Tafuta

Vatican News
 Hati ya Udugu wa Kibinadamu ni nyenzo msingi katika kukuza na kudumisha amani duniani ! Hati ya Udugu wa Kibinadamu ni nyenzo msingi katika kukuza na kudumisha amani duniani!  (Vatican Media)

Hati ya Udugu wa Kibinadamu ni nguzo ya amani duniani!

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Hati ya Udugu wa Kibinadamu, iliyotiwa mkwaju kati yake na Dr. Ahmad Al-Tayyib, Imam Mkuu wa Msikiti wa Al- Azhar, ulioko Kairo, nchini Misri ni mwaliko kwa waamini wa dini mbali mbali duniani, kuungana na kushikamana, ili kufanya kazi katika umoja na udugu, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii anasema, Hati ya Udugu wa Kibinadamu, iliyotiwa mkwaju kati yake na Dr. Ahmad Al-Tayyib, Imam Mkuu wa Msikiti wa Al- Azhar, ulioko Kairo, nchini Misri ni mwaliko kwa waamini wa dini mbali mbali duniani, kuungana na kushikamana, ili kufanya kazi katika umoja na udugu, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu! Hati hii ni matunda ya uvumilivu, busara na hekima inayopania kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini yanayofumbatwa katika ukweli na uwazi, ili kudumisha amani duniani!

Hati ya Udugu wa Kibinadamu imetiwa sahihi wakati wa maadhimisho ya Mkutano wa Majadiliano ya Kidini Kimataifa huko Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu, hapo tarehe 4 Februari 2019. Dr. Alessandro Gisotti, Msemaji wa Muda wa Vatican anakazia umuhimu wa Hati hii, kama chombo cha kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya waamini wa dini mbali mbali duniani. Hati hii ni kiini cha hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko huko Umoja wa Falme za Kiarabu kuanzia tarehe 3-5 Februari 2019.

Hati ya Udugu wa Kibinadamu inawataka waamini kujikita katika kutenda mema; kuendeleza na kudumisha majadiliano ya kidini; kwa kuheshimiana na kuthaminiana kama ndugu wamoja, licha ya tofauti zao msingi. Waamini wawe na ujasiri wa kushirikiana na kushikamana kwa ajili ya huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Baba Mtakatifu Francisko na Dr. Ahmad Al-Tayyib, Imam Mkuu wa Msikiti wa Al- Azhar, wameonesha dira na mwongozo wa hija ya: haki, amani na upatanisho miongoni mwa waamini wa dini mbali mbali. Hii ni dhamana inayowafumbata na kuwaunganisha watu wote wenye mapenzi mema, daima wakijitahidi kuongozwa na dhamiri nyofu.

Lengo ni kujenga mazingira yatakayowawezesha watu kuishi katika ulimwengu unaosimikwa katika haki, upendo na mshikamano. Huu ni mwaliko wa kuondokana na kufuru ya kutumia jina la Mwenyezi Mungu kwa ajili ya mafao binafsi, sababu za kuanzisha vita, ghasia, chuki na mipasuko ya kijamii. Maisha ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu inapaswa kulindwa, kuheshimiwa na kuendelezwa na wote. Huu ni mwanzo wa ujenzi wa utamaduni wa watu kukutana, ili kuimarisha madaraja ya amani kati ya watu wa Mataifa; kizazi cha sasa na kile kijacho!

Hati Udugu Kibinadamu

 

 

05 February 2019, 14:12