Tafuta

Kardinali Angelo De Donatis: Padre ni shuhuda na chombo cha huruma ya Mungu, mwaliko kwa Mapadre kukimbilia huruma ya Mungu katika maisha yao! Kardinali Angelo De Donatis: Padre ni shuhuda na chombo cha huruma ya Mungu, mwaliko kwa Mapadre kukimbilia huruma ya Mungu katika maisha yao! 

Mapadre ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu!

Maadhimisho ya Kipindi cha Kwaresima kwa Wakleri ni muda muafaka wa kuambata toba, wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha, ili kukuza na kudumisha ari na mwamko mpya wa wito na maisha ya Kipadre, yanayojikita katika huduma makini kwa kumfuasa Kristo Yesu, mchungaji mwema: katika ukweli, uwazi na unyoofu wa maisha. Mapadre ni vyombo vya huruma ya Mungu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Wakleri wanakumbushwa kwamba, kabla hata ya kuwekewa mikono na kuwa ni: Mashemasi, Mapadre na Maaskofu,  wao kimsingi ni: waamini waliobatizwa kwa maji na Roho Mtakatifu na kwamba, utambulisho wao wa kwanza ni waamini na wafuasi wa Kristo Yesu. Kwa kuwekwa wakfu katika Sakramenti ya Daraja Takatifu wanakuwa ni mashuhuda, vyombo na wahudumu wa Mafumbo ya Kanisa. Kwa namna ya pekee,  ni wahudumu wa Sakramenti za huruma ya Mungu, yaani: Ekaristi Takatifu inayowajalia waamini chakula cha njiani katika hija ya maisha yao hapa bondeni kwenye machozi pamoja na Sakramenti ya Upatanisho, inayowaonjesha waamini, huruma, upendo na msamaha wa Mungu katika maisha yao, tayari hata wao kuwa ni mashuhuda wa huruma ya Mungu, inayomwilishwa katika vipaumbele vya maisha yao!

Maadhimisho ya Kipindi cha Kwaresima kwa Wakleri hasa wakati huu, baada ya Kanisa kutikiswa na kashfa ya nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo, ni muda muafaka wa kuambata toba, wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha, ili kukuza na kudumisha ari na mwamko mpya wa wito na maisha ya Kipadre, yanayojikita katika huduma makini kwa kumfuasa Kristo Yesu, mchungaji mwema: katika ukweli, uwazi na unyoofu wa maisha. Hiki ni kipindi cha kupanda kwenda mlimani, ili kusali, kutafakari na kuchunguza dhamiri, tayari kuomba toba na msamaha wa dhambi, ili kweli Wakleri hawa waweze kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu kwa waja wake.

Ni katika muktadha huu, Kardinali Angelo De Donatis, Makamu Askofu mkuu Jimbo kuu la Roma katika barua yake kwa wakleri wanaofanya utume wao Jimbo kuu la Roma, anawaalika  kuungana na Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 7 Machi 2019, majira ya Saa 3:30 kwa Saa za Ulaya, kwa ajili ya kuadhimisha Ibada ya Toba, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano. Anawakumbusha Mapadre waungamishaji kwamba, Mwenyezi Mungu aliyeupatanisha ulimwengu wote pamoja naye kwa njia ya Kristo Yesu, amewakabidhi utume huu wa kuwapatanisha watu na Mwenyezi Mungu pamoja na jirani zao. Kumbe, wao ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu, nao wanapaswa kupatanishwa na Mungu ili kweli waweze kuwa ni haki ya Mungu katika Yeye!

Ibada ya Toba na wongofu wa ndani, ni kielelezo cha nguvu kinachoonesha umoja wa viongozi wa Kanisa, ili kufanya toba, kwa kuomba huruma na msamaha wa Mungu. Kama binadamu, wanatambua unyonge na udhaifu wao na kwamba, wanaweza kusimama tena na kusonga mbele kwa neema ya upatanisho, ili kukutana tena na Baba Mwenye huruma, tayari kuwashirikisha waamini  neema ya utakaso na maondoleo ya dhambi, ili kuanza kutembea tena katika upya wa maisha katika Parokia za Jimbo kuu la Roma. Kwa msaada wa maombezi ya Bikira Maria, Malaika na Watakatifu wa Mungu, Wakleri wazidi kuombeana na kuhamasishana, kutubu na kumwongokea Mungu, ili kuonja matunda ya upatanaisho!

