Vatican News
Mheshimiwa Padre Lazarus Vitalis Msimbe, S.D.S. ameteuliwa na Papa Francisko kuwa Msimamizi wa Kitume, Jimbo Katoliki la Morogoro, Tanzania. Mheshimiwa Padre Lazarus Vitalis Msimbe, S.D.S. ameteuliwa na Papa Francisko kuwa Msimamizi wa Kitume, Jimbo Katoliki la Morogoro, Tanzania. 

P. Lazarus Msimbe, ateuliwa kuwa Msimamizi wa Kitume, Morogoro

Papa Francisko amemteua Mheshimiwa Sana Padre Lazarus Vitalis Msimbe, S.D.S kuwa Msimamizi wa Kitume wa Jimbo Katoliki la Morogoro, Tanzania. Kabla ya uteuzi huu, Padre Msimbe, alikuwa ni Makamu wa Shirika la Mungu Mwokozi, maarufu kama Wasalvatoriani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko amemteua Mheshimiwa Sana Padre Lazarus Vitalis Msimbe, S.D.S kuwa Msimamizi wa Kitume wa Jimbo Katoliki la Morogoro, Tanzania. Kabla ya uteuzi huu, Padre Msimbe, alikuwa ni Makamu wa Shirika la Mungu Mwokozi, maarufu kama Wasalvatoriani. Itakumbukwa kwamba, Mheshimiwa Padre Msimbe alizaliwa tarehe 27 Desemba 1963 huko Homboza, Jimbo Katoliki la Morogoro. Baada ya masomo yake ya msingi na sekondari, alijiunga na masomo ya falsafa kwenye Seminari kuu ya Kibosho, Jimbo Katoliki la Moshi.

Baadaye aliendelea na masomo ya taalimungu, Seminari kuu ya Segerea, iliyoko Jimbo kuu la Dar es Salaam. Baada ya majiundo yake ya kitawa, tarehe 8 Desemba, 1987, Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, akaweka nadhiri zake za daima na hatimaye, kupewa daraja Takatifu ya Upadre tarehe 21 Juni 1998. Mheshimiwa Padre Msimbe aliendelea na masomo ya juu huko London, Uingereza na kujipatia Shahada ya Uzamili katika Sheria za Kanisa kutoka katika Chuo Kikuu cha Uingereza. Baadaye pia alijiendeleza na hatimaye kujipatia shahada kwenye Sheria za Kimataifa kutoka katika Chuo Kikuu cha West-England, kilichoko Bristol, Uingereza.

Baada ya kurejea nchini Tanzania, alipangiwa utume wa kuwa ni mlezi wa Wapostulanti na Wanovisi wa Shirika la Mungu Mwokozi. Kuanzia mwaka 2006 hadi mwaka 2012 alichaguliwa kuwa Padre Mkuu wa Kanda ya Shirika la Mungu Mwokozi, nchini Tanzania. Baada ya kumaliza muda wake wa uongozi, ameendelea kuwa ni mlezi wa Shirika kimataifa katika nyumba ya malezi "Mater Salvatoris" iliyoko Jimbo Katoliki la Morogoro. Hadi kuteuliwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Msimamizi wa kitume, mwenye kuwajibika moja kwa moja na Vatican katika masuala yote uongozi wa Jimbo Katoliki la Morogoro, alikuwa ni Makamu mkuu wa Shirika la Mungu Mwokozi nchini Tanzania.

Ieleweke wazi kwamba, Baba Telesphor Mkude, bado ni Askofu wa Jimbo la Morogoro (Sede plena), bali amepumzishwa katika majukumu ya kuongoza, kutakatifuza na kuwafundisha watu wa Mungu Jimbo Katoliki la Morogoro ili kushughulikia zaidi afya yake ambayo kwa miaka ya hivi karibuni iliteteleka sana. Kumbe, kuanzia tarehe 13 Februari 2019 majukumu yote ya Jimbo Katoliki la Morogoro yatasimamiwa na Padre Msimbe, Msimamizi wa kitume. Katika kipindi hiki Askofu Mkude, hawezi kufanya uamuzi wowote wa kiutawala bila kumshirikisha na kuridhiwa na Msimamizi wa kitume.

Jimbo Morogoro

 

 

13 February 2019, 13:48