Tafuta

Vatican News
Mkutano wa Kanisa Kuhusu Ulinzi wa Watoto Wadogo: Kanisa liweze kuwa mahali salama pa malezi na makuzi ya watu wa Mungu. Mkutano wa Kanisa Kuhusu Ulinzi wa Watoto Wadogo: Kanisa liweze kuwa mahali salama pa malezi na makuzi ya watu wa Mungu.  (Vatican Media)

Mkutano kuhusu Ulinzi wa Watoto: Usalama wa watoto!

Baba Mtakatifu Francisko analitaka Kanisa, kwa kuanzia na wachungaji wake wakuu: kutambua madhara ya nyanyaso za kijinsia katika maisha na utume wa Kanisa na katika maisha ya mtu binafsi na kuanza kuwajibika; kwa kuzuia, ili kweli Kanisa liweze kuwa ni mahali safi na salama kwa ajili ya malezi na makuzi ya watoto wa Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakifu Francisko anasema, ameitisha Mkutano wa Kanisa Kuhusu Ulinzi wa Watoto Wadogo Ndani ya Kanisa kuanzia tarehe 21-24 Februari 2019. Mkutano huu unafanyikia mjini Vatican. Hiki ni kielelezo makini cha wajibu wa kichungaji ili kuweza kukabiliana na changamoto hii nyeti katika ulimwengu mamboleo. Lengo ni kutoa katekesi kwa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki sehemu mbali mbali za dunia, ili Maaskofu waweze kutambua madhara ya nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo. Baba Mtakatifu anapania kuona kwamba, Kanisa linakuwa ni nyumba safi na salama kwa malezi na makuzi ya watoto wa Mungu.

Kardinali Blaise J. Cupich, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Chicago, USA, akizungumza na waandishi wa habari mjini Vatican, Jumatatu, tarehe 18 Februari 2019 wakati wa kuwasilisha maadhimisho ya  mkutano Kuhusu Ulinzi wa Watoto Wadogo ndani ya Kanisa, amesema, ujasiri wa waathirika wa nyanyaso za kijinsia, umeliwezesha Kanisa kuendeleza mchakato huu wa kutaka kulipyaisha Kanisa kwa njia ya toba na wongofu wa ndani; kwa kuwa na mwelekeo thabiti katika kudhibiti, kuganga na kuponya madhara ya nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo.

Licha ya machungu na madonda yao ya kiroho, kimwili na kisaikolojia, waathirika wamekuwa na ujasiri wa kutoka kifua mbele ili kuvunjilia mbali ukimya uliokuwepo, tayari kuzungumzia madhara ya nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa. Huu ni mkutano ambao umedhamiriwa na hatimaye kuitishwa na Baba Mtakatifu Francisko kama sehemu ya utekelezaji wa ushauri kutoka kwa Baraza la Makardinali Washauri. Baba Mtakatifu analitaka Kanisa, kwa kuanzia na wachungaji wake wakuu: kutambua madhara ya nyanyaso za kijinsia na kuanza kuwajibika; kwa kuzuia, ili kweli Kanisa liweze kuwa ni mahali safi na salama kwa ajili ya malezi na makuzi ya watoto wa Mungu.

Kardinali Blaise J. Cupich, anasema, Kanisa halina budi kuwa chombo cha faraja na kimbilio la watu wote wa Mungu bila ubaguzi. Ametumia fursa hii kuelezea lengo la mkutano huu, matukio makuu yanayofumbatwa katika sala, tafakari kutoka kwa wawezeshaji mbali mbali pamoja na kazi za makundi, ili kuhakikisha kwamba, wajumbe wote wanapata nafasi ya kushiriki kikamilifu. Huu ni mkutano utakaofunguliwa, kwa uwepo na ushiriki mkamilifu wa Baba Mtakatifu na akipenda, atakuwa na neno baada ya kukamilika kwa mkutano huu, ambao ni sehemu ya utekelezaji wa “dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa”. Kuna jumla ya washiriki 190.

