Umuhimu wa Vatican katika muktadha wa kimataifa tangu mwaka 1929-2019: Uhuru wa kidini & Kuabudu; Utu, heshima na haki msingi za binadamu! Umuhimu wa Vatican katika muktadha wa kimataifa tangu mwaka 1929-2019: Uhuru wa kidini & Kuabudu; Utu, heshima na haki msingi za binadamu! 

Kumbu kumbu ya Miaka 90 ya Mkataba wa Lateran-1929-2019

Miaka 90 ya Mkataba wa Lateran: “Umuhimu wa Vatican katika muktadha wa Jumuiya ya Kimataifa 1929 – 2019”, Kardinali Parolin amekazia: huru wa kuabudu na wa kidini, utu, heshima, haki msingi za binadamu, ustawi, mafao na maendeleo ya wengi. Hizi ni changamoto ambazo zimepewa kipaumbele cha pekee na Vatican katika kipindi cha miaka 90 ya uwepo na utume wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake kwa wanadiplomasia wanao wakilisha nchi pamoja na mashirika ya kimataifa mjini Vatican kwa mwaka 2019 alihimiza zaidi  kuhusu mchakato wa ujenzi wa: amani, urafiki, ushirikiano na mshikamano kati ya watu baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia. Mwaka 2019 Nchi ya Vatican moja ya nchi ndogo kabisa duniani, tarehe 11 Februari, 2019 inatimiza miaka 90 tangu Kanisa Katoliki lilipotiliana sahihi Mkataba na Serikali ya Italia “Patti Lateranensi” iliyokuwa inaibuka baada ya kutenganisha Kanisa na Serikali.

Mkataba wa Lateran uliifanya Vatican kutambuliwa rasmi kama nchi huru yenye uwezo wa kujiamria mambo yake yenyewe katika medani za kimataifa bila kuingiliwa na Serikali ya Italia. Papa Pio XI alilitaka Kanisa kuendelea kushiriki kikamilifu katika ustawi, maendeleo na mafao ya familia ya Mungu nchini Italia: kiroho na kimwili; kwa kutumia amana na utajiri wake wa kihistoria, kitamaduni na kisanaa; mambo yanayofumbatwa katika ukristo. Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuihakikishia Italia uwepo wake wa karibu kwa njia ya sala, ili kweli nchi ya Italia,  iendelee kuwa aminifu kwa Mapokeo pamoja kupyaisha udugu wa mshikamano ambao umeipambanua Italia kwa miaka mingi.

Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, hivi karibuni katika hotuba yake elekezi kwenye Kongamano la kitaifa lililoandaliwa na Chuo Kikuu cha LUMSA kilichoko Roma na kuongozwa na mada “Umuhimu wa Vatican katika muktadha wa Jumuiya ya Kimataifa 1929 – 2019”, amekazia: uhuru wa kuabudu, uhuru wa kidini, utu, heshima, haki msingi za binadamu, ustawi, mafao na maendeleo ya wengi. Amesema, hizi ni changamoto ambazo zimepewa kipaumbele cha pekee na Vatican katika kipindi cha miaka 90 ya uwepo na utume wake.

Vatican imekazia umuhimu wa viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kuheshimu dhamiri nyofu za watu, mahali patakatifu sana katika maisha ya mwanadamu! Ikumbukwe kwamba, Haki msingi za binadamu zinazozungumziwa hapa ni zile zinavyofafanuliwa katika Tamko la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa na wala si ukoloni wa kiitikadi unaotaka kupenyezwa kwa mataifa maskini duniani! Kardinali Parolin, ametumia fursa ya mkutano huu, kufafanua vipengele mbali mbali vilivyomo kwenye Mkataba wa Lateran kwa kusema, kwamba, Mkataba huu, umekuwa ni ngome na ulinzi thabiti kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro, kuweza kutekeleza dhamana na utume wake kwa uhuru zaidi, bila kuingiliwa na chombo chochote kile!

