Tafuta

Vatican News
Famasia ya Vatican imezindua na kubariki eneo jipya kwa ajili ya huduma ya dawa kwa wagonjwa. Famasia ya Vatican imezindua na kubariki eneo jipya kwa ajili ya huduma ya dawa kwa wagonjwa.  (Vatican Media)

Famasia ya Vatican yafungua eneo jipya kwa ajili ya huduma!

Lengo ni kuhakikisha kwamba, Kanisa linaendelea kutoa huduma bora na yenye ufanisi, ili kuzuia na kutibu magonjwa yanayomwandama mwanadamu! Ni katika muktadha huu, Famasia ya Vatican inayojivunia wa kutoa dawa bora zaidi imeboresha huduma yake kwa kufungua eneo jipya ambalo limebarikiwa, tarehe 8 Machi 2019 na Kardinali Giuseppe Bertello, Rais wa mji wa Vatican.

Na Padre Richard A. Mjigwa, - Vatican.

Huduma kwa wagonjwa na wale wote wanaoteseka ni utekelezaji wa Injili ya upendo na huruma ya Mungu kwa watu wote inayomwilishwa katika huduma makini. Hii sehemu ya mchakato wa kutangaza, kushuhudia na kujenga Ufalme wa Mungu kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko kama alivyofanya Msamaria mwema. Kumbe, ni wajibu wa waamini pamoja na wahudumu katika sekta ya afya kuhakikisha kwamba, wanakuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa wagonjwa.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Siku ya Wagonjwa kwa Mwaka 2019 anasema, sadaka na majitoleo ya waamini ni chachu muhimu sana ya uinjilishaji. Hapa ndiyo mahali ambapo tasaufi ya Msamaria mwema inapaswa kumwilishwa katika huduma kwa wagonjwa, kwa kuzingatia na kudumisha haki zao msingi, utu na heshima yao kama binadamu. Kuna haja kwa jamii kuendeleza sera na mikakati ya kuzuia na kutibu magonjwa kwa wakati muafaka; mambo ambayo yanapaswa kuwa ni sehemu ya vinasaba vya huduma kwa wagonjwa.

Miundo mbinu ya huduma kwa wagonjwa inayomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki: vijijini na mijini, iendelee kuboreshwa kwa kusoma alama za nyakati. Lengo ni kuhakikisha kwamba, Kanisa linaendelea kutoa huduma bora na yenye ufanisi, ili kuzuia na kutibu magonjwa yanayomwandama mwanadamu! Ni katika muktadha huu, Famasia ya Vatican inayojivunia wa kutoa dawa bora zaidi imeboresha huduma yake kwa kufungua eneo jipya ambalo limebarikiwa, tarehe 8 Machi 2019 na Kardinali Giuseppe Bertello, Rais wa mji wa Vatican.

Tukio hili limehudhuriwa na viongozi kadhaa kutoka Sekretarieti kuu ya Vatican na wafanyakazi wa Famasia ya Vatican chini ya uongozi wa Br. Binish Thomas Mulackal, Mkurugenzi mkuu wa Famasia ya Vatican inayohudumiwa na Shirika la Wahudumu wa Hospitali la Mtakatifu Yohane wa Mungu, maarufu kama “Fatebenefratelli” ambalo baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni amelitaka kujikita katika mambo makuu matatu: mang’amuzi; ukaribu na ukarimu pamoja na utume shirikishi! Kardinali Giuseppe Bertello, amewapongeza kwa sadaka na huduma yao makini kwa wagonjwa.

Idara ya Vipodozi imeongezwa ili kukidhi mahitaji ya wateja wake wanaotaka kuonekana nadhifu na watanashati anasema, Br. Binish Thomas Mulackal. Lengo kuu ni huduma kwa binadamu na mahitaji yake msingi kama mtu binafsi mintarafu mwelekeo wa kijamii. Huduma zinazotolewa kwenye famasia hii ni zinakidhi viwango vya ubora, utaalam na weledi unaofumbatwa katika majadiliano pamoja na usikivu kwa wateja, ili kuzima kiu ya mahitaji yao msingi.

Upanuzi huu umekuja baada ya ukarabati mkubwa kufanyika katika kipindi cha miaka kumi iliyopita. Huduma inayotolewa kwenye Famasia ya Vatican inazingatia upendo na huduma kwa jirani; kanuni maadili ya Kanisa pamoja na majitoleo ya Kikristo! Famasia ya Vatican ilizundiliwa kunako mwaka 1874 ili kutoa huduma ya dawa kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro pamoja na wasaidizi wake na Shirika la Wahudumu wa Hospitali la Mtakatifu Yohane wa Mungu, maarufu kama “Fatebenefratelli” likapewa dhamana hii ambayo bado linaendeleza hadi wakati huu kwa kuzingatia: ubora, huduma ya ushauri nasaha na ufanisi zaidi!

Famasia Vatican
09 March 2019, 15:26