Tafuta

Siku ya Elimu Duniani 2019: Elimu isaidie mchakato wa ujenzi wa amani na maendeleo fungamani ya binadamu! Siku ya Elimu Duniani 2019: Elimu isaidie mchakato wa ujenzi wa amani na maendeleo fungamani ya binadamu! 

Siku ya Elimu Duniani 2019: Amani na maendeleo fungamani!

Elimu isaidie “kuonesha” watu njia ili kuwaondoa katika giza la ujinga na kuwapeleka katika mwanga wa maarifa, ukuaji na ukomavu. Elimu iwasaidie watu kuwa bora zaidi, kwa kuwaunda na kuwafunda katika maadili, tabia na utu wema. Shule ziwe ni mahali pa kurithisha kanuni maadili ili jamii iweze kupata wasomi watakaolinda na kudumisha uhai dhidi ya utamaduni wa kifo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Elimu ni kati ya haki msingi za kibinadamu, ni sehemu ya mafao ya wengi na inawajibisha. Ni kutokana na umuhimu wa elimu katika jamii, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, mwezi Desemba 2018 likaazimia kuanzishwa kwa Siku ya Elimu Duniani, itakayokuwa inasherehekewa kila mwaka ifikapo tarehe 24 Januari. Askofu mkuu Bernadito Auza, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa anasema, Jumuiya ya Kimataifa imekuwa ikiadhimisha Siku 158 za Kimataifa kwa kujikita katika medani mbali mbali za maisha.

Siku ya Elimu Duniani inajumuisha sekta nzima ya elimu kama nguzo ya maendeleo fungamani na sehemu ya mchakato wa ujenzi pamoja na kudumisha amani na usalama. Baba Mtakatifu Francisko amekuwa akikazia umuhimu wa elimu kwa wote kama njia ya kupambana na umaskini wa hali na kipato; pamoja na kudumisha utu na heshima yao. Umoja wa Mataifa katika Lengo lake la Nne anasema Askofu mkuu Auza ni: kuhakikisha kwamba, kunakuwepo na elimu bora, yenye usawa na kutoa fursa kwa watu wote kujiendeleza.

Lengo hili linasisitiza kuwezesha kila mtu kusoma, kujifunza na kuhakikisha kwamba, binadamu wote wanafikia vipawa vyao kikamilifu. Kuhakikisha kuwa wasichana na wavulana wote wanahitimu elimu ya msingi na sekondari; bure, yenye ubora na usawa unaoleta tija. Kuongeza mahudhurio ya wanafunzi shuleni. Kuhakikisha kuwa wasichana na wavulana wote wana fursa sawa ya kupata elimu bora ya awali ili iwaandae kwa elimu ya msingi.

 

Kuhakikisha fursa sawa kwa wanawake na wanaume ili wapate elimu ya juu, mafunzo na ufundi stadi kwa gharama nafuu. Kuongeza idadi ya vijana na watu wazima wenye ujuzi pamoja na ufundi stadi kwa ajili ya ajira, kazi zenye heshima na ujasiriamali. Kuondoa matabaka ya kijinsia ndani ya elimu na kuhakikisha upatikanaji wa elimu katika ngazi zote ikiwemo mafunzo ya ufundi stadi kwa ajili ya watu wanaoishi katika maeneo hatarishi hususani, wenye ulemavu na watoto.

Lengo la Umoja wa Mataifa ni kubainisha na kuendeleza dhamana ya elimu kama sehemu ya mchakato wa maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu: kiutu na kijamii. Baba Mtakatifu anapenda kuchukua fursa hii, kulihamasisha Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa, UNESCO kukuza na kudumisha juhudi hizi, ili amani iweze kutawala duniani kwa njia ya elimu. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, watu wote watakuwa na fursa ya kupata elimu ambayo kimsingi inapaswa kuwa fungamani na huru dhidi ya ukoloni wa kiitikadi. Baba Mtakatifu anawatakia waalimu wote kazi njema katika kurithisha ujuzi, maarifa na stadi za maisha katika jamii!

Askofu mkuu Bernadito Auza anasikitika kuona kwamba, kuna watoto zaidi ya milioni 120 sehemu mbali mbali za dunia, hawana fursa ya kupata elimu ya msingi na sekondari. Kuna watoto milioni 130 wanaosomea katika mazingira duni sana, kiasi cha kushindwa kufaidika na elimu inayotolewa. Kanisa Katoliki sehemu mbali mbali za dunia limekuwa ni mdau mkubwa wa elimu, licha ya matatizo na changamoto linazokabiliana nazo. Kanisa linamiliki kiasi cha shule 220, 000 kwa kiwango ya elimu ya awali hadi taasisi za elimu ya juu.

