Tafuta

Mkutano wa Kanisa Kuhusu Ulinzi wa Watoto Wadogo: Dr. Linda Ghison: Uwajibikaji na umoja Mkutano wa Kanisa Kuhusu Ulinzi wa Watoto Wadogo: Dr. Linda Ghison: Uwajibikaji na umoja 

Mkutano Kuhusu Ulinzi wa Watoto: Uwajibikaji na umoja!

Mama Kanisa katika kukabiliana na kashfa ya nyanyaso za kijinsia anapaswa kutambua na kuheshimu utu na heshima ya waathirika wa nyanyaso za kijinsia; kusikiliza kwa makini shuhuda zinazotolewa na waamini walei; kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo. Kanisa, familia ya Mungu inapaswa kuwa makini katika ulinzi wa watoto wadogo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Dr. Linda Ghisoni katika hotuba yake elekezi wakati wa Mkutano wa Kanisa Kuhusu Ulinzi wa Watoto Wadogo, Ijumaa, tarehe 22 Februari 2019 amekazia kuhusu “Umoja na umuhimu wa kutenda kwa pamoja” ili kulinda na kudumisha utu na heshima ya watoto; kwa kusikiliza na kujibu nyanyaso za kijinsia, ili kuguswa na madonda ya waathirika; kwa toba na unyenyekevu wa ndani. Amekazia umuhimu wa kuwajibika kwa pamoja, jambo ambalo linawezekana kabisa; kwa kushirikiana kwani Kanisa ni Sakramenti katika Kristo; Ukuhani wa waamini pamoja na utekelezaji wake!

Mama Kanisa katika kukabiliana na kashfa ya nyanyaso za kijinsia anapaswa kutambua na kuheshimu utu na heshima ya waathirika wa nyanyaso za kijinsia; kusikiliza kwa makini shuhuda zinazotolewa na waamini walei; kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo. Kanisa, familia ya Mungu inapaswa kuwa makini katika ulinzi wa watoto wadogo; kwa kuwaheshimu ili kwamba, mchakato mzima wa toba na wongofu wa ndani uwe ni sehemu ya maisha na utume wa Kanisa. Uwajibikaji unapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza na kwamba, hili ni jambo linalowezekana kabisa, kwa kujikita katika: ukweli, haki, toba pamoja na kujenga mazingira ili kwamba, kashfa kama hii isijirudie tena katika maisha na utume wa Kanisa.

Kutambua na kukiri uwepo wa kashfa ya nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo ni hatua ya kwanza. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanakumbusha kwamba, katika Kristo Kanisa ni kama Sakramenti au ishara na chombo cha kuwaunganisha watu kiundani na Mwenyezi Mungu na kuleta umoja kati ya wanadamu wote! Hata katika mwelekeo huu, Kanisa linapaswa kuwajibika kutangaza pia mema yanayotekelezwa na Kanisa katika maisha na utume wake, kwa kuwashirikisha waamini walei ambao kimsingi wanashiriki: Ufalme, Ukuhani na Unabii wa Kristo kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo. Ndani ya Kanisa waamini wana dhamana na wajibu wanaopaswa kuutekeleza. Kumbe, hata waamini walei wanapaswa kuchuchumilia na kuambata utakatifu wa maisha! Maaskofu wahakikishe kwamba, wanashirikiana na kushikamana na wakleri wao katika: malezi ya awali na endelevu na mchakato wa utakatifu wa maisha.

Wakleri wajitahidi kushinda kishawishi cha uchu wa mali na madaraka; uchoyo, ubinafsi na kujikweza kiasi hata cha kuwanyonya waamini wao ili kuzima tamaa zao mbovu! Watu wa Mungu wanapenda kuona ushuhuda wa wakleri na watawa wanaozama katika sala na tafakari ya Neno la Mungu; kwa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma pamoja na kujenga mahusiano mema na watu wa Mungu! Umoja na mshikamano wa watu wa Mungu usimikwe pia katika karama na mapaji mbali mbali yanayoweza kutumiwa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa zima. Waamini walei wanayo dhamana na wajibu wa kuyatakatifuza malimwengu kwa maneno na matendo yao! Shughuli zinazoweza kutekelezwa vyema na waamini walei, wapewe na Maaskofu wajishughulishe zaidi katika masuala imani, maadili na utu wema.

Umoja na ushirikiano uzingatie “Sensus fidei” yaani “hisia ya imani na karama” katika taifa la Mungu. Kanisa linawashukuru na kuwapongeza wale wote waliojisadaka kwa ajili ya kuwasaidia wahanga wa nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa. Watoto walindwe kwa kukazia ukweli; haki, toba na wongofu wa ndani; malipizi yafanywe pale, watoto walipokosewa haki zao na kwamba, Kanisa liendelee kujizatiti katika kujenga mazingira bora zaidi yatakayosaidia kukuza na kudumisha malezi na majiundo yao katika hali ya amani, utulivu na usalama. Kama sehemu ya uwajibikaji wa Kanisa, kuna haja kwa Makanisa mahalia kuwa na Mwongozo utakaotumika kuwalinda watoto wadogo dhidi ya nyanyaso za kijinsia.

Watu wa Mungu wajifunze utamaduni wa kuwajibika katika maisha na utume wa Kanisa kama njia makini ya kujenga na kudumisha umoja na mshikamano. Kuwepo na Tume za Waamini Walei zitakazowasaidia Maaskofu kutekeleza vyema dhamana na wajibu wao pamoja na kuangalia uwezekano wa kuunda Ofisi kuu itakayoshughulikia kesi za nyanyaso za kijinsia katika ngazi mbali mbali. Siri ya Kitume, isaidie kulinda utu na heshima ya wahusika; ustawi na maendeleo ya Kanisa kwa kuzingatia pia misingi ya ukweli na uwazi. Mawasiliano ndani ya Kanisa yazingatie pia siri, Sheria, kanuni na taratibu, ili ukweli uweze kutawala.

Dr. Linda: Taifa la Mungu

 

22 February 2019, 16:30