Tafuta

Vatican News
Sakata la mapadre na watawa wenye watoto mitaani: ulinzi, ustawi na mafao ya mtoto yanapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza! Sakata la mapadre na watawa wenye watoto mitaani: ulinzi, ustawi na mafao ya mtoto yanapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza!  (Vatican Media)

Useja na sakata la Mapadre na Watawa wenye watoto mitaani!

Hata kama kuna mapadre na watawa ambao wamekuwa na uhusiano wa kimapenzi na wanawake kiasi cha kubahatika kupata watoto, lakini ikumbukwe kwamba, Useja ni zawadi na neema ya pekee kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa anasema Kardinali Stella. Kumbe, hakuna wazo la kutoa ruhusa kwa mapadre kuamua kuoa au kuendelea kuwa waseja. Huu ndio msimamo wa Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Dr. Vincent Doyle ni muasisi wa “Coping” yaani Chama cha Kimataifa cha Watoto wa Mapadre na Watawa ambaye amekuwepo mjini Roma kuhudhuria Mkutano wa Kanisa Kuhusu Ulinzi wa Watoto Wadogo uliohitimishwa, tarehe 24 Februari 2019 kwa hotuba kali kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko kuhusu kashfa ya nyanyaso za kijinsia ilivyochafua maisha na utume wa Kanisa! Chama hiki kimekuwa mstari wa mbele kuwasaidia watoto wa mapadre na watawa sehemu mbali mbali za dunia. Chama hiki kinashirikiana na uongozi wa Kanisa ili kulinda na kutetea utu na heshima ya watoto hawa ambao wanapaswa kupewa mahitaji yao msingi. Chama kinaendelea kujipambanua katika kudhibiti nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto sehemu mbali mbali za dunia.

Kardinali Beniamino Stella, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Wakleri katika mahojiano maalum na Andrea Tornelli, Mhariri mkuu wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano anasema, sheria, taratibu, kanuni na mwongozo ulitolewa na Baraza lake wakati Kardinali Claudio Hummes alipokuwa Mwenyekiti wa Baraza, chini ya uongozi wa Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI. Wakleri ambao wamefanikiwa kupata watoto wakiwa chini ya umri wa miaka 40, wanapaswa kuondolewa wadhifa na madaraka yao ya Kipadre, ili kupata muda mrefu zaidi wa kutunza watoto wao. Hii inatokana na ukweli kwamba, watoto wana haki ya kuwa na wazazi wao wa pande zote mbili yaani: Baba na Mama.

Huu ndio mwelekeo ambao pia umeoneshwa na Baba Mtakatifu Francisko katika mahojiano yaliyochapishwa na kuwa kitabu kati yake na Rabbi Abraham Skorka, yaani haki ya mtoto lazima ipewe kipaumbele cha kwanza! Watoto wanapaswa kuwezeshwa kiuchumi pamoja na kusaidiwa malezi, makuzi na elimu makini. Yaani huu ni wajibu wa baba mzazi kwa mtoto katika umri wa miaka ile ya awali. Kwenye Baraza la Kipapa la Wakleri kuna “Mwongozo wa Kiufundi” unaopaswa kutumika kwa ajili ya kuamua kesi zinazowahusu mapadre wenye watoto mitaani. Ni mwongozo unaotolewa kwa Mabaraza ya Maaskofu na Maaskofu mahalia wanaoshughulikia kesi kama hizi. Mwongozo huu unamwezesha Padre mwenye mtoto au watoto kuondolewa nyadhifa zake za kipadre haraka iwezekanvyo mara tu kesi hii inapomfikia Baba Mtakatifu, ili kumwezesha padre huyo kuwa karibu na mtoto pamoja na mama watoto wake!

Wakati mwingine inatokea kwamba, Mapadre wenye watoto wanaendelea kuwa na watoto bila kuomba ridhaa ya Kanisa kuondolewa wadhifa wao hata kama wanatimiza wajibu wao kiuchumi! Kanisa linakazia umuhimu wa watoto kuwa na wazazi wao wanaowajibika kuwatunza na kuwalea barabara. Kesi kama hii ikiwasilishwa kwenye Baraza, mchakato utaanza mara moja na hatimaye, padre mhusika kuwajibishwa kwa kutambua kwamba, kimsingi mtoto ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Kwa mapadre walioko kwenye madhehebu ya Kilatini, kisheria, hawaruhusiwi kuwa na watoto wa kuzaa. Kesi kama hizi, zinapaswa kufikiriwa sana na Maaskofu mahalia pamoja na wakuu wa Mashirika ya Kazi za Kitume, ili hatimaye kufanya mang’amuzi ya busara kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa.

Hata kama kuna mapadre na watawa ambao wamekuwa na uhusiano wa kimapenzi na wanawake kiasi cha kubahatika kupata watoto, lakini ikumbukwe kwamba, Useja ni zawadi na neema ya pekee kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa anasema Kardinali Stella. Kumbe, hakuna wazo la kutoa ruhusa kwa mapadre kuamua kuoa au kuendelea kuwa waseja. Huu ndio msimamo wa Kanisa tangu kwa Mtakatifu Paulo VI hadi Baba Mtakatifu Francisko. Katika hali na mazingira kama haya, Padre atambue wajibu na dhamana yake kwa mtoto! Ustawi, maendeleo, mafao, malezi na makuzi yake ni mambo msingi yanayopewa msukumo wa pekee na Kanisa!

Mapadre Wenye Watoto

 

27 February 2019, 15:01