Kardinali Pietro Parolin: Hijna ya Papa Francisko nchini Morocco inajikita katika mambo makuu matatu: Majadiliano ya kidini, Udugu wa kibinadamu na Ushuhuda wa imani kwa Kristo na Kanisa lake. Kardinali Pietro Parolin: Hijna ya Papa Francisko nchini Morocco inajikita katika mambo makuu matatu: Majadiliano ya kidini, Udugu wa kibinadamu na Ushuhuda wa imani kwa Kristo na Kanisa lake. 

Hija ya Papa Francisko Morocco: Majadiliano, Udugu na Ushuhuda!

Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican anasema, Baba Mtakatifu Francisko anafanya hija hii kama hujaji wa amani, udugu na mahudumu wa matumaini! Hija hii inajikita katika mambo makuu matatu: majadiliano ya kidini; huduma kwa maskini yaani wakimbizi na wahamiaji pamoja ushuhuda wa imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, kutoka kwa waamini nchini Morocco!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko kuanzia Jumamosi tarehe 30 hadi Jumapili tarehe 31 Machi 2019 anafanya hija ya 28 ya kimataifa nchini Morocco kwa kuongozwa na kauli mbiu “Papa Francisko mhudumu wa matumaini Morocco 2019”. Baba Mtakatifu anafanya hija hii kama hujaji wa amani, udugu na mahudumu wa matumaini! Hija hii inajikita katika mambo makuu matatu: majadiliano ya kidini; huduma kwa maskini yaani wakimbizi na wahamiaji pamoja ushuhuda wa imani kutoka kwa waamini nchini Morocco!

Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican katika mahojiano maalum na Vatican News kama sehemu ya maandalizi ya hija hii ya kitume anasema, Baba Mtakatifu anataka kujenga, kukuza na kudumisha utamaduni wa watu kukutana katika huduma ya matumaini! Lengo ni kukabiliana na changamoto ya utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine kutokana na kukithiri kwa ubinafsi na uchoyo; hali ya kujitafuta wenyewe pamoja na kuendekeza misigano na mipasuko ya kijamii kwa ajili ya kudumisha masilahi ya watu binafsi!

Ili kuweza kukabiliana na changamoto hizi zote, Baba Mtakatifu Francisko anawahimiza waamini wa dini mbali mbali kujenga utamaduni wa kukutana, kusaidiana na kushirikishana tunu msingi za maisha, katika ukweli na uwazi; kwa kuheshimiana na kuthaminiana kama ndugu wamoja! Kardinali Parolin anakaza kusema, hija hii ni mwendelezo wa mchakato wa majadiliano ya kidini kama sehemu ya ujenzi wa udugu wa kibinadamu, kama ile iliyofanyika kwenye Umoja wa Falme za Kiarabu.

Lengo ni kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini na maridhiano kati ya Waislam na Wakristo! Ili kusonga mbele anasema Kardinali Parolin, kuna haja ya kuwa na imani, matumaini na mapendo! Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake, amekwisha kutembelea nchi nyingi zenye waamini wengi wa dini ya Kiislam, ili kukuza mchakato wa majadiliano ya kidini na ujenzi wa udugu wa kibinadamu. Udugu huu ni msingi wa umoja na mshikamano, ili kukuza na kudumisha: haki, amani na mardhiano kati ya watu, chachu muhimu sana katika mchakato wa maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu!

Kardinali Parolin anakaza kusema, haya ni mambo msingi yanayofumbatwa katika Hati ya Udugu wa Kibinadamu, iliyotiwa mkwaju kati yake na Dr. Ahmad Al-Tayyib, Imam Mkuu wa Msikiti wa Al- Azhar, ulioko Kairo, nchini Misri, Jumatatu, tarehe 4 Februari 2019 huko Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu. Viongozi wa kidini wanakiri kwa pamoja wito wa watu wote kwamba, wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu; wote ni watoto wa Baba mmoja! Kwa nguvu zote viongozi hawa wa kidini wanalaani vitendo vyote vinavyosababisha vita na ghasia hasa zile zinazofumbatwa katika misingi ya udini. Kwa pamoja wanataka kusimama kidete kutangaza na kushuhudia tunu msingi za maisha ya kiroho na amani duniani. Udugu wa kibinadamu ni tema endelevu katika hija hizi za Baba Mtakatifu katika nchi za Kiislam!

