Tafuta

Mkutano wa Kanisa Kuhusu Ulinzi kwa Watoto Wadogo: Uwajibikaji wa pamoja: Urika wa Maaskofu na Dhana ya Sinodi! Mkutano wa Kanisa Kuhusu Ulinzi kwa Watoto Wadogo: Uwajibikaji wa pamoja: Urika wa Maaskofu na Dhana ya Sinodi! 

Mkutano wa Kanisa Kuhusu Ulinzi wa Watoto Wadogo: Uwajibikaji

Kardinali Gracias anasema changamoto ya nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa inaweza kudhibitiwa ikiwa kama Kanisa litajikita katika utekelezaji wa “dhana ya Sinodi" kwa: kufanya maamuzi na utekelezaji wake katika ngazi mbali mbali; mchakato ambao unawahusisha watu wote wa Mungu! Uaminifu, ukweli na uwazi ni mambo muhimu katika utekelezaji wa maamuzi yanayowajibisha.

Na Padre Richard A. Mjigwa. – Vatican.

Uwajibikaji karika urika wa Maaskofu mintarafu utekelezaji wa “dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa”, ndiyo mada iliyowasilishwa na Kardinali Oswald Gracias, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Bombay, India katika Mkutano wa Kanisa Kuhusu Ulinzi wa Watoto Wadogo, uliofunguliwa, rasmi Alhamisi, tarehe 21 Februari 2019. Kardinali Oswald Gracias, Ijumaa, tarehe 22 Februari 2019 amekazia kuhusu umuhimu wa: Urika wa Maaskofu na Utendaji wa Kisinodi; mambo ambayo yanafumbatwa katika utamaduni wa kukosoana kidugu.

Amegusia kuhusu changamoto ya nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa; haki, mchakato wa uponyaji pamoja na hija ya Kanisa linalosafiri ambalo ni chemchemi ya utakatifu kwa neema ya Mungu na kwamba, utimilifu wake ni katika utukufu wa mbinguni! Changamoto ya nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa inaweza kudhibitiwa ikiwa kama Kanisa litajikita katika utekelezaji wa “dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa” kwa: kufanya maamuzi na utekelezaji wake katika ngazi mbali mbali; mchakato ambao unawahusisha watu wote wa Mungu!

Uaminifu, ukweli na uwazi ni mambo muhimu katika utekelezaji wa maamuzi yanayowajibisha kama Sinodi. Maaskofu wasijisikie pweke katika kukabiliana na nyanyaso za kijinsia, bali wajenge na kuimarisha urika wa Maaskofu. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanawakumbusha Maaskofu kwamba, wanapaswa kudumisha: umoja na mshikamano, huku wakiwa wameungana na Khalifa wa Mtakatifu Petro, kama kielelezo cha Kanisa zima katika kifungo cha amani, upendo na umoja huku wakisaidiana kidugu.

Kardinali Oswald Gracias,anaendelea kufafanua kwamba, dhana ya “Urika na Sinodi” zinapaswa kumwilishwa katika maisha na utume wa Kanisa kwa kuwajibika kwa pamoja na kurekebishana kidugu, ili kuboresha utume wa kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Maaskofu wakubali na kukiri makosa pale wanapoteleza na kuanguka. Wajenge na kudumisha umoja, mshikamano na utii kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Kuwepo na ushirikiano na majadiliano kati ya Mabaraza ya Maaskofu pamoja Sekretarieti kuu ya Vatican kwa kutambua umoja wa Kanisa unaofumbatwa katika utofauti wake.

Mawasiliano yaendelee kuboreshwa na watu washiriki kikamilifu katika mijadala inayotolewa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa zima! Ni kwa njia hii kwamba, dhana ya urika wa Maaskofu na Sinodi zitaweza kuwa ni sehemu ya utambulisho wa Kanisa. Kashfa ya nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa ni mtandao ambao umekita mizizi yake katika matatizo ya kisaikolojia, maamuzi yanayokwenda kinyume cha kanuni maadili na utu wema; mazingira ya dhambi na utepetevu wa moyo pamoja na kutowajibika barabara.

Nyanyaso hizi zimefanywa na wakleri pamoja na wahudumu wa Kanisa, kiasi cha kuchafua maisha na utume wa Kanisa; waathirika na matokeo yake ni watu kuona kwamba, wamesalitiwa na watu waliokuwa wanapaswa kuwa ni chemchemi ya matumaini na maboresho ya maisha ya kiroho! Haya ndiyo yanayowatumbukiza waathirika katika hali ya kukata na kujikatia tamaa ya maisha. Kanisa limeshindwa kujenga na kudumisha utamaduni wa kusikiliza kwa makini mateso na mahangaiko ya waathirika wa nyanyaso za kijinsia.

Waathirika wengi hawakupewa msaada wa hali na mali na matokeo yake, Kanisa likataka kutunza jina na kuhifadhi heshima yake, lakini kwa bahati mbaya, falsafa hii imelitumbukiza Kanisa katika aibu kubwa zaidi. Dhana ya Urika na Sinodi ni nyenzo muhimu sana katika mapambano dhidi ya nyanyaso za kijinsia katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Kumbe, haki, uponyaji na hija ya watu wa Mungu ni muhimu sana katika mchakato mzima wa mapambano dhidi ya nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa.

Nyanyaso za kijinsia ni uvunjaji wa haki, ni kielelezo cha usaliti, changamoto ni kuhakikisha kwamba, haki ya Mungu inarejeshwa tena katika Jumuiya za waamini na kwamba, Sheria, kanuni na taratibu za Kanisa zitekelezwe kwa uaminifu na uadilifu mkubwa, pamoja na kushirikiana na vyombo vya Sheria, ili haki iweze kutendeka na Kanisa liendelee kuwa ni chombo cha wokovu wa watu wa Mungu na amani na utulivu viweze kurejeshwa tena.

Uponyaji kwa waathirika wa nyanyaso za kijinsia ni muhimu sana; jambo linalokita mizizi yake katika ukweli, uwazi na mawasiliano; kwa kuwaheshimu na kutambua madonda wanayobeba katika maisha yao. Uponyaji unaweza kufanyika kwa njia ya ushauri nasaha pamoja na kuweka mbinu mkakati wa kuwalinda watoto dhidi ya nyanyaso za kijinsia. Kashfa hii ni sehemu ya mapungufu ya kibinadamu, kumbe, hata jamii inahamasishwa kusimama kidete kulinda na kuwatetea watoto dhidi ya nyanyaso za kijinsia.

Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanakaza kusema, Kanisa ni chemchemi ya neema na utakatifu na kwamba, utimilifu wake uko katika utukufu wa mbinguni! Kanisa linalosafiri, katika Sakramenti zake na taasisi zake zilizo za wakati huu, linachukua sura ya ulimwengu unaopita na linaishi kati ya viumbe ambavyo vinagua na vina utungu hata sasa na vinatazamia kwa shauku kubwa kufunuliwa kwa wana wa Mungu! Kardinali Oswald Gracias  anakaza kusema, Kanisa si kamilifu ndiyo maana waamini wanahamasishwa kutubu na kumwongokea Mungu; kuendeleza mchakato wa mang’amuzi na kuomba msamaha. Baraza la Maaskofu Katoliki DRC ni mfano bora wa kuigwa katika kusimamia haki, amani, ustawi na maendeleo ya watu wa Mungu kama Baraza na matokeo yake yanaonekana kwa sasa hata kama si katika utimilifu wake!

Urika wa Maaskofu
22 February 2019, 11:09