Tafuta

Papa Francisko anahimiza taalimungu ya kuwasindikiza na kuwahudumia wagonjwa kama ushuhuda wa Injili ya huruma na upendo, sehemu muhimu ya Uinjilishaji! Papa Francisko anahimiza taalimungu ya kuwasindikiza na kuwahudumia wagonjwa kama ushuhuda wa Injili ya huruma na upendo, sehemu muhimu ya Uinjilishaji! 

Taalimungu ya kuwasindikiza na kuwahudumia wagonjwa!

Huduma kwa wagonjwa na wale wote wanaoteseka ni utekelezaji wa Injili ya upendo na huruma ya Mungu kwa watu wote. Ni sehemu ya mchakato wa kutangaza, kushuhudia na kujenga Ufalme wa Mungu kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko kama alivyofanya Msamaria mwema. Kumbe, ni wajibu wa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kuwa ni mashuhuda amini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa maadhimisho ya Siku ya 27 ya Wagonjwa Duniani kwa mwaka 2019, inayoongozwa na kauli mbiu “Mmepata bure, toeni bure”. Mt. 10:8. Anasema,  Kanisa kama Mama anawakumbusha watoto wake kuwa wakarimu na watu wenye upendo kwa wagonjwa. Wawe mstari wa mbele katika kuwajali na kuwatunza wagonjwa wanaohitaji kuonjeshwa utaalam na weledi; upole, unyoofu na unyenyekevu, kwa kujisadaka bila ya kujibakiza, ili wagonjwa waweze kutambua kwamba, wanapendwa na kuthaminiwa!

Baba Mtakatifu anaonya kwamba, maisha ya binadamu kamwe hayawezi kubinafsishwa hasa kutokana na maendeleo makubwa ya sayansi ya tiba ya mwanadamu na teknolojia inayotoa kishawishi cha watu kutaka kuchezea uhai wa binadamu! Anawataka waamini pamoja na wadau mbali mbali kumwilisha ndani mwao, mfano wa Msamaria mwema, ili kuganga kwa mafuta ya faraja na divai ya matumaini, wale wote wanaoteseka, wanaosumbuliwa na kunyanyasika kutokana na magonjwa! Maadhimisho ya Siku ya 27 ya Wagonjwa Duniani, Kimataifa yalifunguliwa rasmi, hapo tarehe 9 Februari huko Calcutta, India na kilele chake ni tarehe 11 Februari, Kanisa linapoadhimisha kumbu kumbu ya Bikira Maria wa Lourdes.

Kardinali Peter Kodwo Appiah Turkson, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu, kuanzia tarehe 8-12 Februari 2019 anaongoza ujumbe wa mshikamano na udugu kutoka Vatican katika maadhimisho ya Siku ya 27 ya Wagonjwa Duniani kwa mwaka 2019 huko Calcutta, nchini India, ambako kuna changamoto kubwa ya umaskini, magonjwa, ujinga na ubaguzi wa aina mbali mbali. Katika uzinduzi wa maadhimisho haya, tarehe 9 Februari 2019, Kardinali Turkson, amepembua taalimungu ya kuwasindikiza na kuwahudumia wagonjwa na wanaoteseka mintarafu tafakari ya Baba Mtakatifu Francisko.

Huduma kwa wagonjwa na wale wote wanaoteseka ni utekelezaji wa Injili ya upendo na huruma ya Mungu kwa watu wote. Ni sehemu ya mchakato wa kutangaza, kushuhudia na kujenga Ufalme wa Mungu kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko kama alivyofanya Msamaria mwema. Kumbe, ni wajibu wa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma na upendo wa Mungu kwa wagonjwa, maskini na wale wote wanaoteseka. Baba Mtakatifu anawataka watu wamwone Kristo Yesu anayeendelea kuteseka kati pamoja na wagonjwa, maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Wawe ni mashuhuda wa imani tendaji inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, daima wakiwa tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kama ilivyo kwa Kristo Yesu anayeendelea kujisadaka kila siku katika Sakramenti ya Ekaristi Takatifu. Kristo Yesu, kwa njia ya mateso na kifo chake Msalabani, ametoa maana mpya ya mateso na mahangaiko ya binadamu, mwaliko kwa wagonjwa na wale wote wanaoteseka, kujiaminisha kwa Kristo Yesu, ili kweli mateso na mahangaiko yao, yaweze kuwa ni chachu ya kulitakatifuza Kanisa kwa kutambua kwamba, maisha yana thamani kubwa sana mbele ya Mungu. Hapa, Baba Mtakatifu anakazia utu, heshima na haki msingi za wagonjwa ambao wanapaswa kutambua kwamba, wao ni amana na utajiri wa Kanisa. Wagonjwa wavumilie mateso yao kwa amani na utulivu wa ndani kama chachu ya uinjilishaji.