Mkataba wa Kimataifa wa Usalama wa Wahamiaji 2018 “Global Compact 2018” ulitiwa mkwaju huko Marrakesh, Morocco. Huu ni Mkataba ulioandaliwa na Umoja wa Mataifa unalenga kuratibu na kuboresha mchakato wa wahamiaji na wakimbizi duniani, ili kulinda na kudumisha haki msingi, utu na heshima ya wahamiaji! Unakazia umuhimu wa Jamii kusikiliza na kujibu kilio cha wakimbizi na wahamiaji duniani; kwa kukusanya maoni; kwa kupunguza gharama za kuwahudumia wahamiaji sanjari na kudumisha usalama na maisha bora zaidi. Mkataba unapania pamoja na mambo mengine, kuboresha: ulinzi na usalama; haki msingi za binadamu pamoja na wakimbizi kupatiwa huduma ya msaada wa kisheria pale haki zao zinapovunjwa.

Mkataba huu unawatupia jicho wakimbizi na wahamiaji hatari kwa maisha na usalama wa raia wengine. Watu hatari wanaweza kurejeshwa makwao pamoja na  uwezekano wa kudhibiti uhuru wa wakimbizi. Unataka kukomesha ubaguzi na maamuzi mbele; kuongeza fursa za ushirikishwaji wa wahamiaji katika maisha ya nchi wahisani; kupunguza gharama za kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji ambazo kwa sasa umekuwa ni mzigo mkubwa kwa baadhi ya serikali pamoja na kuangalia umuhimu wa kutumia nguvu ya wakimbizi katika kuzalisha na kutoa huduma, mwishoni ni suala la udhibiti wa mipaka!

Kanisa Katoliki katika sera na mikakati yake kuhusu huduma kwa wakimbizi na wahamiaji linapenda kukazia kwa namna ya pekee umuhimu wa: “Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji” katika maisha ya jamii inayowakirimia. Baba Mtakatifu Francisko, tangu mwanzo wa utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, ameguswa sana na matatizo na changamoto zinazowakabili wakimbizi na wahamiaji sehemu mbali mbali za dunia. Hawa ni watu wanaokimbia vita, dhuluma, nyanyaso, majanga asilia na umaskini, changamoto na mwaliko kwa familia ya binadamu kusoma alama za nyakati.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Ekaristi takatifu ni shule ya upendo, ukarimu, umoja na mshikamano wa dhati. Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya Upendo; zawadi na sadaka ya Kristo Yesu Msalabani; kielelezo cha huduma inayomwilishwa na kuwasha mapendo kwa Mungu na jirani. Ni Sakramenti ya Altare, mahali pa kukutana mubashara na Kristo Yesu katika maumbo ya Mkate na Divai; Mwili na Damu yake Azizi. Kumbe, maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, yatakuwa ni kilele cha hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Morocco. Hii ni fursa ya kuwaimarisha ndugu zake katika imani, matumaini na mapendo anasema Kardinali Parolin.

Familia ya Mungu nchini Morocco, inatarajiwa kushiriki kikamilifu katika Ibada hii ya Misa Takatifu, kielelezo cha umoja na mshikamano na Khalifa wa Mtakatifu Petro; umoja na upendo kati ya Kanisa mahalia na Kanisa la Kiulimwengu. Kardinali Parolin anasema, Baba Mtakatifu anapenda kuwaimarisha Wakristo nchini Morocco, ili kuwa ni vyombo, mashuhuda na wahudumu wa Injili inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha yao ya kila siku! Kwa njia hii, watashiriki kuchangia: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi nchini Morocco!

kardinali Parolin: Morocco
29 March 2019, 16:53