Huu ni wakati wa kujipatanisha na Mwenyezi Mungu, kwa kuuangalia ukweli mbele ya upendo wa Mwenyezi Mungu. Wakleri wamepewa dhamana ya kuwapeleka watu kwa Kristo; Kulinda umoja wa Jumuiya ya waamini; kwa kuganga na kuponya madonda ya mahusiano na mafungamano yaliyotibuka katika maisha! Upatanisho wa Mungu kwa njia ya Kristo Yesu katika Fumbo la Pasaka, inakuwa ni nguvu ya msamaha katika Jumuiya kwa ndugu kujifunza kujisadaka kwa ajili ya wengine, ili kuzama katika huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake!

Kardinali Angelo De Donatis, anasisitiza kwamba, wakleri, kamwe wasichoke kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu kwa waja wake. Utume huu, unahitaji kwa namna ya pekee kabisa fadhila ya unyenyekevu na uvumilivu, ili kuonja huruma, wema na upendo wa Mungu. Wakleri wawe wa kwanza kukimbilia huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao kama ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Mchungaji mwema anajionesha kwa namna ya pekee, katika maisha ya toba, wongofu wa ndani na msamaha wa dhambi. Kiongozi wa Kanisa awe na ujasiri wa kupiga hatua ya kwanza kumwendea Baba mwenye huruma, kwa kushikamana na ndugu zake katika Kristo! Hii ni sifa njema kwa kiongozi wa Kanisa!

Kipindi cha Kwaresima ni muda muafaka wa “Diakonia” yaani “Huduma ya Upatanisho” inayofumbatwa katika mafungo ya maisha ya kiroho na tafakari ya Neno la Mungu inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Hiki ni kipindi cha kutoa nafasi ya kumsikiliza Mwenyezi Mungu kutoka katika undani wa dhamiri zao nyoofu! Huu ni muda muafaka wa kujipatanisha na Mungu, kwa kutambua kwamba, kama binadamu bado wanaogelea katika dhambi: kwa maneno, matendo na kwa kutotimiza wajibu! Kumbe, upendo wa Kristo unawawajibisha kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani zao.

Huruma ya Mungu inajionesha katika maisha ya watu kwa kuwasaidia kutubu na kuongoka, ili hatimaye, kushirikiana na Mungu kama vyombo na mashuhuda wake. Kwa njia ya Fumbo la Pasaka, Mwenyezi Mungu ameweza kuupatanisha ulimwengu wote pamoja naye. Kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho, Mwenyezi Mungu anachukua hatua ya kwanza ili kuonesha upendo kwa mdhambi, kama ilivyo kwa Mama Kanisa kuanza kwa ushupavu kuwaendea na kuwatafauta walioanguka na kutopea dhambini, waliotengwa na kuwakaribisha tena ili kuwaonjesha mang’amuzi ya huruma na upendo wa Mungu, ambayo ni matunda ya nguvu ya Baba isiyokuwa na kikomo!

Mapadre waungamishaji wawe ni vyombo vya faraja kwa waamini wanaotubu na kumwongokea Mungu na kwamba, mang’amuzi ya Sakramenti ya Upatanisho yawaonjeshe watu upendo na huruma ya Mungu. Mapadre wawasaidie waamini kutambua udhaifu na dhambi zao, kwa kuwapokea na kuwakumbatia kama Baba Mwenye huruma, ili waamini  waweze kukutana na Mwenyezi Mungu katika undani wa maisha yao, Mungu ambaye daima ni mwingi wa huruma na mapendo!

Mwenyezi Mungu hujawa na furaha pale anapomwona mdhambi akitubu na kumwongokea. Mapadre waungamishaji wawaangalie watu kwa macho ya huruma na upendo; wawasikilize kwa saburi na unyenyekevu mkuu, ili kuwaonjesha huruma na upendo wa Mungu unaosamehe, kuganga na kuwaponya watu wake. Kwa njia hii, Mwenyezi Mungu yuko tayari kuwavika pete ya uaminifu na kuwaonesha kwamba, wao ni sehemu ya familia yake, urithi wake. Huruma inafungua malango ya matumaini, inajenga imani na kurutubisha mapendo!

Kardinali De Donatis

 

07 March 2019, 11:27