Tafuta

Vatican News
Hospitali ya Bambino Gesù, tarehe 19 Machi 2019 inaadhimisha Jubilei ya Miaka 150 ya Uwepo na utume wake kwa ajili ya watoto wagonjwa! Hospitali ya Bambino Gesù, tarehe 19 Machi 2019 inaadhimisha Jubilei ya Miaka 150 ya Uwepo na Utume wake kwa ajili ya watoto wagonjwa!  (ANSA)

Jubilei ya Miaka 150 ya Hospitali ya Bambino Gesù, Roma!

Mwaka 1924, familia ya Jacqueline Arabela de Fitz-James Salviati wamiliki wa Hospitali hii wakatoa zawadi kwa Vatican na kupokelewa na Papa Pio IX. Tangu wakati huo ikaanza kufahamika kama Hospitali ya Bambino Gesù, Hospitali ya Papa kwa ajili ya watoto wagonjwa. Huduma kwa watoto wagonjwa na maskini anasema Papa Pio XI ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Papa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Hospitali ya Bambino Gesù inayoendeshwa na kumilikiwa na Vatican, ilianzishwa kunako mwaka 1869 kama Hospitali ya kwanza kwa ajili ya watoto wagonjwa nchini Italia. Kunako mwaka 1924, familia ya Jacqueline Arabela de Fitz-James Salviati wamiliki wa Hospitali hii wakatoa zawadi kwa Vatican na kupokelewa na Papa Pio IX. Tangu wakati huo ikaanza kufahamika kama Hospitali ya Bambino Gesù, Hospitali ya Papa kwa ajili ya watoto wagonjwa. Huduma kwa watoto wagonjwa na maskini anasema Papa Pio XI ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Huduma inayotolewa Hospitalini hapo inawalenga watoto wagonjwa pamoja na familia zao. Hii ni Hospitali ambayo imegawanyika katika maeneo makubwa manne: Makao makuu ya Hospitali, Kituo cha “San Paolo”, Kituo cha Palidoro pamoja na “Santa Marinella”. Jumla Hospitali ina vitanda 607 na ina uwezo wa kulaza wagonjwa 27, 000 kwa Mwaka. Hospitali ina uwezo wa kupandikiza viungo kwa wagonjwa 339. Wagonjwa 44, 000 wanahudumiwa katika “Day Hospital”. Familia 3700 zinapata huduma kwa gharama nafuu na kwamba, asilimia 13% ya watoto wagonjwa wanaohudumiwa hapa ni kutoka nje ya Italia. Hawa ni watoto wanaotoka katika maeneo ya vita, nchi maskini zaidi duniani; watoto ambao wanahitaji kupata huduma ya tiba kwa muda mrefu zaidi. Hospitali ya Bambino Gesù inashirikiana kwa karibu zaidi na Hospitali zinazoendeshwa na Makanisa, sehemu mbali mbali za dunia!

Barani Afrika, inashirikiana pia na Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Gaspar, Itigi, Manyoni, Singida nchini Tanzania pamoja na Hospitali ya Watoto Wadogo Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati! Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Siku ya Wagonjwa Duniani 2019 anasema, Huduma kwa wagonjwa na wale wote wanaoteseka ni utekelezaji wa Injili ya upendo na huruma ya Mungu kwa watu wote. Ni sehemu ya mchakato wa kutangaza, kushuhudia na kujenga Ufalme wa Mungu kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko kama alivyofanya Msamaria mwema. Kumbe, ni wajibu wa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma na upendo wa Mungu kwa wagonjwa, maskini na wale wote wanaoteseka. Baba Mtakatifu anawataka watu wamwone Kristo Yesu anayeendelea kuteseka kati pamoja na wagonjwa, maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Historia ya Hospitali
19 March 2019, 16:17