Tafuta

Vatican News
Papa Francisko: Hija ya Kitume Umoja wa Falme za Kiarabu: Waamini 135, 00 0 tu ndio watakaoruhisiwa kushiriki! Papa Francisko: Hija ya Kitume Umoja wa Falme za Kiarabu: Waamini 135, 00 0 tu ndio watakaoruhisiwa kushiriki! 

Papa Francisko Umoja wa Falme za Kiarabu: Misa ni watu 135, 000!

Mfalme Mrithi Mohammed bin Zayed Al Nahyan ametangaza kwamba, tarehe 5 Februari 2019 kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema watakaoshiriki Ibada ya Misa Takatifu itakayoongozwa na Baba Mtakatifu Francisko, itakuwa ni siku ya mapumziko kwao. Lakini kutokana na sababu za ulinzi na usalama ni watu 135, 000 tu ndio watakaoruhusiwa kuingia uwanjani humo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu itakayoendeshwa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya kitume huko Abu Dhabi, kwenye Umoja wa Falme za Kiarabu,  Jumanne, tarehe 5 Februari 2019 kwenye Uwanja wa Michezo wa Zayed  ni kati ya zawadi kubwa zinazotarajiwa kwa ajili ya Wakristo huko Falme za Kiarabu. Hili ni Kanisa linaloundwa na wahamiaji pamoja na wakimbizi kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Ni fursa kwa Baba Mtakatifu kutambua mchango wao katika maisha na utume wa Kanisa na hivyo uwepo wa Baba Mtakatifu kati yao ni kutaka kuimarisha umoja, upendo na mshikamano; kwa kuheshimu uhuru wa kidini pamoja na uhuru wa kuabudu.

“Nifanye chombo cha amani” ndiyo kauli mbiu inayoongoza hija ya 27 ya Baba Mtakatifu Francisko kimataifa. Hii inaonesha kwamba, amani, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi yanawezekana kwa kutambua kuwa, tofauti msingi ni amana na utajiri na kamwe si fursa ya kuwagawa na kuwasambaratisha watu. Baba Mtakatifu anasema imani kwa Mwenyezi Mungu ni sumaku inayowaunganisha waamini wa dini mbali mbali! Kwa njia ya tofauti msingi katika imani, waamini wanaweza kujenga na kudumisha udugu wa kibinadamu, kauli mbiu itakayoongoza Mkutano wa Kimataifa wa majadiliano ya kidini huko Abu Dhabi!

Mfalme Mrithi Mohammed bin Zayed Al Nahyan ametangaza kwamba, tarehe 5 Februari 2019 kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema watakaoshiriki Ibada ya Misa Takatifu itakayoongozwa na Baba Mtakatifu Francisko, itakuwa ni siku ya mapumziko kwao. Lakini kutokana na sababu za ulinzi na usalama ni watu 135, 000 tu ndio watakaoruhusiwa kuingia uwanjani na kushikiri Ibada ya Misa Takatifu, ingawa kuna Wakristo zaidi ya milioni moja.

Itakumbukwa kwamba, Mwaka 2019 umetangazwa na Nchi za Umoja wa Falme za Kiarabu kuwa ni Mwaka wa Maridhiano na wengine wanapenda kuuita Mwaka wa Kuvumiliana. Mwaka 2018, Waziri Sheikha Lubna Al Qassimi alitembelea mjini Vatican na kubahatika kukutana na Baba Mtakatifu Francisko pamoja na viongozi wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini. Umoja wa Falme za Kiarabu zina historia kubwa ya majadiliano ya kidini na uhuru wa kuabudu.

Askofu Paul Hinder, Msimamizi wa Kitume huko Umoja wa Falme za Kiarabu, Oman na Yemen anasema, Baba Mtakatifu anakwenda Abu Dhabi kama chombo cha amani na shuhuda wa majadiliano ya kidini, tayari kuwasha moto wa imani na matumaini kwa watu wanaoteseka kwa vita, chuki na uhasama kutokana na misimamo mikali ya kiimani. Baba Mtakatifu amekuwa ni mtetezi wa maskini na wanyonge, lakini zaidi waathirika wa vita, dhuluma na nyanyaso mbali mbali huko Mashariki ya Kati. Uwepo wake kwenye Umoja wa Falme za Kiarabu ni fursa ya kujenga matumaini mapya!

Papa: Umoja wa Falme Kiarabu
01 February 2019, 15:44