Tafuta

Mkutano wa Kanisa Kuhusu Ulinzi wa Watoto: Umuhimu wa Kanisa kuboresha mawasiliano kwa wote! Mkutano wa Kanisa Kuhusu Ulinzi wa Watoto: Umuhimu wa Kanisa kuboresha mawasiliano kwa wote! 

Mkutano Kuhusu Ulinzi wa Watoto: Umuhimu wa mawasiliano!

Kanisa halina budi kujifunza kutokana na makosa yaliyopita, kwa kujikita katika kanuni ya ukweli na uwazi unaotoa kipaumbele cha kwanza kwa waathirika. Viongozi wa Kanisa wawe na ujasiri wa kuomba ushauri pamoja na kuhakikisha kwamba, wanajenga uwezo wa kuwasiliana kitaaluma! Mawasiliano ni kwa ajili ya wote! Mawasiliano yaboreshwe zaidi ndani ya Kanisa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mchakato wa mawasiliano katika ukweli na uwazi ni nyenzo madhubuti katika kupambana na kashfa ya nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa kama Mama na Mwalimu anayewapenda na kuwaheshimu watoto wake wote bila ubaguzi. Kanisa lina dhamana ya kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo mintarafu kanuni maadili na utu wema unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Nyanyaso za kijinsia ni uhalifu unaosababisha mateso makubwa kwa watu. Kanisa linapaswa kuchukua msimamo wake katika kupambana na kashfa ya nyanyaso za kijinsia; kwa kuendelea kujikita katika kuboresha mawasiliano kwa kuchukua hatua madhubuti.

Hii ni changamoto na mwaliko kwa Kanisa kujifunza kutokana na makosa yaliyopita, kwa kujikita katika kanuni ya ukweli na uwazi unaotoa kipaumbele cha kwanza kwa waathirika. Viongozi wa Kanisa wawe na ujasiri wa kuomba ushauri pamoja na kuhakikisha kwamba, wanajenga uwezo wa kuwasiliana kitaaluma! Mawasiliano ni kwa ajili ya wote! Huu ndio mchango uliotolewa, Jumamosi, tarehe 23 Februari 2019 na DR. Valentina Alazraki, katika hotuba yake elekezi kwenye Mkutano wa Kanisa Kuhusu Ulinzi wa Watoto Wadogo. Dr. Alazraki, mwandishi wa habari kutoka Mexico, aliyebobea katika safari za kichungaji tangu kwa Mtakatifu Yohane Paulo II hadi Papa Francisko kwa wakati huu!

DR. Valentina Alazraki anasema, waandishi wa habari kwa kawaida wanatafuta ustawi na mafao ya wengi, kumbe, Kanisa halina budi kujifunza kushirikiana na wadau katika tasnia ya mawasiliano ya jamii, ili kuondoa mashaka na wasi wasi unaoweza kutanda katika akili za watu. Tasnia ya habari mara nyingi ina malengo ya kisiasa, kijamii na kiuchumi na kwamba, hakuna sababu kwa Kanisa kulaani na kushutumu vyombo vya mawasiliano ya jamii vilivyoibua kashfa ya nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI aliwahi kusema, adui mkubwa wa Kanisa ni dhambi zinazotendwa na watoto wake!

Kumbe, waandishi wa habari wataendelea kuwa mstari wa mbele kutetea haki ya watu kupata habari mintarafu ukweli, ili haki iweze kutendeka. Vyombo vya habari vinalikomalia sana Kanisa kutokana na dhamana na wajibu wake wa kimaadili na kiutu. Kanisa kushindwa kuwasiliana vyema na tasnia ya habari ni dalili za matumizi mabaya ya mawasiliano na madaraka. Kanisa kwa kuficha kashfa za nyanyaso za kijinsia, limejikuta likisumbuka sana, kumbe, mawasiliano ni muhimu ili kuganga na kuponya kashfa za kijinsia ndani ya Kanisa, kwa kuwapatia waathirika nyenzo muhimu ya kuweza kujikinga dhidi ya uhalifu huu.

Kwa kushindwa kuwasiliana barabara, Kanisa linajijengea mazingira ya chuki na uhasama kama ilivyoshuhudiwa wakati wa hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Chile, kunako mwaka 2018. Wahanga wanayo haki ya kufahamu kile kilichotendeka na adhabu iliyochukuliwa, hii ikiwa ni pamoja na kuwafariji wahusika ambao wameteseka na madonda haya kwa muda mrefu katika maisha yao, mwanzo wa kuganga na kuponya watu katika mahangaiko yao! Kanisa lichukue hatua ya kuanza kutoa habari kwa kutambua kwamba, ulimwengu mamboleo si rahisi sana kuficha siri. Kumbe, Kanisa halina budi kujikita katika mchakato wa ukweli na uwazi kwa kusema wazi!

Kanisa lijitahidi kujifunza kutokana na makosa yaliyopita kwa kufanya mawasiliano sahihi na kwamba, kesi ya Marcial Maciel kutoka Mexico, muasisi wa Chama cha Kristo “Legion of Christ” ni mfano hai kabisa wa rushwa katika mawasiliano yaliyofanywa na Kanisa, kiasi kwamba, watu wengi walibaki na madonda makubwa katika akili na nyoyo zao. Ukweli na uwazi utalisaidia Kanisa kupambana na rushwa pamoja na ufisadi wa mali ya Kanisa na hata katika Serikali mbali mbali duniani. Baba Mtakatifu Benedikto XVI ni kiongozi shupavu aliyesimamia ukweli na saratani ya nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa ikaibuliwa wazi, sasa inatafutiwa dawa, ili kweli waamini waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa furaha ya Injili.

Viongozi wa Kanisa watambue kwamba, wanawajibika kikamilifu kwa Mungu na Kanisa! Huu ni mwaliko kwa Kanisa kuachana na dhana ya siri na kuanza kuambata falsafa ya ukweli na uwazi; kwa kuondokana na matumizi mabaya ya madaraka. Nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa ni ukweli usioweza kufumbiwa macho! Pale ambapo viongozi wa Kanisa wanaondolewa madarakani kutokana na kashfa mbali mbali, waamini wana haki ya kufahamu sababu hizi. Ili Kanisa kuweza kudumisha kanuni ya ukweli na uwazi, linapaswa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa waathirika wa nyanyaso za kijinsia.

Viongozi wa Kanisa waoneshe unyenyekevu kwa kuomba msaada kabla ya kufanya maamuzi makubwa. Viongozi wa Kanisa wajitahidi kujifunza kuwasiliana vyema na ukamilifu zaidi, kwa kutoa habari muhimu bila mashaka na kwamba, habari itolewe kwa wakati! Mawasiliano bora ni mtaji wa Kanisa kwa siku za usoni! Kanisa liwe mstari wa mbele kubainisha kashfa ya nyanyaso dhidi ya watawa, matumizi mabaya ya madaraka pamoja na ufisadi ndani ya Kanisa. DR. Valentina Alazraki anahitimisha kwa kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kuwatia shime waandishi wa habari kuendelea kutekeleza dhamana na wajibu wao katika ukweli na uwazi. Viongozi wa Kanisa wajenge utamaduni wa kushirikiana vyema na waandishi wa habari katika maisha na utume wa Kanisa!

Dr. Valentina
23 February 2019, 16:30