwezo wa kufikiri na kutenda kadiri ya dhamiri yake nyofu na kwamba, haki hii ni chimbuko la utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Uhuru wa kidini unapaswa kuzingatiwa na kuendelezwa kisheria. Binadamu aliyeumbwa kwa akili na utashi kamili, anasukumwa na maumbile na kanuni maadili kuutafuta ukweli, kuuambata na kuushuhudia. Uhuru wa kidini ni muhimu sana katika kukuza na kudumisha mahusiano na mafungamano ya kijamii na kati ya Mungu na binadamu.

Uhuru wa kidini ambao wakati mwingine unajulikana kama uhuru wa kuabudu unafumbatwa katika mambo makuu matatu yanayopaswa kuzingatiwa na wote: kwanza kabisa kuna umuhimu wa kujenga na kudumisha umoja na mshikamano miongoni mwa waamini wa dini mbali mbali; Pili, kulinda na kudumisha amani na utulivu kama chachu muhimu ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Tatu, majadiliano ya kidini katika ukweli na uwazi ni mbinu mkakati unaoweza kuleta suluhu ya changamoto mbali mbali zinazoiandama familia ya Mungu huko Mashariki ya Kati, kiasi cha amani na utulivu kushindwa kutawala katika akili na nyoyo za watu ili kujenga jamii inayosimikwa katika utu na ustaarabu!

Uhuru wa kidini ni kati ya haki msingi za binadamu zinazopaswa kulindwa na kuendelezwa kwa kuheshimu na kuthamini dhamiri ya mtu binafsi na Jamii katika ujumla wake. Hii ni haki inayojikita katika masuala ya kidini na uhuru wa kuabudu. Uhuru wa kidini unapata chimbuko lake katika utu na heshima ya binadamu. Lakini jambo la kushangaza ni kuona kwamba, madhulumu na nyanyaso za kidini dhidi ya Wakristo sehemu mbali mbali za dunia yanazidi kuongezeka mwaka hadi mwaka hata katika nchi zile ambazo zinadai kwamba, zinafuata demokrasia, hali inayoonesha kinzani katika uelewa na ufahamu wa demokrasia ya kweli!

Kardinali Leonardo Sandri, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki katika mahojiano maalum na Gazeti la L’Osservatore Romano, kuhusu mwelekeo na vipaumbele vya Baraza lake anasema, katika vita, nyanyaso na madhulumu yanayoendelea kutendeka huko Mashariki ya Kati kwa takribani miaka kumi sasa, walengwa wakuu wamekuwa ni Wakristo kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Hivi karibuni, Kardinali Sandri alipata fursa ya kutembelea maeneo mbali mbali na kushuhudia maisha na utume wa Kanisa huko Mashariki ya Kati.

Ameshuhudia jinsi ambavyo haki msingi za binadamu, utu na heshima yake vinavyosiginwa huko Mashariki ya Kati na kusema kwamba, kuna umuhimu wa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu na heshima ya binadamu, kwa kuzingatia uhuru wa kuabudu kama msingi wa mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi, msamaha na upatanisho, ili watu wa Mungu huko Mashariki ya Kati, waweze kuishi kwa amani na utulivu! Kuna matumaini makubwa huko nchini Siria na Iraq kwamba, amani na utulivu vitaweza kurejea tena kama alivyobainisha Kardinali Pietro Parolin katika ziara yake ya kichungaji huko Iraq wakati wa Sherehe za Noeli kwa Mwaka 2018.

Tangu mwaka 2010, Kanisa limekuwa mstari wa mbele kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini na huduma ya upendo kwa watu wa Mungu huko Mashariki ya kati. Hii ni changamoto endelevu iliyoibuliwa na Mtakatifu Paulo VI kunako mwaka 1964 na hatimaye tarehe 25 Machi 1974 akachapisha Waraka wake wa kitume unaojulikana kama “Nobis in Animo” yaani “Kuhusu Mahitaji ya Kanisa katika Nchi Takatifu”. Anasema, Wakristo wanaoishi katika Nchi Takatifu ni mashuhuda wa mahali patakatifu katika maisha na utume wa Kristo Yesu hapa duniani. Hawa ni watu wenye upendeleo wa pekee machoni pa Mwenyezi Mungu na amana ya maisha ya kiroho kwa Wakristo wote. Kumbe, umoja na mshikamano wa kidugu miongoni mwa Wakristo ni changamoto fungamani na endelevu.

