Mkutano wa Kanisa Kuhusu Ulinzi wa Watoto Wadogo: Mchakato wa Uponyaji wa Madonda katika mwanga wa imani! Mkutano wa Kanisa Kuhusu Ulinzi wa Watoto Wadogo: Mchakato wa Uponyaji wa Madonda katika mwanga wa imani! 

Mkutano Kuhusu Ulinzi wa Watoto: Uponyaji wa madonda!

Hii ni fursa ya toba na wongofu wa ndani tayari kuanza mchakato wa kuganga na kuponya madonda haya ambayo yamegusa utu na heshima ya binadamu. Hii ndiyo changamoto kubwa ya kichungaji kwa viongozi wa Kanisa. Jambo la msingi ni kuimarisha imani, kwa kugusa madonda ya udhaifu wa binadamu; kutambua na madhara yake katika maisha na utume wa Kanisa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mkutano wa Kanisa kuhusu Ulinzi wa Watoto Wadogo ni muda muafaka wa kufahamu machungu wanayokabiliana nayo wale walionyanyaswa kijinsia; ni fursa ya toba na wongofu wa ndani tayari kuanza mchakato wa kuganga na kuponya madonda haya ambayo yamegusa utu na heshima ya binadamu. Hii ndiyo changamoto kubwa ya kichungaji kwa viongozi wa Kanisa. Jambo la msingi ni kuimarisha imani, kwa kugusa madonda ya udhaifu wa binadamu; kutambua madhara yake katika maisha na utume wa Kanisa; tayari kusimama katika misingi ya imani, maadili na utu wema na kusonga mbele katika mshikamano na uwajibikaji wa pamoja!

Kwa ufupi kabisa, haya ndiyo yaliyosemwa na Kardinali Luis Antonio Tagle, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Manila, Alhamisi, tarehe 21 Februari 2019, wakati wa mkutano wa Kanisa kuhusu Ulinzi wa Watoto Wadogo, uliofunguliwa mjini Vatican kwa kuwashirikisha Marais wa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki kutoka sehemu mbali mbali za dunia pamoja na viongozi waandamizi wa Kanisa Katoliki. Kardinali Tagle anasema, nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo zisesababisha madonda makubwa kwa wahusika na familia zao; kwa Kanisa na jamii katika ujumla wake.

Maaskofu kutowajibika barabara, tabia ya kuwalinda waliotenda nyanyaso hizi na hata wakati mwingine kupindisha ukweli wake, imesababisha mtikisiko mkubwa kati ya viongozi wa Kanisa na watu wa Mungu katika ujumla wao. Haiwezekani kabisa, wale waliopewa dhamana ya kuwalinda na kuwatetea watoto hawa, ndio waliogeuka na kuwa ni chanzo cha nyanyaso zenyewe! Madonda haya yanahitaji kugangwa na kuponywa katika mwanga wa imani, maisha na utume wa Kanisa. Huu ni mwaliko wa kumwangalia tena na tena Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu!

Zawadi ya kwanza kabisa kwa wafuasi wake waliokuwa wameguswa na kutikiswa sana na kashfa ya Msalaba, ilikuwa “Amani kwenu”. Lakini kwa bahati mbaya, wakati Kristo Yesu alipowatokea Mitume wake, Mtakatifu Thoma, hakuwepo pamoja na wengine na wala hakuamini ushuhuda alioambiwa na akataka kuhakiki mwenyewe kwa kutumbukiza kidole chake katika Madonda Matakatifu ya Kristo Mfufuka na hatimaye siku ilipowadia akakiri mwenyewe “Bwana na Mungu wangu”!

