Mkutano wa Kanisa Kuhusu Ulinzi wa Watoto Wadogo: Dhana ya Sinodi na Uwajibikaji wa pamoja1 Mkutano wa Kanisa Kuhusu Ulinzi wa Watoto Wadogo: Dhana ya Sinodi na Uwajibikaji wa pamoja1 

Mkutano Kuhusu Ulinzi wa Watoto: Uwajibikaji wa Kisinodi

Urika wa Maaskofu, utekelezaji wa dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa; toba na wongofu wa ndani ni mambo msingi katika kupambana na nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa. Kanisa linapaswa kuwa kana “Mama mpendelevu, anayeguswa na mateso pamoja na mahangaiko ya watoto wake, ili kweli liweze kuwa ni chombo cha faraja, upendo na huruma ya Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kardinali Blasé Joseph Cupich, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Chicago, nchini Marekani, katika hotuba yake elekezi, Ijumaa, tarehe 22 Februari 2019 amekazia tena umuhimu wa urika wa Maaskofu na utekelezaji wa “dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa”. Amesema, wazazi wana kifungo kitakatifu cha mahusiano na watoto wao, changamoto na mwaliko wa kujenga utamaduni wa kuwajibika kuwalinda na kuwaendeleza watoto. Kuna umuhimu wa kudumisha utamaduni wa kusikiliza kwa makini; kupata ushuhuda kutoka kwa waamini walei; kufikiri na kutenda katika urika wa Maaskofu.

Kanisa linapaswa kuwasindikiza waathirika katika hija ya maisha yao ya ndani; Kanisa lianzishe miundo mbinu makini kama sehemu ya utekelezaji wa Sheria, kanuni na taratibu kama zinavyofafanuliwa na viongozi wa Kanisa: kwa kuweka viwango vya uchunguzi pamoja na kutoa taarifa ya shutuma za nyanyaso za kijinsia katika maeneo husika.  Urika wa Maaskofu, utekelezaji wa dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa; toba na wongofu wa ndani ni mambo msingi katika kupambana na nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa.

Kardinali Blasé Cupich anakaza kusema, Kanisa linapaswa kuwa kama “Mama mpendelevu", anayeguswa na mateso pamoja na mahangaiko ya watoto wake, ili kweli liweze kuwa ni chombo cha faraja, upendo na huruma ya Mungu. Kanisa halina budi kujenga utamaduni wa kusikiliza kwa makini waathirika wa nyanyaso za kijinsia. Kanisa liwe na ujasiri wa kuwaendea wale wote walionyanyaswa ili kuweza kuwasikiliza. Kanisa liwe makini ili kuhakikisha kwamba, nyanyaso za kijinsia hazijirudii tena na kwamba, makosa ya wakleri na watawa kwa miaka iliyopita, yalisaidie Kanisa kuwajibika kutokana na uzembe wake!

Kanisa liwe na ujasiri wa kusikiliza ushuhuda kutoka kwa waamini walei, ili kuliwezesha kuendelea kutekeleza dhamana na utume wake, kwa kung’oa mambo yale ambayo yamepelekea kuibuka kwa kashfa ya nyanyaso ndani ya Kanisa. Utekelezaji wa dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa, uliwezeshe Kanisa kuwashirikisha zaidi watu wa Mungu. Huu ni mwelekeo unaokazia umoja na mshikamano; mawasiliano katika ukweli na uwazi pamoja na kuwajibika. Umoja na mshikamano kati ya Askofu, Mabaraza ya Maaskofu, Sekretarieti kuu ya Vatican pamoja na Khalifa wa Mtakatifu Petro ni muhimu sana katika mapambano dhidi ya kashfa ya nyanyaso za kijinsia.

Maaskofu katika urika wao wanaweza kutenda na kusaidiana katika hali ya unyenyekevu, ukweli na uwazi; kwa kuwasindikiza waathirika wa nyanyaso za kijinsia katika maisha yao ya kiroho! Kanisa lionje na kuguswa na madonda ya mahangaiko ya waathirika wa nyanyaso za kijinsia, tayari kutoa hukumu ya haki, kama Mama mwenye huruma na upendo anayewatakia watoto wake mema na ustawi wa maisha. Kanisa liwe makini, ili wakleri na watawa wasichafuliwe sifa na heshima yao kwa shutuma zilizokuwa na msingi wala ukweli ndani yake.

