Tafuta

Mkutano wa Kanisa Kuhusu Ulinzi wa Watoto: Ukweli na Uwazi kama Jumuiya ya Waamini Mkutano wa Kanisa Kuhusu Ulinzi wa Watoto: Ukweli na Uwazi kama Jumuiya ya Waamini 

Mkutano wa Kanisa Kuhusu Ulinzi wa Watoto: Ukweli na uwazi!

Kanisa linapaswa kujitambua kwamba, ni Jumuiya a waamini katika Kristo Yesu, inayosimikwa katika imani, matumaini na mapendo. Kanisa ni Fumbo la Mwili wa Kristo na linaendelea kutegemezwa kwa nguvu ya Roho Mtakatifu. Kanisa kama Jumuiya ya waamini lina sheria, kanuni na taratibu zake zinazopaswa kufuatwa na kuzingatiwa barabara!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ukweli na uwazi kama Jumuiya ya Waamini ni dhana inayofumbata mchakato mzima wa mawazo, maamuzi na utekelezaji wake mintarafu mwanga wa Injili kuhusu uongozi wa Kanisa katika kukabiliana na kashfa ya nyanyaso za kijinsia. Haya ni maisha ya Sala, Sakramenti na Huduma ya Kanisa. Uongozi thabiti wa Kanisa unaweza kushughulikia kashfa ya nyanyaso za kijinsia kwa ukamilifu wote kwa kutambua kwamba, Kanisa ni Sakramenti ya Wokovu na chombo cha umoja kati ya Mungu na waja wake.

Kanisa linapaswa kujitambua kwamba, ni Jumuiya a waamini katika Kristo Yesu, inayosimikwa katika imani, matumaini na mapendo. Kanisa ni Fumbo la Mwili wa Kristo na linaendelea kutegemezwa kwa nguvu ya Roho Mtakatifu. Kanisa kama Jumuiya ya waamini lina sheria, kanuni na taratibu zake zinazopaswa kufuatwa na kuzingatiwa barabara. Kanisa linashughulikia maisha ya kiroho lakini pia linaendesha shughuli zake hapa ulimwenguni zinazopangwa kuongozwa na kanuni ya haki.

Nyaraka, Sheria, Kanuni na Taratibu zilizobainishwa zinapaswa kufuatwa kikamilifu. Uongozi unapaswa kuhakikisha kwamba, sheria, kanuni na maamuzi mbali mbali yanafuatwa na kuzingatiwa, pale yanapokiukwa, sheria ichukue mkondo wake. Uongozi unapaswa kuwa ni kiungo muhimu kati ya watu kama ilivyo hata ndani ya Kanisa. Hii ni sehemu ya hotuba elekezi iliyotolewa Jumamosi, tarehe 23 Februari 2019 na Kardinali Reinhard Marx, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Ujerumani na Mratibu wa Baraza la Kipapa la Uchumi wakati wa Mkutano wa Kanisa Kuhusu Ulinzi wa Watoto wa Wadogo.

Ili kuleta ufanisi, tija na kufikia malengo yaliyowekwa, kuna haja kwa uongozi kutekeleza vyema wajibu wake. Kashfa ya nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo ni kielelezo cha matumizi mabaya ya madaraka pamoja na kushindwa kutekeleza sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa. Matokeo yake, haki za waathirika wa nyanyaso za kijinsia zilisiginwa, kiasi cha kulifanya Kanisa kuyumba na kupoteza mwelekeo wake, badala ya kuwasogeza watu karibu na Mwenyezi Mungu, likajikuta linawakatisha tamaa na kuwasukumiza mbali zaidi.

Kutokana na kashfa ya nyanyaso za kijinsia, kuna haja kwa Kanisa sasa kujikita kikamilifu katika misingi ya ukweli na uwazi, ili kuwawezesha waamini kujisikia wako salama nyumbani, wanakubalika na kutendewa haki: kwa kusikilizwa na maoni yao halali kupokelewa na kufanyiwa kazi. Kwa njia hii, Kanisa litaweza kuwasogeza watu karibu zaidi na Mwenyezi Mungu na huu ndio uelewa wa kitaalimungu kuhusu utume wa uongozi wa Kanisa. Kanisa lisipowatendea watu haki, watu watalikimbia na kumwacha Kristo Yesu anayepaswa kuwa ni dira na kiongozi wa maisha yao. Kanisa liendelee kujikita katika misingi ya ukweli na uwazi; kwa kuweka kumbu kumbu ya mambo yaliyopita. Hapa watu wataweza kugundua makosa yaliyopita na kuchukua hatua madhubuti; wanaweza kuridhika na hatua zilizochukuliwa na kusonga mbele kwa matumaini.

Utangulizi kuhusu uongozi wa Kanisa katika masuala ya sheria ndani ya Kanisa ni muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa. Ili kuhakikisha kwamba, haki inatendeka na hakuna hisia za kuvunjwa kwa siri za kipapa na wala mapadre na Kanisa kushutumiwa kwa uwongo!Kanuni ya ukweli na uwazi inapofafanuliwa katika mchakato hatua kwa hatua hadi kufikia maamuzi, Kanisa litaweza kuepuka shutuma na maamuzi mbele dhidi yake. Mchakato wa ukweli na uwazi unapania kufafanua kanuni zinazopaswa kufuatwa na kuzingatiwa na jinsi ambavyo umma na Sekretarieti kuu ya Vatican inapaswa kuhabarishwa. Kashfa ya nyanyaso za kijinsia ndiyo inayolichafua Kanisa na wala si kukosekana kwa ukweli na uwazi katika kushughulikia kesi hizi.

Kardinali Reinhard Marx, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Ujerumani na Mratibu wa Baraza la Kipapa la Uchumi anakaza kusema, kumbu kumbu, ukweli na uwazi ni changamoto inayopaswa kushughulikiwa na wataalam, kwa kuonesha utashi wa kutaka kushirikiana na watu wengine. Kumbe, kuna haja ya kufafanua kuhusu lengo na mipaka ya siri ya kipapa hasa katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano. Kuna haja ya kukazia ukweli na uwazi katika mchakato wa utekelezaji wa sheria, kanuni na taratibu za Kanisa ili kuhakikisha kwamba, haki inatendeka katika ubora wake. Takwimu na idadi za kesi zitolewe kwa usahihi na ukamilifu mkubwa. Hukumu iyotolewa kwenye kesi husika, ichapishwe ili kuondoa shaka na wasi wasi kuhusu mwenendo wa kesi za Kanisa.

Kard. Marx: Uwazi wa Jumuiya

 

 

23 February 2019, 13:15