Tafuta

Vatican News
Tahariri ya Andrea Tornielli: Mkutano wa Kanisa Kuhusu Ulinzi wa Watoto Wadogo! Tahariri ya Andrea Tornielli: Mkutano wa Kanisa Kuhusu Ulinzi wa Watoto Wadogo! 

TAHARIRI: Mkutano wa Kanisa Kuhusu Ulinzi wa Watoto Wadogo!

Kanisa lihakikishe kwamba, linang’oa ndago za kashfa ya nyanyaso za kijinsia katika maisha na utume wa Kanisa, kwa kuuangalia ukweli bila “kupepesa macho hata kidogo”. Huu ni mwaliko wa kuangalia “Madonda Matakatifu ya Yesu” yanayoendelea kujitokeza katika Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa, ili kufikiri, kuamua na kitenda kwa pamoja kama familia ya Mungu inayowajibika!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, umefika wakati kwa Kanisa kuhakikisha kwamba, linang’oa ndago za kashfa ya nyanyaso za kijinsia katika maisha na utume wake, kwa kuuangalia ukweli bila “kupepesa macho hata kidogo”. Huu ni mwaliko wa kuyaangalia “Madonda Matakatifu ya Yesu” yanayoendelea kujitokeza katika Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa, ili kufikiri, kuamua na kutenda kwa pamoja kama familia ya Mungu inayowajibika!

Umefika wakati wa kuondokana na woga ambao umepelekea baadhi ya viongozi wa Kanisa kujenga utamaduni wa kulindana na kwamba, kwa sasa ukweli na uwazi ndio sera zinazoliongoza Kanisa ili kuendelea kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia! Kanisa liwajibike kutunza historia ili kuendeleza mchakato wa ukweli, uwazi na uwajibikaji! Dhana ya kulindana imepitwa na wakati. Changamoto iliyojitokeza sehemu mbali mbali za dunia dhidi ya Kanisa ni kilio kinachohitaji jibu makini linalofumbatwa katika toba na wongofu wa ndani, tayari kuambata utakatifu wa maisha!

Andrea Tornieli, Mhariri Mkuu wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano katika Tahariri yake baada ya kuhitimishwa kwa Mkutano wa Kanisa Kuhusu Ulinzi wa Watoto Wadogo anarejea tena kwenye maneno yaliyosemwa na Baba Mtakatifu Francisko kuhusu nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa kwamba, “Hapa si bure, kuna mkono wa Shetani”. Baba Mtakatifu anasema, nyanyaso za kijinsia ni janga ambalo linawaandama watu wote, ndiyo maana Baba Mtakatifu akataka Kanisa kushirikiana ili kujibu kashfa hii kwa kutumia “dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa”.

Mkutano huu imekuwa ni fursa ya kuwasikiliza waathirika wa nyanyaso za kijinsia; kusali na kuomba msamaha kwa Mwenyezi Mungu na wale watu ambao hawakutendewa haki. Utambuzi huu anasema Andrea Tornieli haulengi kufifisha na kusahau ufafanuzi uliotolewa; au kupunguza uwajibikaji wa kiongozi mmoja mmoja au katika ujumla wao kama Taasisi ya Kanisa, bali Baba Mtakatifu anataka dhana hii ieleweke katika upana na ukubwa wake! Baba Mtakatifu amezungumzia kuhusu nyanyaso za kijinsia sehemu mbali mbali za dunia na kwa masikitiko makubwa hata ndani ya Kanisa.

Huu ni ushuhuda unaotolewa na Baba ambaye pia ni Mchungaji mkuu anayetaka kuonesha madhara ya nyanyaso za kijinsia katika maisha na utume wa Kanisa! Nyanyaso hizi ni uhalifu dhidi ya utu na heshima ya binadamu na kwamba, kwa Kanisa, hii ni kashfa! Hii inatokana na ukweli kwamba, wazazi na walezi waliokuwa wamewadhaminisha watoto kwa viongozi wa Kanisa, ili wawasaidie katika malezi ya imani, hao ndio waliowageuzia kisogo na kuanza kuwasababishia madonda makubwa katika maisha. Katika muktadha wa hasira na chuki ya watu wa Mungu dhidi ya Kanisa anasema Baba Mtakatifu, viongozi wa Kanisa wanapaswa kutafakari kuhusu hasira ya Mungu juu ya mapadre na watawa ambao wamesababisha kashfa hizi katika maisha na utume wa Kanisa.

Kilio cha waathirika hakikuweza kusikilizwa na Kanisa na kwamba, machozi yao yamekuwa kama “machozi ya Samaki” yameishia majini! Maisha ya watu hawa yameharibiwa kutokana na baadhi ya mapadre na watawa kugeuka kuwa ni watu wa kutisha, kwa kumezwa na malimwengu pamoja na matumizi mabaya ya madaraka. Ni mambo ambayo yamesikika masikioni mwa Maaskofu na Wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume, ili kufyekelea mbali sababu ambazo zilizopelekea kuhalalishwa kwa vitendo hivyo; ugumu wa mioyo na majadiliano ya kifundi, ili kupindisha ukweli uliotolewa kwenye takwimu!

Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake ya mwisho wa mkutano huu, amewashukuru na kuwapongeza mapadre na watawa wengi wanaoendelea kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu; kwa kuwaelimisha watoto wadogo pamoja na kuwasaidia maskini. Kwa sasa Kanisa lina ufahamu na uelewa mpana zaidi kuhusu kashfa ya nyanyaso za kijinsia. Ni muda wa kufanya toba, kuomba msamaha kwa kujikita katika wongofu wa ndani, tayari kuambata utakatifu wa maisha na kuendelea kufuata nyayo za Kristo Yesu!

Ni wakati muafaka wa kuanza utekelezaji wa maamuzi yaliyofikiwa bila kuchelewa sana. Ukubwa wa kashfa hii unalielemea sana Kanisa. Dhamana hii inapaswa kutekelezwa kwa njia ya upya wa maisha, ili kweli, maeneo ya maisha na utume wa Kanisa yaweze kuwa salama kwa malezi na majiundo makini ya watoto, kwa matumaini kwamba, mchakato huu utaweza kugusa hata maisha ya watu katika jamii mbali mbali.

Tahariri: Tornielli
26 February 2019, 11:03