Mkutano wa Kanisa Kuhusu Ulinzi wa Watoto Wadogo: Padre Federico Lombardi, SJ., Tamko la Kanisa 2019 Mkutano wa Kanisa Kuhusu Ulinzi wa Watoto Wadogo: Padre Federico Lombardi, SJ., Tamko la Kanisa 2019 

Mkutano wa Kanisa Kuhusu Ulinzi wa Watoto: TAMKO LA KANISA 2019

Baba Mtakatifu Francisko anatarajia kuandika Barua Binafsi kuhusu Ulinzi wa Watoto Wadogo. Waraka huu, utasindikizwa na Sheria Mpya ya Vatican katika mada hii. Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa litachapisha “Vademecum” na kwamba, Baba Mtakatifu ameonesha nia ya kuunda “Kikosi Kazi cha wataalam na Mabingwa” kitakachoyasaidia Mabaraza ya Maaskofu Katoliki.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kanisa limesikiliza kwa uchungu mkubwa shuhuda zilizotolewa kuhusu nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo. Kanisa linapenda kuchukua fursa hii, kuomba msamaha kwa uhalifu huu mkubwa uliofanywa dhidi ya watu hawa. Linaomba msamaha kwa kushindwa kutekeleza dhamana na wajibu wake. Maaskofu sasa wanarejea kwenye majimbo na Makanisa yao, huku wakiwa na uelewa mpana zaidi kuhusu madhara ya nyanyaso za kijinsia na madonda yake katika utu na heshima ya binadamu!

Mtakatifu Yohane Paulo II, kunako mwaka 2002 alisema kwa msisitizo kwamba, watu wanapaswa kutambua kwamba, katika maisha na wito wa upadre na utawa hakuna nafasi tena kwa watu wanaoweza kusababisha mateso na mahangaiko kwa watoto wadogo. Kanisa linataka kuona kwamba, maeneo ya shughuli zake zote ni salama kwa malezi na makuzi ya watoto wadogo; mahali ambapo utu na heshima ya binadamu vitathaminiwa na kudumishwa, ili kuwasaidia watoto kukua: kiroho na kimwili!

Hii ni sehemu ya tamko lililotolewa na Padre Federico Lombardi, SJ., Rais wa Mfuko wa Joseph Ratzinger/Benedikto XVI, ambaye pia ni Mratibu wa Mkutano wa Kanisa Kuhusu Ulinzi wa Watoto Wadogo uliofungwa rasmi, Jumapili tarehe 24 Februari 2019. Kanisa litaendeleza mchakato wa: uwajibikaji, dhamana ya uwajibikaji; ukweli na uwazi. Kansa limesali, limetafakari na kushirikishana uzoefu na mang’amuzi kuhusu nyanyaso za kijinsia chini ya uongozi wa Baba Mtakatifu Francisko na kwamba, huu ni wakati wa kuyafanyia kazi katika maisha na utume wa Kanisa maamuzi ambayo maaskofu wamshirikisha na hatimaye, kufikia maamuzi mazito!

Huu ni wakati wa kutekeleza “dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa”. Ukweli na uwazi ni mambo msingi yatakayoliwezesha Kanisa kupambana kikamilifu na kashfa ya nyanyaso za kijinsia. Kwa njia hii, Kanisa litaweza kupyaisha maisha na utume wake na hatimaye, kuondokana si tu na kashfa ya nyanyaso za kijinsia, bali pia matumizi mabaya ya madaraka na dhamiri mfu! Baada ya mkutano huu, yafuatayo yanatarajiwa kutekelezwa na Mama Kanisa: Baba Mtakatifu Francisko anatarajia kuandika Barua Binafsi kuhusu Ulinzi wa Watoto Wadogo, ili kupambana na kashfa hii kutoka katika Sekretarieti kuu ya Vatican.

Waraka huu, utasindikizwa na Sheria Mpya ya Vatican katika mada hii. Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa litachapisha “Vademecum” yaani “Mwongozo” utakaowasaidia Maaskofu Katoliki kufahamu wajibu na dhamana yao. Baba Mtakatifu ameonesha nia ya kutaka kuunda “Kikosi Kazi cha wataalam na Mabingwa” kitakachoyasaidia Mabaraza ya Maaskofu Katoliki kukabiliana na changamoto hii pamoja na kuanzisha sera mbali mbali zitakazosaidia ulinzi wa watoto wadogo. Jumatatu, tarehe 25 Februari 2019, Kamati Kuu ya Mkutano wa Kanisa Kuhusu Ulinzi wa Watoto Wadogo ndani ya Kanisa inakutana na Viongozi waandamizi wa Sekretarieti kuu ya Vatican kuangalia jinsi ya kuanza kutekeleza maamuzi na utashi wa Baba Mtakatifu Francisko.

Hizi ni dalili za matumaini anasema Padre Federico Lombardi, zitakazolisindikiza Kanisa katika maisha na utume wake wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu pamoja na kuwahudumia watoto, kwa kuonesha mshikamano na watu wote. Kanisa litaendelea kushirikiana na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, kashfa hii inang’olewa ndani ya Kanisa na Jamii katika ujumla wake!

Tamko: Padre Lombardi

 

 

25 February 2019, 10:50