Waathirika watapata nafasi ya kutoa ushuhuda wao, kama sehemu muhimu sana ya mkutano huu. Itakumbukwa kwamba, kabla ya wajumbe kuhudhuria mkutano huu, waliombwa na Baba Mtakatifu Francisko kuhakikisha kwamba, wanawasikiliza waathirika wa nyanyaso za kijinsia katika maeneo na nchi zao. Lengo ni kuwawezesha viongozi wa Kanisa kufahamu madhara na hatimaye, kuchukua hatua ya kuzuia nyanyaso za kijinsia katika maeneo yao, hasa dhidi ya watoto wadogo, mkazo ambao unatolewa na Baba Mtakatifu Francisko kwa wakati huu.

Kwa upande wake, Askofu mkuu Charles Jude Scicluna wa Jimbo kuu la Malta, ambaye pia ni Katibu Mwambata wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa, amewakumbusha wajumbe kwamba, huu ni mkutano wa shughuli za kichungaji unaopania kuhakikisha kwamba, Kanisa linajitakasa, ili kweli liweze kuwa ni  mahali salama zaidi pa malezi na makuzi ya watoto wa Mungu. Kumbe ni mkutano wa sala na tafakari ya kina, ili kumwomba Mwenyezi Mungu huruma, upendo na msamaha, tayari kuanza upya, kwa Kanisa kujikita zaidi katika mambo makuu matatu: uwajibikaji kwa Maaskofu kukubali na kukiri pale ambapo kumekuwepo na uzembe.

Pili, ni dhamana ya uwajibikaji ili kuwawezesha Maaskofu kutekeleza kikamilifu wajibu wao mintarafu Sheria, Kanuni na Taratibu za Kanisa. Tatu, ni ukweli na uwazi, Jambo ambalo limesisitiziwa zaidi na Padre Federico Lombardi, SJ:,  Rais wa Mfuko wa Joseph Ratzinger/Benedikto XVI. Kanisa linawashukuru na kuwapongeza wadau katika tasnia ya mawasiliano waliosaidia kuibua “sakata hili katika maisha na utume wa Kanisa”. Haya ni matendo ya kinyama dhidi ya utu na heshima ya binadamu. Kwa tukio hili, Kanisa linataka kuwa wazi zaidi na kwamba, habari zaidi zinaweza kupatikana kwenye tovuti kwa anuani ifuatayo: (www.pbc2019.org).

Mkutano huu unafanyika katika vikao vikuu viwili kwa siku: Kikao cha kwanza asubuhi na kingine alasiri! Wawezeshaji watatoa tafakari tatu kwa siku, mbili asubuhi na moja, itawasilishwa alasiri. Kutakuwepo pia kazi za makundi. Alhamisi, tarehe 21 Februari 2019, Papa Francisko anatarajiwa kufungua mkutano huu kwa kutoa hotuba elekezi. Jumamosi, tarehe 23 Februari 2019 kutakuwa na Ibada ya Toba na Jumapili, tarehe 24 Februari 2019 kutakuwa na Ibada ya Misa Takatifu.

Kamati ya Maandalizi ya Mkutano huu, imeanza pia kukutana na kuzungumza na wawakilishi wa waathirika wa nyanyaso za kijinsia kutoka sehemu mbali mbali za dunia na kwamba, Padre Lombardi atakuwa tayari kupokea ujumbe kutoka kwenye vikundi na kwa watu mbali mbali. Kwa upande wake, Padre  Hans Zollner, Rais wa Kituo cha Ulinzi kwa Watoto Wadogo, Chuo Kikuu cha Kipapa cha Gregorian ambaye pia ni mjumbe wa Kamati kuu inayoratibu mkutano maalum wa Kanisa kwa ajili ya kuwalinda watoto wadogo dhidi ya nyanyaso za kijinsia anasema, Mabaraza la Maaskofu Katoliki yaliweza kujibu maswali dodoso na kwamba, asilimia 89% ya watu walioshirikishwa, walionesha ushirikiano mkubwa. Takwimu hizi ni muhimu sana katika kuangalia hali ya Kanisa katika ujumla wake, ili hatimaye, kutoa majibu muafaka kwa Makanisa mahalia na Kanisa la Kiulimwengu katika ujumla wake.

Ulinzi wa Watoto
19 February 2019, 15:26