Tafuta

Maduro anaomba msaada wa kuwapo mchakato wa upatanisho katika nchi ya Venezuela Maduro anaomba msaada wa kuwapo mchakato wa upatanisho katika nchi ya Venezuela 

Kard.Parolin:Maduro amemwandikia Papa akiomba mazungumzo ya upatanisho!

Kutoka Abu Dhabi,Katibu wa Vatican amethibitisha juu ya barua ya Maduro akimwomba Baba Mtakatifu Francisko atoe wito wa mchakato wa mazungumzo kwa ajili ya amani nchini Venezuela

Na Sr. Angela Rwezaula -Vatican

Kuhusiana  na kipeo cha nchi ya Venezuela hasa ya kiongozi Maduro,msemaji mkuu wa mpito wa vyombo vya habari Bwana Alessandro Gissotti amethibitisha kuwa, wakiwa Abu Dhabi, Katibu wa Vatican Kardinali Pietro Parolin ametoa uthibitisho wa Baba Mtakatifu Francisko kupokea barua kutoka kwa Maduro. Msemaji wa Vatican Bwana Gissotti amethibitisha hayo kwa waandishi wa habari, walotaka kujua kama ni kweli, taarifa iliyotolewa katika vyombo vya habari kuhusu mahojiano na rais Maduro, aliyekuwa amesema kwamba ametuma barua kwa Baba Mtakatifu akimwomba aweze kusaidia mchakato wa mapatano ya nchi ya Venezuela.

Rais wa Baraza la Maaskofu nchini Venezuela kuhusu ukosefu wa msimamo wa kisiasa na kijamii

Na Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki nchini Venezuela Askofu Mkuu José Luis Azuaje, wa jimbo la Maracaibo amewaelekeza wawakilishi wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Binadamu na Tume ya Juu ya haki za binadamu ili kufikiria kuwa ni fursa ya kungilia kati katika kipeo cha Venezuela ambacho kwa sasa hakishikiki. Wito wa Rais wa Baraza la Maaskofu wa Venezuela (CEV) uliotolewa katika tovuti ya Jimbo Kuu la Santiago ya Chile unaoonesha kwamba wanapaswa watambue kuwa kuna watu, lakini ambao kwa sasa wamegeuka kuwa kitu. Ni watu wanao hitaji mabadiliko na wanasubiri, na kwa maana hiyo shughuli  kama Kanisa anasema, ni ile ya kuwafanya watu wawe na dhamiri  zaidi kwa njia ya mafundisho jamii ya Kanisa.

Wito katika Umoja wa Mataifa wasaidie nchi ya Venezuela

Kuhusiana na kuingilia kati kwa namna ya pekee wa Tume ya juu ya Bachelet, Askofu Mkuu Azuaje anathibitisha kuwa yote hayo yanawezekana kutafuta njia ya mapatano na kuweza kuondoa mikanda ambayo imewafunga, ambayo inaendelea kuzaa vurugu. Mashirika ya kimataifa yapo kwa sababu hiyo. Lakini daima kukubaliana na watu wa Venezuela ili kuepuka hatari ambayo inaweza kuleta vurugu kubwa zaidi.

Umoja wa Mataifa hautaegemea kundi lolote katika kipeo cha Venezuela

Tarehe 4 Februari 2019 Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Antonio Guterres amesema kuhusu hali ya Venezuela kuna hatua kadhaa zilizoanzishwa na makundi mbalimbali katika kusaka suluhu ya mgogoro unaoendelea nchini humo. Amethibitisha ya kwamba Umoja wa Mataifa umewasiliana na makundi hayo lakini hautofungama na kundi lolote:“Umoja wa Mataifa umeamua kutokuwa sehemu yoyote ya makundi haya ili kuendelea kutoa uaminifu wa kazi za ofisi yetu kwa pande zote husika na kuweza kwa ombi lao kusaidia kusaka suluhu ya kisiasa.”

Bwana Guaidó ambaye ni kiongozi wa upinzani, tarehe 23 mwezi Januari alijitangaza kuwa rais wa muda wa Venezuela, wakati huo Rais Maduros aliapishwa rasmi kuendelea na wadhifa wa urais kufuatia uchaguzi uliofanyika nchini humo mwezi Mei mwaka jana. Tayari Marekani na mataifa mengine ya Amerika ya Kusini yametangaza kumtambua Bwana Guaidó, huku Muungano wa Ulaya ukitaka Rais Maduros aitishe upya uchaguzi huru na wa haki la sivyo nao watachukua hatua kwa mujibu wa kipengele namba 233 cha katiba ya Venezuela kinachotambua uwepo wa Kaimu Rais. Vile vile nchi ya Uholanzi pamoja na Hipania, Uingereza,Ujerumani, Ufaransa, Austria,Sweden,Lithuania na Danimark,linamtambua Guaidó kama rais halisi wa nchi. Hata hivyo Urusi na mataifa mengine kama vile Afrika Kusini na Equatorial Guinea zimesema suala la Venezuela ni suala la ndani ya nchi hiyo na halipaswi kuingiliwa.

Mtaalam maalum wa Umoja wa Mataifa ana hofu ya vikwazo dhidi ya Venezuela

Na Mtalaamu maalum wa Umoja wa Mataifa amesema vikwazo vilivyowekwa dhidi ya Venezuela si jibu la mzozo unaoendelea nchini humo na badala yake vita sababisha njaa na ukosefu wa huduma za matibabu. Idriss Jazairy ambaye anahusika na haki za binadamu zikiukwazo kutokana na vikwazo, amesema hayo kufuatia hatua ya Marekani kuwekea vikwazo kampuni ya mafuta ya taifa nchini Venezuela. Kupitia taarifa iliyotolewa mapema wiki hii na ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, OHCHR, huko Geneva, Uswisi, Bwana Jazairy ameonesa hofu kubwa zaidi kufuatia ripoti ya kwamba vikwazo hivi vinalenga kubadili serikali ya Venezuela. Mashinikizo, kupitia nguvu za kijeshi au kiuchumi kamwe hayapaswi kutumiwa ili kubadili serikali ya nchi huru. Matumizi ya vikwazo yanayofanywa na mataifa ya kigeni ili kubadili serikali iliyochaguliwa ni ukiukwaji wa maadili ya sheria za kimataifa, amethibitisha.

Aidha Bwana Jazairy ametoa wito kwa jamii ya kimataifa kusaka mazungumzo na Venezuela ili kupata  jibu la kudumu dhidi ya changamoto kuu zinazokabili taifa hilo. Mtaalamu huyo amesema mazungumzo ni muhimu kwa kuwa vikwazo vya kiuchumi vinazidisha janga la uchumi wa Venezuela akiongeza kuwa, vinachochea mlipuko  wa bei kupita kiasi na kuporomoka kwa bei ya mafuta. Akisisitiza zaidi amesema huu ni wakati wa kuonyesha utu kwa wanavenezuela kwa kuendeleza mbinu za kupata huduma za dawa na chakula badala ya kuweka mbinu za kuzuia wananchi kupata huduma hizo.

05 February 2019, 10:52