Tafuta

Vatican News
Biashara ya binadamu na utumwa mamboleo ni uhalifu dhidi ya utu na heshima ya binadamu! Biashara ya binadamu na utumwa mamboleo ni uhalifu dhidi ya utu na heshima ya binadamu! 

Mapambano dhidi ya biashara na utumwa mamboleo duniani

Askofu Mkuu Auza anasema, kuna haja ya kwa Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete ili kutokomeza: kazi za suluba, biashara ya binadamu na mifumo yote ya utumwa mamboleo; nyanyaso na dhuluma dhidi ya wanawake na wasichana; mambo ambayo yanazidi kuongezeka kila kukicha! Waathirika wa biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo, wanapaswa kuwezeshwa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Wanawake na wasichana wanapaswa kuwezeshwa kiuchumi, kulindwa pamoja na kupatiwa huduma msingi za kijamii, ili kukoleza mchakato wa ujenzi wa jamii inayosimikwa katika usawa na haki msingi. Lengo liwe ni ustawi, maendeleo na mafao ya wengi kama njia muafaka ya kuweza kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu na fungamani ya binadamu ifikapo mwaka 2030. Kati ya mambo haya ni kuhakikisha kwamba, wanawake pia wanapewa nafasi ya kumiliki ardhi kama rasilimali na mtaji; wajengewe uwezo wa kifedha kwa kuwapatia mikopo midogo midogo ili kuinua hali ya maisha na uchumi wa kaya zao!

Juhudi hizi hazina budi kwenda sanjari na ubora unaotolewa katika sekta ya elimu na afya; kwa kuzingatia pia ulinzi na usalama pamoja na uwezo wa wanawake na wasichana kugharimia huduma hizi! Wanawake wapewe fursa sawa katika masuala ya ajira pamoja na kulipwa sawa bila ubaguzi wala upendeleo, ili kudumisha haki kwa wote. Huu ni mchango ulitolewa hivi karibuni na Askofu Mkuu Bernardito Auza, Mwakilishi wa Kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa, alipokuwa akichangia hoja kuhusu mapambano dhidi ya biashara haramu ya binadamu na mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo; inayodhalilisha utu, heshima na haki msingi za binadamu!

Askofu Mkuu Auza anasema, kuna haja ya kwa Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete ili kutokomeza: kazi za suluba, biashara ya binadamu na mifumo yote ya utumwa mamboleo; nyanyaso na dhuluma dhidi ya wanawake na wasichana; mambo ambayo yanazidi kuongezeka kila kukicha! Waathirika wa biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo, wanapaswa kuwezeshwa, ili kuanza kuandika tena ukurasa mpya wa maisha yao! Vatican itaendelea kushirikiana na wadau mbali mbali ili kupambana na biashara ya binadamu pamoja na utumwa mamboleo.

Kanisa tayari limekwisha kutoa Mwongozo kwa ajili ya kupambana na biashara ya binadamu na utumwa mamboleo. Mkazo katika Mwongozo huu kwanza kabisa ni kusaidia kulipa deni la wahusika, kuwapatia nafasi ya kujifunza kazi pamoja na kuwapatia kazi itakayowawezesha kuwa na kipato chenye uhakika pamoja na kuwa na makazi bora zaidi. Huduma kwa waathirika wa biashara ya binadamu na utumwa mamboleo ni mchakato unaowashirikisha wadau wengi, kumbe, washirikiane, ili kulinda utu na heshima ya wanawake!

Wanawake

 

 

19 March 2019, 11:03