Askofu mkuu Protase Rugambwa amewataka watanzania kujenga na kudumisha umoja wa kitaifa, sehemu muhimu sana ya utambulisho wao! Askofu mkuu Protase Rugambwa amewataka watanzania kujenga na kudumisha umoja wa kitaifa, sehemu muhimu sana ya utambulisho wao! 

Askofu mkuu Rugambwa: Jengeni na kudumisha umoja wa kitaifa!

Askofu mkuu Protase Rugambwa amewataka watanzania wanaoishi na kusoma mjini Roma kujenga na kuimarisha umoja, upendo na mshikamano wa dhati kama sehemu ya utambulisho wao kitaifa. Wakuze na kudumisha dhana ya uongozi shirikishi, ili kushirikishana tunu na karama mbali mbali kutoka kwa Roho Mtakatifu, kwa ajili ya mafao, ustawi na maendeleo ya wengi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Askofu mkuu Protase Rugambwa, Katibu wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu, Jumapili, tarehe 24 Machi 2019 amewataka watanzania wanaoishi na kusoma Roma kujenga na kudumisha: umoja, upendo na mshikamano wa kitaifa, mambo msingi yanayowatambulisha watanzania, licha ya tofauti zao msingi. Amewataka viongozi kukuza na kudumisha dhana ya uongozi shirikishi, wao wakiwa mstari wa mbele kujisadaka na kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watanzania wanaoishi mjini Roma!

Askofu mkuu Rugambwa ametoa nasaha hizi kwa Jumuiya ya Watanzania wanaoishi na Kusoma mjini Roma baada ya Misa Takatifu na kufuatiwa na uchaguzi wa viongozi wapya ambao wamepewa dhamana kwa kipindi cha mwaka 2019-2020. Waliochaguliwa ni Padre Paschal Ighondo, Mwenyekiti; Padre Onesmus Komba, Katibu, Sr. Generosa J. Mwaghui, Mtunza hazina, Padre Angelo Shikombe, Mwongoza Ibada pamoja na Padre Thomas Mushi ambaye amechaguliwa kuwa Mkutubi. Askofu mkuu Rugambwa amewashukuru viongozi waliomaliza muda wao kwa kujenga na kudumisha: umoja, upendo na mshikamano wa kitaifa. Viongozi wamekumbushwa kwamba, uongozi ni huduma inayofumbatwa katika: upendo, sadaka na unyenyekevu mkuu.

Changamoto iliyoko mbele ya uongozi mpya wa Umoja wa Watanzania wanaosoma na kuishi Roma ni kuhakikisha kwamba, wanajenga na kuimarisha umoja na mshikamano kati ya: wakleri, watawa, waseminaristi pamoja na waamini walei wanaoishi na kufanya shughuli zao mjini Roma, ili kudumisha umoja na mshikamano wa watanzania wote. Haya ndiyo matamanio makubwa hata kwa Ubalozi wa Tanzania nchini Italia. Askofu mkuu Protase Rugambwa, aliwashukuru na kuwapongeza watanzania waliohudhuria mkutano kama huu mwezi Novemba 2018. Utambulisho wa watanzania unajikita katika: umoja, upendo, amani na mshikamano wa kitaifa.

Itapendeza na kuvutia sana, ikiwa kama familia ya Mungu kutoka Tanzania katika ujumla wake, ikakutana kumshukuru Mungu kwa wema, upendo na ukarimu wake katika maisha yao; au kushikana mkono wakati shida na majonzi; wakati wa raha na shida. Askofu mkuu Rugambwa amekazia sana kuhusu dhana ya uongozi shirikishi katika maisha na utume wa Kanisa, kwani uongozi unapaswa kuwa ni huduma shiriki. Kwanza kabisa wale waliopewa dhamana na wajibu huu wanapaswa kujisadaka bila ya kujibakiza, huku wakisaidiwa na ndugu zao, ambao wao pia wanapaswa kuchangia: uwepo na karama zao. Watu wasiogope kukubali kuchukua dhamana ya uongozi kwa kutambua kwanza kabisa hii ni huduma. Kumbe, umoja na mshikamano miongoni mwa watanzania, uwe ni kikolezo cha Jumuiya ya Watanzania kusonga mbele.

Watanzania Roma 2019
26 March 2019, 10:36