Kardinali Tagle anakaza kusema, wale wote walioitwa na kutumwa kwenda kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo hawana budi kuguswa na madonda ya watu wa Mungu, tayari kuungama na kusema, “Bwana na Mungu wangu”. Madonda ya mwanadamu ni majanga mbali mbali yanayoendelea kumwandama kila kukicha na katika muktadha huu, donda kubwa linagusa na kutikisa imani, maisha na utume wa Kanisa. Uhalifu huu dhidi ya utu na heshima ya binadamu ni sehemu ya madonda makubwa katika Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Hii ni changamoto ya kusimama kidete ili kuhakikisha kwamba, watoto wanaundiwa mazingira bora na salama kwa ajili ya malezi na makuzi yao.

Kristo Yesu katika maisha na utume wake, hakuondoa mateso, ukosefu wa haki na hata wakati mwingine kushindwa, lakini aliwapatia wafuasi wake nguvu ya kuweza kuyaangalia yote haya katika mwanga wa imani. Baada ya mateso, kifo na ufufuko wake, Kristo Yesu aliwaonesha wafuasi wake, Mwili wake uliotukuka, upendo, huruma na msamaha usiokuwa na kifani kama ulivyojionesha kwa maskini, wagonjwa, watoza ushuru, wakoma bila kumsahau yule mwanamke mzinzi aliyekuwa amehukumiwa adhabu ya kifo! Wote hawa walikuwa ni sehemu ya mateso na Madonda Matakatifu ya Kristo Yesu.

Maandiko Matakatifu yanawakumbusha waamini kwamba, Kristo Yesu, ingawa ni Mwana, alijifunza kutii kwa mateso hayo yaliyompata; naye alipokwisha kukamilishwa, akawa sababu ya wokovu wa milele kwa watu wote wanaomtii! Katika mchakato wa viongozi wa Kanisa kutaka kuganga na kuponya madonda haya, watambue kwamba, wanakabiliwa na changamoto kubwa mbele yao; yaani wanapaswa kujivika huruma na upendo; mambo muhimu katika kuganga na kuponya madonda haya katika Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa!

Kamwe, Kanisa lisiogope kusimama kidete kupambana na mambo yanayosababisha madonda haya katika maisha na utume wake yaani: Uchu wa mali na madaraka; matumizi mabaya ya madaraka pamoja na upofu wa Sheria, kanuni na taratibu za Kanisa. Madonda haya ni kumbu kumbu ya udhaifu wa binadamu, uwepo wa dhambi na umuhimu wa toba na wongofu wa ndani! Ikiwa kama viongozi wa Kanisa wanataka kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya uponyaji, hawana budi kuguswa kwanza kabisa katika undani wa maisha na imani yao kwa Kristo Mfufuka, ili kusaidia upyaisho wa maisha ya wale walioathirika. Watambue, udhaifu wao na uwepo wa dhambi pamoja na mahangaiko ya watu wasiokuwa na hatia!

Kardinali Tagle anaendelea kufafanua kwamba, watu wanataka kuona haki inatendeka, kwani wengi wao wameathirika kiasi hata cha kupoteza maisha! Ni wakati wa toba na wongofu wa ndani; wakati wa kusamehe na kusonga mbele; ili kwa pamoja, Kanisa na waathirika waweze kushikamana na kusonga mbele; kwa kuaminiana, kupendana bila masharti na kusamehe, ili kweli haki iweze kukita mizizi yake katika nyoyo za watu kama neema kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Kardinali Luis Antonio Tagle, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Manila, anahitimisha kwa kusema, waathirika wasaidiwe na waliotenda makosa haya, haki itendeke pamoja na kuwasaidia kukabiliana na undani wa maisha yao bila kuwageuzia kisogo! Haki itendeke ili kuimarisha msamaha na upatanisho wa ndani. Waamini wajifunze kutoka kwa Kristo kuwa kweli ni vyombo vya msamaha na upendo wa kweli. Kanisa liendelee kuwa ni Jumuiya ya haki, huruma, umoja na upendo, ili kweli amani ya Kristo iweze kukaa kati ya watu wake!

Kardinali Tagle: Madonda
21 February 2019, 12:10