Taasisi hizi zinatoa fursa ya elimu kwa watoto na vijana zaidi ya milioni 65 na kwamba, kuna maelfu ya vijana wanaopata elimu katika vyuo vya ufundi pamoja na vyuo vikuu vya kikatoliki. Hii ni huduma inayotolewa kwa watu wote bila upendeleo. Shule zinazomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki zinapania kwanza kabisa kumkomboa mwanadamu: kiroho na kimwili; kwa kuwapatia wazazi na walezi fursa ya watoto wao kupata malezi na elimu bora zaidi itakayowawezesha kupambana na hali pamoja na mazingira yao kwa kuwajengea leo na kesho yenye matumaini zaidi.

Askofu mkuu Bernadito Auza anakazia umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kuwekeza zaidi katika ubora wa elimu inayotolewa kwa kuzama zaidi katika maana ya neno elimu katika mzizi wake kwa lugha ya Kilatini, yaani “Edùcere”, yaani “kuonesha” watu njia ili kuwaondoa katika giza la ujinga na kuwapeleka katika mwanga wa maarifa, ukuaji na ukomavu. Elimu iwasaidie watu kuwa bora zaidi, kwa kuwaunda na kuwafunda katika maadili, tabia na utu wema. Shule zinapaswa kuwa ni mahali pa kurithisha kanuni maadili mema, ili jamii iweze kupata wasomi watakaolinda na kudumisha uhai wa binadamu dhidi ya utamaduni wa kifo.Elimu iwasaidie watu kuwa wema zaidi na kamwe shule na taasisi za elimu zisiwe ni mahali pa kuzalishia watu hatari katika jamii. Maadhimisho ya Siku ya Elimu Duniani iwe ni fursa ya kuihamasisha Jumuiya ya Kimataifa kutoa kipaumbele cha pekee katika elimu; kwa kuzingatia haki elimu yenye viwango na ubora wa hali ya juu, tayari kuwafunda vijana kuwa ni wadau wa maendeleo fungamani, vyombo na wajenzi wa amani duniani!

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres  katika maadhimisho ya Siku ya kwanza ya Elimu Duniani kwa mwaka 2019 anasema, elimu ni ufunguo unaoleta mabadiliko katika maisha. Katibu Mkuu amemnukuu balozi mwema wa amani wa Umoja wa Mataifa Malala Yousafzai ambaye aliwahi kusema, “mtoto mmoja, mwalimu mmoja, kitabu kimoja, na kalamu moja vinaweza kubadili ulimwengu.” Na Mzee Nelson Mandela aliwahi kusema pia elimu ni “silaha kubwa zaidi ambayo unaweza kutumia kubadili ulimwengu.” Elimu ni kiini cha maendeleo ili kujenga na kudumisha usawa, kuimarisha afya, kutokomeza ndoa za utotoni pamoja na kulinda rasilimali na mali asili ya dunia.

Elimu ina mchango mkubwa katika mchakato wa kufyekelea mbali chuki na uhasama dhidi ya wageni; pamoja na hali ya kutovumiliana. Katibu Mkuu amesema elimu inaweza kuvunja minyororo ya umaskini kwani utafiti unaonyesha kuwa iwapo watoto watafaulu kuhitimu masomo ya sekondari, watu milioni 420 wanawaza kuepukana na umaskini. Hivyo ametoa wito kwa dunia kuweka elimu kama kipaumbele, kuiunga mkono kwa ushirikiano na ufadhili na kutambua kuwa kutomwacha mtu yeyote nyuma kunaanza na elimu.

Bi Audrey Azoulay, Mkurugenzi mkuu wa UNESCO katika ujumbe wake kwa Siku ya Kwanza ya Elimu Duniani anakaza kusema, elimu ni kati ya vipaumbele vilivyotolewa kwenye Malengo ya Maendeleo Endelevu ifikapo mwaka 2030, kama chachu ya mageuzi yanayofumbatwa katika ubora, usawa na fursa kwa wote kuweza kujiendeleza. Bila elimu bora, itakuwa vigumu sana kuweza kupambana na mnyororo wa umaskini unaoendelea kupekenyua maisha ya watoto, vijana na wazee wengi duniani.

Bi Azoulay anasema, Jumuiya ya Kimataifa itashindwa kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi wala kwenda na wakati katika matumizi ya maendeleo ya sayansi na teknolojia. Elimu bora itasaidia sana mchakato wa kujenga na kudumisha usawa kati ya watu, dhamana inayohitaji utashi wa kisiasa kama sehemu ya utekelezaji wake! Takwimu za Umoja wa Mataifa zinabainisha kwamba, kuna watoto na vijana zaidi ya milioni 262 ambao hawana nafasi ya kuhudhuria masomo shuleni.

Watoto milioni 617 hawajui kusoma wala kuandika na kwamba, asilimia 40% ya idadi ya watoto hawa ni wasichana wanaoishi katika maeneo ya vijijini! Hali ya Elimu Kusini mwa Jangwa la Sahara inaonesha kwamba, kuna zaidi ya watoto milioni 4 ambao wengi wao ni wakimbizi na wahamiaji wamelazimika kuacha kuendelea na masomo kutokana na vita, kinzani pamoja na mipasuko ya kijamii.

Askofu Mkuu Auza: Elimu
28 February 2019, 15:27