Tafuta

Mkutano wa Kanisa kuhusu Ulinzi kwa Watoto Wadogo: Mwenendo wa Kesi na Mkakati wa kuzuia nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa Mkutano wa Kanisa kuhusu Ulinzi kwa Watoto Wadogo: Mwenendo wa Kesi na Mkakati wa kuzuia nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa 

Mkutano Kuhusu Ulinzi wa Watoto: Mwenendo wa kesi & kuzuia

Kashfa ya nyanyaso za kijinsia ni matokeo ya kulega lega katika uteuzi wa majandokasisi katika malezi na majiundo ya kikasisi na maisha ya kuwekwa wakfu. Hizi ni dalili za kuporomoka kwa malezi na tunu msingi za kiutu, kimaadili, kiakili na katika maisha ya kiroho! Upendeleo na aibu kwa Kanisa na matokeo yake ni kushindwa kutekeleza Sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Askofu mkuu Charles Jude Scicluna wa Jimbo kuu la Malta, ambaye pia ni Katibu Mwambata wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa, katika hotuba yake elekezi kwenye mkutano wa Kanisa kuhusu Ulinzi wa Watoto wadogo ndani ya Kanisa, tarehe 21 Februari 2019 amegusia kuhusu dhamana na wajibu katika mchakato wa kesi za nyanyaso za kijinsia na hatua zinazopaswa kuchukuliwa ili kuzuia vitendo hivi katika maisha na utume wa Kanisa!

Katika hotuba yake, amezungumzia sababu zilizopelekea kuibuka kwa kashfa ya nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa; Umuhimu wa kutoa taarifa kuhusu makosa ya kijinsia, uchunguzi wake, adhabu na utekelezaji wa Sheria, kanuni na taratibu za Kanisa pamoja na mbinu mkakati wa kuzuia nyanyaso za kijinsia. Kashfa ya nyanyaso za kijinsia ni matokeo ya kulega lega katika uteuzi wa majandokasisi katika malezi na majiundo ya kikasisi na maisha ya kuwekwa wakfu. Hizi ni dalili za kuporomoka kwa malezi na tunu msingi za kiutu, kimaadili, kiakili na katika maisha ya kiroho! Upendeleo na aibu kwa Kanisa na matokeo yake ni kushindwa kutekeleza Sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa!

Kanisa linapaswa kuanzia sasa kuhakikisha kwamba, linasimamia mambo haya msingi katika maisha na utume wake ili mwanga wa Injili ya Kristo uendelee kuangaza ulimwenguni! Mchakato wa kesi za nyanyaso za kijinsia kwanza kabisa ni kuhakikisha kwamba, taarifa zinatolewa kuhusu makosa ya kijinsia kwa Askofu au kwa Mkuu wa Shirika husika. Protokali itakayotolewa itapaswa kuheshimiwa, kwa kuhakikisha kwamba, sheria, taratibu na kanuni za Kanisa pamoja na Sheria za Nchi zinafuatwa kwa ukamilifu. Uchunguzi wa kesi ufanywe na waatalam na maamuzi yafikiwe kwa umoja. Watuhumiwa na waathirika wasaidiwe kukabiliana na changamoto iliyoko mbele yao na kwamba, hii ni sehemu nyeti sana ya kuweza kukutana na Kristo Yesu katika madonda ya watu: kisaikolojia na katika maisha ya kiroho.

Kuhusu uchunguzi wa makosa ya kijinsia: Baba Mtakatifu Yohane Paulo II, mnamo mwaka 2001 kwa Barua binafsi Motu proprio, Sacramentorum sanctitatis tutela, yaani Ulindaji wa Utakatifu wa Sakramenti, alitoa taratibu za mchakato wa kuendesha kesi hizo katika Mahakama za Kanisa. Ikiwa kama kosa hili ametendewa mtoto mwenye umri chini ya miaka 18, kesi lazima ipelekwe kwenye Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa baada ya Askofu au Mkuu wa Shirika kupata ushauri wa kitaalam. Ufuatiliaji wa kesi hizi utaamriwa na Vatican. Sheria za Nchi hazina budi kuzingatiwa katika mchakato mzima.

Ni wajibu na dhamana ya Askofu mahalia au Mkuu wa Shirika husika kuhakikisha kwamba, anatekeleza kikamilifu maamuzi yaliyotolewa na Mahakama za Kanisa kuhusu kesi iliyokuwa mbele yao na kutangazwa. Waathirika lazima wahudumiwe na Kanisa kwa kuzingatia kanuni na taratibu za haki, ili utakatifu wa maisha uendelee kung’ara ndani ya Kanisa. Askofu mkuu Charles Jude Scicluna anasema, ili kuzuia kashfa ya nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa kuna haja ya kuzingatia mambo yafuatayo: Kwanza ni kuhakikisha kwamba, vijana wanaoteuliwa kujiunga na majiundo na malezi ya kipadre ni wale wenye sifa njema.

Mwongozo wa malezi ya Kipadre unaojulikana kama “Ratio Fundamentalisi Institutionis Sacerdotalis” yaani “Zawadi ya wito wa Kipadre”. Utangulizi wa mwongozo huu unabainisha changamoto iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kama sehemu ya mchakato wa kulinda, kukuza na kudumisha wito na maisha ya Daraja Takatifu ya Upadre. Huu ni wito wenye thamani kubwa katika maisha na utume wa Kanisa unaopaswa kuhudumiwa kwa umakini mkubwa kwa kuheshimu dhamiri nyofu, wajibu unaotekelezwa kwa unyenyekevu na uvumilivu mkubwa, ili kweli Wakleri waweze kung’ara kati pamoja na watu wa Mungu wanaowahudumia!

Viongozi wa kanisa wanapaswa kuzingatia: Kanuni msingi za maisha na wito wa Daraja Takatifu ya Upadre; misingi ya malezi ya Kipadre; Malezi ya awali na endelevu, malezi ya maisha ya kiroho na kiutu. Katika majiundo yao, majandokasisi waelimishwe kuhusu biashara ya binadamu na utumwa mamboleo. Wafundwe kuhusu uhuru wa kibinadamu, kanuni maadili na utu wema. Jumuiya za waamini zielimishwe jinsi ya kuzuia na kupambana na kashfa ya nyanyaso za kijinsia. Askofu awe mstari wa mbele kuchagua vijana wanaofaa katika maisha na utume wa kipadre. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Kanisa halina budi kutambua na kukiri dhambi iliyotendwa na watoto wake; kwa kulaani kwa masikitiko na aibu kuwa vitendo hivi ambavyo vimefanywa na viongozi wa Kanisa. Ni wakati wa kufanya toba na kuomba msamaha wa dhambi, ili kusimama kidete kuweza kuendelea na safari ya toba na wongofu wa ndani!

Askofu Mkuu Scicluna
21 February 2019, 14:33