Dhamana na wito wa Vatican katika diplomasia, unafumbatwa katika utume wake wa maisha ya kiroho, kimaadili na utu wema kwa ajili ya familia ya Mungu sehemu mbali mbali za dunia. Vatican haipendi kuingilia mambo ya ndani ya nchi,  bali inapenda kusikilizwa kwa makini, kama chombo cha ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu, dhamana inayotekelezwa kwa unyoofu na unyenyekevu mkuu! Itakumbukwa kwamba, Mkataba wa Lateran, ulifanyiwa marekebisho ya msingi kunako mwaka 1984 wakati wa uongozi wa Mtakatifu Yohane Paulo II,  ili kuendana na Sheria, Kanuni na Taratibu zilizokuwa zimeibuliwa na Mababa wa Mtaguso Mkuu wa pili wa Vatican. Ushirikiano kati ya Serikali ya Italia na Vatica unaolenga kulinda, kudumisha na kutetea utu, heshima na haki msingi za binadamu. Ni mkataba unaojipambanua kwa kukazia uhuru wa kuabudu na uhuru wa kidini.

Nchi ya Vatican inapaswa kuendelea kuwepo, ikiwa huru katika kujiamria mambo yake yenyewe, ili kutekeleza utume wake katika maisha ya kiroho, kiutu na kimaadili ulimwenguni kote. Mifumo ya kisiasa na sera mbali mbali zinazogusa utu, heshima na maisha ya mwanadamu na hata wakati mwingine kuzama katika undani wake. Vatican imekuwa mstari wa mbele kukemea uhuru usiokuwa na mipaka wala uwajibikaji; imekazia majadiliano katika ukweli na uwazi na mshikamano wa kidugu. Vatican ni kati ya nchi ambazo ziko mstari wa mbele kutetea haki msingi za binadamu, kama mtu mmoja mmoja au taifa.Zote hizi ni kati ya sababu ambazo zinahalalisha uwepo wa Nchi ya Vatican ili iweze kutekeleza majukumu yake katika misingi ya ukweli na haki.

Vatican kutokana na ushiriki wake kwenye Jumuiya ya Kimataifa inaendelea kutoa mchango mkubwa unaofumbata maendeleo endelevu na fungamani binadamu pamoja na kuhakikisha kwamba, uhuru wa kuabudu na ule wa kidini unazingatiwa na kuheshimiwa na Jumuiya ya Kimataifa. Mama Kanisa anapenda kutekeleza wajibu na utume wake akiwa huru kabisa, ili kuchangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Uhuru wa kidini ni haki ya kila dini au dhehebu lolote lile kadiri ya sheria, kanuni na taratibu za nchi husika. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wamekazia umuhimu wa Kabnisa na Serikali kushirikian ana kushikamana kwa ajili ya kuwahudumia watu wa Mungu: kiroho na kimwili.

Uhusiano kati ya Kanisa na Serikali unategemea kwa kiasi kikubwa: hali ya kitamaduni, kijamii, kisiasa na kihistoria kwa nchi husika. Mahali ambapo utawala wa sheria unaheshimiwa, Kanisa limekuwa likitekeleza wajibu kwa ajili ya maendeleo ya watu kiroho na kimwili. Lakini, katika baadhi ya nchi, Kanisa limekuwa likikumbana na madhulumu na sera za kibaguzi zinazolibeza Kanisa kwa kudhani kwamba, linaingilia mambo yake. Kanuni ya mpe Kaisari yaliyo ya Kaisari na Mungu yaliyo ya Mungu inapaswa kuwaongoza wanasiasa wenye misimamo mikali ya maisha. Kanisa, daima limeendelea kusoma alama za nyakati na kwamba, Khalifa wa Mtakatifu Petro anapaswa kutekeleza dhamana na utume wake katika mazingira huru kabisa.

Kamwe, Khalifa wa Mtakatifu Petro, hatasita kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; haki msingi za wakimbizi na wahamiaji pamoja na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote na kwamba, misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu ni muhimu sana katika ustawi na maendeleo ya wengi! Biashara haramu ya silaha duniani, biashara ya binadamu na viungo vyake pamoja na mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo ni kati ya mambo ambayo Baba Mtakatifu Francisko ameyavalia njuga katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro!

Mkataba wa Lateran 90Yrs

 

 

11 February 2019, 09:46