Tafuta

Vatican News
Jubilei ya Miaka 150 ya Hospitali ya Bambino Gesù: Kanisa kuendelea kuwekeza katika huduma kwa wagonjwa na maskini duniani! Jubilei ya Miaka 150 ya Hospitali ya Bambino Gesù: Kanisa kuendelea kuwekeza katika huduma kwa wagonjwa na maskini duniani!  (ANSA)

Miaka 150 ya Hospitali ya Bambino Gesù, Roma: Watoto na maskini

Licha ya maboresho katika sekta ya afya, bado Kanisa litaendelea kuwekeza katika huduma kwa wagonjwa, kama sehemu ya utekelezaji wa dhamana na utume wake wa kinabii, kwa ajili ya maskini wapya katika sekta ya afya! Yaani: wagonjwa wanaosumbuliwa na magonjwa sugu; magonjwa nasibu, wagonjwa wa afya ya akili, wazee na maskini wanaoteseka kupata huduma bora ya tiba.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 150 ya Hospitali ya Bambino Gesù inayomilikiwa na kuendeshwa na Vatican ni kipindi muafaka cha kuyatafakari yaliyopita kwa moyo wa shukrani, kuyaishi ya sasa kwa moyo wa hamasa na kuyakumbatia ya mbeleni kwa moyo wa matumaini! Huu ni muda wa kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa wale wote waliojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa watoto wagonjwa. Ni muda wa kuimarisha umoja, upendo na mshikamano wa dhati, kama utambulisho wa maisha na utume ya Hospitali ya Bambino Gesù.

Ikumbukwe kwamba, utambulisho huu unapata chimbuko lake kutoka katika Injili ya huruma ya Mungu, “nilikuwa mgonjwa, mkaja kunitazama”. Haya ni matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kielelezo cha imani tendaji. Hii ndiyo changamoto changamani ambayo imefanyiwa kazi na Mama Kanisa kwa kuanzisha vituo vya huduma kwa ajili ya wagonjwa na maskini, kama sehemu ya utekelezaji wake wa utume wa kinabii: kwa kusoma alama za nyakati, kusikiliza na hatimaye, kujibu kilio cha maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii mintarafu mwanga wa Injili.

Uwepo na utume wa Hospitali ya Bambino Gesù ni ndoto ya upendo, kielelezo cha upendo unaowawezesha waamini kuona, ili kutambua na kung’amua tayari kujizatiti kutoa msaada, kama jibu makini kwa mahitaji ya watu kwa nyakati hizi na hata kwa siku za mbeleni! Ndoto ya upendo inawawajibisha waamini kutoa huduma makini, kujenga uwezo wa ujirani mwema na mshikamano na wale wote wanaoteseka, kielelezo makini cha udugu na mshikamano wa dhati! Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, Jumatatu, tarehe 19 Machi 2019, wakati wa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 150 ya Hospitali ya Bambino Gesù.

Tukio hili limehudhuriwa pia na viongozi waandamizi kutoka Serikali ya Italia chini ya uongozi wa Rais Sergio Mattarella pamoja na viongozi wa Kanisa kutoka Italia. Kardinali Parolin anakaza kusema, historia ya Hospitali ya Bambino Gesù ni maono ya watu yanayomwilishwa katika mradi unaoishirikisha jamii na hatimaye, kuupatia utambulisho wake kama kielelezo cha upendo na mshikamano kwa ajili ya wagonjwa hata kwa siku za mbeleni! Historia ya huduma ya afya imebadilika sana nchini Italia, ikilinganishwa na miaka 150 iliyopita wakati Hospitali hii ikianzishwa. Huduma za Afya Kitaifa zimeendelea kuimarishwa, kwa kujikita katika usawa unaofafanuliwa kwenye Katiba ya Italia, ili kulinda na kudumisha uhai!

Ubora wa huduma inayotolewa unapaswa kulinda na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu katika ukweli wake wote: katika: hisia, mahusiano, kisaikolojia na katika maisha ya kiroho. Hospitali hii, katika historia yake, kuanzia mwaka 1985 imeendelea kujipambanua kuwa ni Kituo cha Tafiti za Kimataifa, huduma ambayo inatambuliwa ulimwenguni kote! Hospitali hii ni Kituo Kikuu cha Tafiti za Magonjwa ya Watoto Barani Ulaya. Hatua hii imeweza kufikiwa kutokana na Kanisa kuendelea kuwekeza zaidi katika tafiti za kisayansi, miundo mbinu, teknolojia pamoja na katika rasilimali watu, kama njia ya kukabiliana na changamoto changamani kwa siku za usoni.

Licha ya maboresho katika sekta ya afya, bado Kanisa litaendelea kuwekeza katika huduma kwa wagonjwa, kama sehemu ya utekelezaji wa dhamana na utume wake wa kinabii, kwa ajili ya maskini wapya wanaoendelea kujitokeza katika sekta ya afya! Hawa ni wagonjwa wanaosumbuliwa na magonjwa ya kudumu; wagonjwa wa magonjwa nasibu, wagonjwa wa afya ya akili, wazee na maskini wanaoteseka kupata huduma bora ya tiba. Wote hawa wanapaswa kupewa kipaumbele cha pekee pamoja na kuzishirikisha familia husika, ili hatimaye, kujenga mtandao wa mshikamano katika huduma, ili kuimarisha imani, urafiki na udugu!

Hii ni Hospitali inayotekeleza dhamana na wajibu wake, ndani na nje ya Italia kama kielelezo cha Ukatoliki wa Kanisa linaloangalia pia watoto maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Utume huu kama unavyojulikana “ubi amor ibi oculos” unaiwezesha Hospitali kushirikishana ujuzi na maarifa; majiundo ya kitaaluma pamoja na kusindikizana kama inavyojionesha katika ujenzi na hatimaye, ufunguzi wa Hospitali ya Watoto Wadogo, huko Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati. Hospitali hii ni shuhuda wa umoja na upendo kati ya watu wa Mungu! Huu ndio upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake!

Hospitali ya Bambino Gesù
19 March 2019, 16:51