Waamini wanaalikwa kushiriki mateso na mahangaiko ya wagonjwa kwa njia ya imani, matumaini na mapendo yanayotakatifuza na kuwaokoa watu. Kwa njia ya ushiriki huu mkamilifu, waamini na watu wote wenye mapenzi mema, wataweza kujenga na kuimarisha mafungamano ya umoja na udugu wa kibinadamu. Wagonjwa, maskini na wale wanaoteseka, wanapaswa kupewa kipaumbele cha pekee katika sera na mikakati ya huduma na maendeleo fungamani ya binadamu. Huduma kwa wagonjwa inafumbatwa katika sadaka na majitoleo pasi na kujibakiza hata kidogo kwa kutambua kwamba, nguvu ya kweli katika maisha ya mwanadamu ni huduma inayotambua: utu, heshima na haki msingi za binadamu. Hii ni huduma inayotolewa kama mashuhuda wa furaha ya Injili!

Baba Mtakatifu anawataka waamini katika kuwahudumia wagonjwa na maskini, kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya matumaini, upendo na mshikamano, ili kuwafunulia watu, upendo na huruma ya Mungu. Waamini wawe na ujasiri wa kukabiliana na mateso pamoja na mahangaiko yao kwa imani na matumaini thabiti, pasi na kukata wala kukatishwa tamaa, daima wamwone Kristo Yesu Msalabani mbele ya macho yao! Baada ya mateso ya Ijumaa kuu, waweze kushiriki tena ushindi na utukufu wa Kristo Mfufuka! Baba Mtakatifu analihamasisha Kanisa kuwa ni chombo na shuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa wagonjwa na maskini! Kanisa liwe ni jicho kwa vipofu, miguu kwa viwete na nuru kwa wale wanaotembea katika giza la dhambi na mauti!

Kanisa liendelee kuwa ni sauti ya kinabii kwa yatima na wale wote wanaoteseka kwa sababu mbali mbali katika maisha. Watu hawa watambue kwamba, kilio chao kina nguvu hata ya kuweza kumfikia Mwenyezi Mungu, kwani hawa ni watu wanaolitegemeza Kanisa kwa sadaka na mateso yao! Mwishoni kabisa, Papa Francisko anatoa mwaliko kwa Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, anashirikiana na wadau mbali mbali ili kupambana na maadui wakubwa wa binadamu, yaani:umaskini, ujinga, maradhi, baa la njaa bila kusahau uchafuzi wa mazingira nyumba ya wote! Maadhimisho ya Mwaka 2019 yanafanyika Calcutta, nchini India kama njia ya kumuenzi Mama Theresa wa Calcutta, mfano wa ukarimu, upendo na huruma ya Mungu kwa maskini na wagonjwa.

Maisha yake yote, yalikuwa ni kutangaza na kushuhudia huruma na upendo wa Mungu! Akasimama kidete na kuwa kweli mtetezi wa Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo! Daima ndani ya maskini na wale wote walioachwa pweke kandoni mwa barabara, aliiona ile sura na mfano wa Mungu! Mama Theresa wa Calcutta akawa ni sauti ya wanyonge, ili kuamsha dhamiri kwa viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa ili waweze kujifunga kibwebwe, kupambana na umaskini. Katika ushuhuda huu, Mama Theresa akawa ni nuru ya ulimwengu na  chumvi ya dunia, mwaliko wa kujisadaka bila ya kujibakiza ili kuzima kiu ya uelewa wa upendo na huruma ya Mungu kwa wagonjwa.

Ukarimu uwe ni sehemu ya vinasaba na utambulisho wa wahudumu katika sekta ya afya, kama ilivyokuwa kwa Msamaria mwema. Huduma ya kujitolea kuwasaidia wagonjwa na maskini ni sehemu ya mchakato wa kutetea na kudumisha haki msingi kwa wagonjwa na hasa zaidi wagonjwa wanaoteseka kwa magonjwa ya muda mrefu!

Taalimungu ya Wagonjwa
11 February 2019, 12:57