Kardinali Leonardo Sandri  anafafanua kwamba, Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki kunako mwaka 2017 limeadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu kuanzishwa kwake. Tukio hili likapambwa kwa Jubilei ya Miaka 25 tangu kuchapishwa kwa Gombo la Sheria za Makanisa ya Mashariki. Mwaka 2018, Shirikisho la Mashirika ya Misaada kwa Makanisa ya Mashariki, ROACO limeadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwake rasmi. ROACO ni chombo cha matumaini ya Wakristo huko Mashariki ya Kati, eneo ambalo kwa sasa limegeuka kuwa uwanja wa vita. Jubilei hii ni kipindi cha shukrani kwa Mwenyezi Mungu na wafadhili mbali mbali waliojisadaka kwa ajili ya kuwasaidia watu wa Mungu huko Mashariki ya Kati. ROACO imetoa msaada mkubwa katika ujenzi na ukarabati wa Makanisa na miundombinu ya huduma ya Injili ya upendo; imegharimia malezi na majiundo ya wakleri na watawa kutoka katika Makanisa ya Mashariki ya Kati.

Hii ni sehemu ya huduma ya maendeleo fungamani ya binadamu yanayogusa mahitaji msingi ya binadamu: kiroho na kimwili. Huu ni wakati wa kuganga na kuponya madonda ya vita, chuki na uhasama, ili kutembea katika mwanga wa umoja, upendo na mshikamano wa kidugu! Kuhusu uhuru wa kidini Kardinali Leonardo Sandri  anakaza kusema, Vatican inapenda kuchangia mambo muhimu yafuatayo  ili kukuza na kudumisha uhuru wa kidini: Kwanza kabisa: Wamini wa dini mbali mbali wanapaswa kuheshimiana, kuthaminiana, kulindana na kusaidiana kwa hali na mali pamoja na ushiriki mkamilifu katika maisha ya kisiasa, kijamii na kiuchumi ili kuhakikisha kwamba haki, amani na maridhiano vinatawala miongoni mwa watu! Pili: Utawala wa sheria, usawa wa watu wote mbele ya sheria ni muhimu sana katika kukuza na kudumisha haki msingi za binadamu na kwamba, uhuru wa kidini hauna budi kutambuliwa na kudumishwa na wote bila ubaguzi!

Baba Mtakatifu Francisko anasikitika kusema kwamba, kuna baadhi wafanyabiashara haramu wa silaha wanaotumia mianya ya kinzani na mipasuko ya kidini kama chambo cha kujitafutia faida kubwa na matokeo yake ni mauaji kwa misingi ya kidini. Ikiwa kama kuna uzalishaji, usambazaji hatimaye, matumizi ya silaha hizi ni vigumu sana kwa amani na utulivu kupatikana huko Mashariki ya Kati. Leo hii watu wengi wana kiu ya haki, amani na utulivu wa ndani. Bado kuna watu wanaoteseka kutokana na vita, majanga asilia, umaskini na magonjwa. Biashara haramu ya silaha duniani, inaendelea kubomoa furaha ya maisha kwa kupandikiza utamaduni wa kifo; uchu wa mali, madaraka na utajiri wa haraka haraka! Kumbe, kuna umuhimu kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kujibidisha kutafuta na kudumisha amani, utu na heshima ya binadamu!

Baba Mtakatifu anasema, amani maana yake ni msamaha, toba na wongofu wa ndani. Ni matunda ya sala na mshikamano na Mwenyezi Mungu anayetaka kuganga na kuponyesha madonda ya ndani. Amani maana yake ni ukarimu, utayari, uwajibikaji na majadiliano katika ukweli na uwazi, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi! Amani inajikita katika umoja, ushirikiano na mshikamano wa dhati, kwa kuthaminiana na kuheshimiana kama ndugu, ili kuitengeneza dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Amani ni elimu inayofumbatwa katika sanaa ya umoja, ili kujenga utamaduni wa watu kukutana, kwa kutakasa dhamiri dhidi ya mambo yanayokwenda kinyume cha mapenzi ya Mungu; utu, heshima na haki msingi za binadamu!

Haya ndiyo yaliyokuwa matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku ya Sala ya Kiekumene kwa ajili ya Kuombea Amani huko Mashariki ya Kati iliyofanyika huko Bari, Kusini mwa Italia. Changamoto ya wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji ni mwaliko kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuonesha mshikamano wa umoja, udugu na upendo. Vatican inapenda kuipongeza Nchi ya Lebanon ambayo imekuwa kweli ni maabara ya majadiliano ya kidini na kisiasa, umoja na udugu na ukarimu. Ni matumaini ya Kardinali Leonardo Sandri  kwamba, usalama, amani na utulivu vitaweza kurejea tena nchini Siria na Iraq, ili wananchi waliokimbia nchini mwao, waweze kurejea tena na kuanza ujenzi wa nchi yao kwa kuzingatia uhuru wa kuabudu, utu na heshima ya binadamu!

Baraza la Kipapa: Mashariki

 

14 March 2019, 12:11