Kardinali Blasé Joseph Cupich, anakaza kusema, kanuni za “dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa zinafumbatwa katika: Kusikiliza, ushuhuda wa waamini walei, urika wa Maaskofu pamoja na kuwasindikiza waathirika ni kati ya changamoto pevu zinazotolewa na Baba Mtakatifu Francisko. Kunapaswa kuwepo kwa taasisi na mfumo wa sheria unaowawajibisha viongozi wa Kanisa kama ambavyo umefafanuliwa na Baba Mtakatifu Francisko katika Barua yake Binafsi ya kichungaji, “Kama Mama mpendelevu” iliyochapishwa Juni, 2016, anasema nyanyaso za kijinsia ni kati ya makosa makubwa ambayo yamebainishwa barabara kwenye Sheria, kanuni na taratibu za Kanisa.

Baba Mtakatifu anapenda kuwahimiza viongozi wa Kanisa kuwa macho dhidi ya nyanyaso za kijinsia wanazoweza kufanyiwa watoto wadogo; anaonesha hatua zitakazochukuliwa ili kutekeleza vifungu vya Sheria ambavyo viko tayari kwenye Sheria za Kanisa Namba 193§ 1 na Sheria za Kanisa la Mashariki Namba 975§1. Mkazo hapa ni wajibu wa viongozi wa Kanisa katika kutekeleza dhamana na utume wao! Malezi na majiundo endelevu kwa Maaskofu ni mambo muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa.

Mama Kanisa katika kuendeleza Utume wake wa kutaka kudhibiti uhalifu unaoweza kutendwa na waamini: lengo likiwa ni kumrekebisha mhalifu; kutenda haki kwa waliokosewa; na kuondoa kashfa (Rej. CIC, c. 1341). Kati ya makosa ya uhalifu, yapo yale ambayo yanatambuliwa kuwa ni makosa makubwa ya uhalifu, Delicta graviora, na yametengwa ili kushughulikiwa, sio tena na Askofu Jimbo wala Wakuu wa Mashirika ya Kitawa na kazi za kitume, bali na Mahakama maalumu ya Baba Mtakatifu. Mahakama hiyo ni Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa. Makosa husika yanayoshughulikiwa na Mahakama hiyo ni makosa dhidi ya Sakramenti ya Kitubio, dhidi ya Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na dhidi ya Amri ya sita ya Mungu.

Kuhusu Sakramenti ya Kitubio, makosa ambayo mchakato wake umetengwa ili kushughulikiwa na Kiti Takatifu, yaani Mahakama ya Baba Mtakatifu ni: makosa ya padri kuvunja siri ya kitubio, kumtongoza kimapenzi kwa maneno au ishara mwamini anayekuwa katika kitubio, au kutumia kwa namna yeyote maongezi ya kwenye kitubio kwa kumuumiza aliyetubu kwake. Kwa upande wa Ekaristi Takatifu, ni kukejeli au kutoweka heshima kwa Sakramenti hiyo kwa nia ya kukufuru. Kosa hili laweza kutendwa ama na waamini walei ama na wakleri. Makosa dhidi ya Amri ya sita ya Mungu, yanawahusu wakleri wanaojihusisha na masuala ya ngono dhidi ya watoto wadogo hata kama ni kwa njia ya mtandao, pedopornographia (CIC, c. 1395§2)

Baba Mtakatifu Yohane Paulo II, mnamo mwaka 2001 kwa Barua binafsi Motu proprio, Sacramentorum sanctitatis tutela, yaani Ulindaji wa Utakatifu wa Sakramenti, alitoa taratibu za mchakato wa kuendesha kesi hizo katika Mahakama za Kanisa. Mnamo mwaka 2010 Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI kwa Tamko, Reformatio Normae gravioribus delictis, juu ya marekebisho ya kanuni za makosa makubwa ya uhalifu, aliziboresha taratibu hizo kwa baadhi ya vipengele ambavyo vilikuwa havikueleweka barabara!

Kardinali Blasé Joseph Cupich, anasema, kuna haja ya kuweka viwango, kutoa taarifa ya nyanyaso za kijinsia pamoja na kuhakikisha kwamba, zinatekelezwa kikamilifu kwa kuheshimu utu wa waathirika; ukweli na uwazi; bila mtu kutengwa; uwajibikaji upewe kipaumbele cha kwanza; ushirikiano katika taaluma ya Sheria za Kanisa ili haki iweze kutendeka na maamuzi kufikiwa haraka iwezekanavyo bila kucheleweshwa na matokeo yake kutumwa Vatican na hatimaye, Khalifa wa Mtakatifu Petro kuyatolea maamuzi.

Kardinali Cupich: Uwajibikaji
22 February 2019, 11:32