Tafuta

Kardinali George Pell atiwa hatiani kwa kosa la nyanyaso za kijinsia nchini Australia! Kardinali George Pell atiwa hatiani kwa kosa la nyanyaso za kijinsia nchini Australia! 

Kardinali George Pell atiwa hatiani kwa nyanyaso za kijinsia!

Kesi hii kwa mara ya kwanza iliibuliwa kunako mwaka 2014, Kardinali Pell alipotakiwa kwenda kutoa ushahidi Mahakamani kwa shutuma ya kuwalinda mapadre waliotuhumiwa kujihusisha na nyanyaso za kijinsia. Wakati wote, Kardinali Pell amekanusha madai haya kwamba, hakuwa na taarifa zozote kuhusu nyanyaso za kijinsia zilizotokea katika Jimbo Katoliki Ballarat.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mahakama nchini Australia imetia hatiani Kardinali George Pell, mwenye umri wa miaka 77 kwa kupatikana na kosa la kunyanyasa watoto wadogo, kwenye miaka 1990 wakati alipokuwa Askofu msaidizi wa Melbourne kati ya mwaka 1987-1998, kabla ya kuteuliwa kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Melbourne na kuongoza kati ya mwaka 1996-2001. Kuanzia mwaka 2001-2014 alikuwa ni Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Sydney nchini Australia; na kuteuliwa kuwa Kardinali kunako mwaka 2003. Kunako mwaka 2013 kama sehemu ya mageuzi makubwa kwenye Sekretarieti kuu ya Vatican, Baba Mtakatifu Francisko akamteua Kardinali Pell kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uchumi!

Kesi hii kwa mara ya kwanza iliibuliwa kunako mwaka 2014, Kardinali Pell alipotakiwa kwenda kutoa ushahidi Mahakamani kwa shutuma ya kuwalinda mapadre waliotuhumiwa kujihusisha na nyanyaso za kijinsia. Wakati wote, Kardinali Pell amekanusha madai haya kwamba, hakuwa na taarifa zozote kuhusu nyanyaso za kijinsia zilizotokea katika Jimbo Katoliki Ballarat. Kunako mwaka 2016 Kardinali akahojiwa mjini Roma na tarehe 26 Julai 2018 akatakiwa kuwepo Mahakamani ili kuweza kujitetea mwenyewe.

Kardinali George Pell amekuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya nyanyaso za kijinsia sanjari na kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Baba Mtakatifu Francisko. Baraza la Maaskofu Katoliki Australia limeonesha mshikamano wake wa dhati na Kardinali Pell na kwamba, sheria ni msumeno; watu wote wako sawa mbele ya sheria. Maaskofu wanasema, wana amini utendaji wa Mahakama. Mawakili wa Kardinali Pell tayari wamekata rufaa, huku wakiamini kwamba, haki itatendeka! Maaskofu wanaendelea kusali na kuwaombea wale wote walioathirika kwa nyanyaso za kijinsia nchini humo!

Taarifa iliyotolewa na Dr. Alessandro Gisotti, Msemaji mkuu wa muda wa Vatican inaeleza kwamba, Vatican inapenda kuchukua fursa hii kuungana na Baraza la Maaskofu Katoliki Australia kutambua uamuzi wa Mahakama nchini humo, hata kama habari hizi zimepokelewa kwa majonzi makubwa sehemu mbali mbali za dunia. Vatican inasubiri hukumu ya mwisho, baada ya Kardinali Pell kukata rufaa! Ili kuhakikisha kwamba, haki inatendeka, Baba Mtakatifu Francisko kwa kuchukua tahadhari, kuanzia sasa amemsimamisha Kardinali George Pell kufanya shughuli za kichungaji hadharani na wala haruhisiwi kukutana tena na watoto wadogo kadiri ya sheria, kanuni na taratibu zilizoko!

Kardinali Pell
26 February 2019, 10:35