Tafuta

Kardinali Parolin asema, hija ya Papa Francisko kwenye Umoja wa Falme za Kiarabu inapania kujenga madaraja ya watu kukutana ili kudumisha haki, amani na maridhiano! Kardinali Parolin asema, hija ya Papa Francisko kwenye Umoja wa Falme za Kiarabu inapania kujenga madaraja ya watu kukutana ili kudumisha haki, amani na maridhiano! 

Papa Francisko Umoja wa Falme za Kiarabu: Umoja na mshikamano!

Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican anasema, viongozi wa kidini wanapaswa kusimama kidete kupambana na misimamo mikali ya kidini na kiimani, ili kujenga na kudumisha haki, amani na maridhiano kati ya watu, ili kuwajengea tena watu wa Mungu matumaini ya ulimwengu mpya ambao kwa sasa unaonekana kumezwa na mipasuko ya kila aina!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Umoja wa Falme za Kiarabu ni daraja muhimu sana linalounganisha nchi za Mashariki na Magharibi. Ni nchi ambayo ina utajiri mkubwa wa watu kutoka katika mataifa mbali mbali duniani; watu wenye lugha, tamaduni, mila na desturi zao; amana na utajiri mkubwa kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kumbe, hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini humo, kuanzia tarehe 3-5 Februari 2019 inapania pamoja na mambo mengine kuandika ukurasa mpya wa historia na matumaini ya watu wa Mungu mintarafru majadiliano ya kidini.

Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican katika mahojiano maalum na Vatican News anasema, matukio makuu mawili katika hija hii ya kitume ni hotuba ya Baba Mtakatifu katika mkutano wa kimataifa wa majadiliano ya kidini pamoja na maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa Michezo wa Kumbu kumbu ya Zayed. Mkutano wa Kimataifa wa majadiliano ya kidini unaongozwa na kauli mbiu "Udugu wa kibinadamu”. Baba Mtakatifu katika hija hii anapenda kuwa ni chombo cha amani, mjenzi wa madaraja ya watu kukutana ili kudumisha udugu wa kibinadamu; haki msingi, utu na heshima ya binadamu, daima uhuru wa kidini na uhuru wa kuabudu vikipewa nafasi ya pekee!

Baba Mtakatifu anataka kuwahamasisha viongozi wakuu wa dini na waamini katika ujumla wao kushikamana kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na utulivu sehemu mbali mbali za dunia. Kwa Wakristo wanaoishi na kufanya kazi zao kwenye Umoja wa Falme za Kiarabu wanatiwa shime, kuwa kweli ni mashuhuda wa tunu msingi za maisha ya Kikristo. Kardinali Parolin anakaza kusema, licha ya dunia kuendelea kuwa na madonda makubwa ya vitendo vya kigaidi, mkutano wa wakuu wa dini mbali mbali duniani, ni alama ya kutaka kujenga na kudumisha utu na heshima ya binadamu; unaozingatia haki na wajibu na kwamba, wote hawa ni watoto wa Mwenyezi Mungu, licha ya tofauti zao msingi.

Viongozi wa kidini wanapaswa kusimama kidete kupambana na misimamo mikali ya kidini na kiimani, ili kujenga na kudumisha haki, amani na maridhiano kati ya watu, ili kuwajengea tena watu wa Mungu matumaini ya ulimwengu mpya ambao kwa sasa unaonekana kumezwa na mipasuko ya kila aina! Watu kutoka sehemu mbali mbali za dunia, wanaishi na kufanya kazi kwenye nchi ya Umoja wa Falme za Kiarabu! Kumbe, uwepo wao ni sehemu ya mchakato wa ujenzi wa madaraja ya watu kukutana, ili kuishi kwa amani, umoja na ushirikiano kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, jitihada zinazotekelezwa na Serikali ya Umoja wa Falme za Kiarabu.

Hiki ni kielelezo makini cha cha ujenzi wa jamii inayosimikwa katika: haki, amani na maridhiano. Kanisa liko karibu na Wakristo sehemu mbali mbali za dunia, wanaopata shida katika kutangaza na kushuhudia imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Katika hali na mazingira kama haya, watambue kwamba, wanakumbukwa na wakristo wenzao kutoka sehemu mbali mbali za dunia! Kardinali Parolin kunako mwezi Juni, 2015 alipata nafasi ya kutembelea na kushiriki katika maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa katika Nchi ya Umoja wa Falme za Kiarabu. Alitabaruku Kanisa la Mtakatifu Paulo Mtume na Mwalimu wa Mataifa. Katika Ibada ambayo ilihudhuriwa na viongozi mbali mbali wa Kanisa pamoja na Familia ya Mungu nchini humo, ili kushiriki kikamilifu katika upendo wa Mungu kwa ajili ya wote alikazia juu ya upendo wa Mungu uliotundika juu ya Msalaba wa Kristo Yesu.

Alisema, huu ni upendo endelevu unaojikita katika uaminifu unaomkirimia mwamini  huruma, neema na utumilifu wa maisha. Kwa namna ya pekee, Yesu alijionesha si kwa mafundisho yake, wala kwa miujiza aliyowatendea watu, bali pale alipoinuliwa juu Msalabani, akainamisha kichwa na kukata roho, kielelezo cha hali ya juu kabisa cha upendo wa Mungu unaokoa na kuponya dhambi za mwanadamu. Kardinali Parolin, katika mahubiri yake alisema kwamba, kwa mwamini anayetaka kufahamu, kuonja na kuukumbatia upendo na huruma ya Mungu, hana budi kumwangalia Yesu aliyetundikwa Msalabani, Yesu aliyetobolewa ubavuni kwa mkuki, humo zikatoka Sakramenti za Kanisa.

Waamini wajitahidi kumwomba Yesu katika sala na maisha ili awajalie kuwa na moyo mkuu unaoguswa na mahangaiko ya watu, hasa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Wakristo wanaoishi katika Umoja wa Falme za Kiarabu wanatoka katika mataifa, lugha na tamaduni mbali mbali, kielelezo cha umoja na mshikamano wa Kanisa moja, takatifu, katoliki na la mitume! Changamoto kwa waamini katika mazingira kama haya ni mchakato wa ujenzi wa umoja wa Kanisa unaovuka mipaka ya utaifa. Waamini hawa wanakabiliana na changamoto zao, lakini kuna juhudi za ujenzi wa umoja na mshikamano wa Kikanisa; ushuhuda wa tunu msingi za Kikristo zinazomwilishwa katika mchakato wa ujenzi wa jamii inayowazunguka.

Kardinali: Umoja wa Falme za Kiarabu
03 February 2019, 10:29