Mwaka 2018 utakumbukwa kuwa ni mwaka "annus horribilis" kutokana na mauaji ya wamisionari wengi Barani Afrika. Mwaka 2018 utakumbukwa kuwa ni mwaka "annus horribilis" kutokana na mauaji ya wamisionari wengi Barani Afrika. 

Wamisionari 40 wameuwawa katika kipindi cha mwaka 2018

Takwimu zinaonesha kwamba, Mapadre waliouwawa ni 35, Mseminari mmoja na waamini walei ni 4. Bara la Afrika, mapadre 19, Mseminari mmoja na mwamini mlei mmoja waliuwawa. Barani Amerika, wameuwawa mapadre 12 na waamini walei 3; Barani Asia, wameuwawa mapadre 3 na Bara la Ulaya, ameuwawa padre mmoja.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican

Shirika la Kipapa kwa ajili ya Makanisa Hitaji linasema kwamba, katika kipindi cha mwaka 2018 kuna Wamisionari 40 waliouwawa, wengi wao ni wale wanaojisadaka kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu katika nchi za kimisionari. Takwimu zinaonesha kwamba, Mapadre waliouwawa ni 35, Mseminari mmoja na waamini walei ni 4.  Bara la Afrika, mapadre 19, Mseminari mmoja na mwamini mlei mmoja waliuwawa. Barani Amerika, wameuwawa mapadre 12 na waamini walei 3; Barani Asia, wameuwawa mapadre 3 na Bara la Ulaya, ameuwawa padre mmoja.

Itakumbukwa kwamba, kwa mwaka 2017, Mapadre waliouwawa walikuwa ni 17. Hawa ni viongozi wa Kanisa waliouwawa kutokana na chuki ya imani na kwamba, zaidi ya wakristo elfu tatu waliuwawa kikatili kutokana na imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Hizi ni takwimu zilizotolewa na Shirika la Habari za Kimisionari, Fides, mwishoni mwa mwaka 2018 na kuonya kwamba, idadi ya wakristo wanaoendelea kuuwawa duniani inaongnezeka maradufu, kila kukicha! Kwa mwaka 2018, Bara la Afrika linaonekana kuongoza kwa mauaji ya mihimili ya uinjilishaji. Kuna mapadre 19, mseminari mmoja na mwamini mlei mmoja, waliuwawa kutokana na chuki za kidini.

Mwaka 2018 unakumbukwa kuwa ni mwaka wa hatari “annus horribilis” kutokana na mauaji ya kikatili dhidi ya mapadre. Kanisa Barani Afrika linamkubuka na kumwombea Padre John Njoroge Muhia ambaye hivi karibuni aliuwawa katika mazingira ya kutatanisha. Ndiyo maana Kardinali John Njue, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Nairobi, wakati wa Ibada ya mazihi ya Padre Njoroge alivitaka vyombo vya ulinzi na usalama kufanya uchunguzi wa kina, ili ukweli uweze kufahamika na wahusika kufikishwa kwenye vyombo vya sheria. Mapadre katika maisha na utume wao, kama watangazaji na mashuhuda wa Injili; wanaojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; viongozi ambao kimsingi ni sauti ya wanyonge, hata wao pia wanakabiliana na fumbo la kifo, kila siku ya maisha yao.

Sehemu kubwa ya mauaji yaliyofanyika ni katika harakati za kutaka kupora mali ya Kanisa kwa kisingizio cha umaskini na hali ngumu inayowakabili watu sehemu mbali mbali za dunia kutoka na rushwa, ufisadi pamoja na watu kukengeuka. Lakini, hizi ni sababu ambazo wakati mwingine zinafunika sababu msingi yaani mauaji ya wamisionari kutokana na chuki za kidini. Licha ya changamoto za maisha na hatari za kifo zinazowaandama mapadre, bado wanaendelea kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kama vyombo vya haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa.

Wamisionari Waliouwawa mwaka 2018
02 January 2019, 09:34