Maaskofu  Katoliki nchini Taiwan wakati wa hija yao ya kitume mjini Roma 2018 Maaskofu Katoliki nchini Taiwan wakati wa hija yao ya kitume mjini Roma 2018 

Taiwan:Kard Filoni ni mwakilishi Maalum wa Papa katika Kongamano la Ekaristi Kitaifa

Kardinali Ferdinando Filoni Rais wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu atakuwa mwakilishi Maalum wa Papa katika hitimisho la Kongamano la Ekaristi Takatifu nchini Taiwan tarehe 1 Machi 2019

Sr. Angela Rwezaula – Vatican

Baba Mtakatifu Francisko amemteua Kardinali Ferdinando Filoni, Rais wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu kuwa mwakilishi wake maalum katika kilele cha Maadhimisho ya kuhitimisha  Kongamano la IV la Ekaristi Takatifu Kitaifa nchini Taiwan. Kilele cha maadhimisho hayo kitafanyika huko Chiayi, tarehe 1 Machi 2019.

Mwezi Machi  2019  kunafanyika Kongamo la Ekaristi Takatifu kitaifa nchini Taiwan

Maaskofu wa Taiwan wakiwa katika hija yao ya kichungaji mjini Vatican kukutana na Baba Mtakatifu kwa  mwaka 2018 walimwalika aweze kwenda kutembelea nchi yao, japokuwa hakujibu ndiyo wala hapana, bali kwa tabasamu tu . Hayo ni maelezo kwa mujibu wa Askofu Mkuu John Hung Shan-chuan wa Jimbo kuu Katoliki la Taipei  akifafanua katika vyombo vya habari (ACI), mara baada ya mkutano wao ambao ulifanyika na uwakilishi wa jumuiya ndogo ya maaskofu wa Taiwan. Kwa mujibu wa Askofu Mkuu Shan- chuan, Maaskofu walijazwa na furaha kubwa kukutana na Baba Mtakatifu ambapo alithibitisha kuwa Papa alijionesha kuwa mtu mwenyenyekevu na mkarimu. Walikaa naye na kuruhusiwa kuzungumza  wazi na uhuru  wote kwa lolote walilokuwa wanataka kumwambia papa ambaye kwa karibu saa moja, aliweza kuwasikiliza.

Jambo pia moja na alilomweleza askofu Mkuu Shan- chuan Papa, ni kuhusu uwepo wa Kongamano la Ekaristi Takatifu la mwezi Machi 2019 na kama angeweza kuudhuria maadhimisho hayo. Hata hivyo pia alibanisha kuwa, hata Rais wa Taiwan Bwana Tsai Ing-wen alikuwa tayari amesha mtumia barua ya kawaida ya kumwalika  Baba Mtakatifu mwezi Septemba 2017, wakati alipokutana na Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la Maendeleo fungamani ya watu.  Kutokana na hili Askofu Mkuu Shan- chuan alithibitisha kuwa, jibu  la Baba Mtakatifu lilikuwa ni kutoa tabasamu tu, kwa maana hakujibu ndiyo wala hapana.

Ukaribu wa nchi ya Taiwan na Vatican ni mzuri

Hata hivyo Askofu Mkuu Shan – chuan aliweza kuelezea juu ya ukaribu wao uliopo kati ya Vatican na Kanisa la Taiwan  na kwamba mwaka 2017 wakati wa Kongamano la Kimataifa ya Utume wa Bahari kumekuwapo na uwakilishi kutoka Vatican  na tarehe 14 Machi 2018 walifika hata wawakilishi wa dhehebu ya Kitau kutoka Taiwan, ambao walimtembelea Baba Mtakatifu. Na tangu tarehe 13- 16 Novemba 2018 nchini Taiwan kulikuwa na Mkutano wa IV wa dini ya Wabudha na wakristo, iliyoandaliwa na Baraza la Kipapa la Mazungumzo ya Kidini,  kwa maana hiyo katika matukio mbalimbali ni kuonesha kuwa kuna  uhusiano wa nguvu sana kati ya Taiwan na Vatican.

Uhusiano wa Kanisa na serikali nchini Taiwan ni wa amani

Kadhalika Kanisa la Taiwan, liko wazi kwa ufunguzi wa semina mbalimbali na vitivo vya kitaalimungu kwa mamia ya mapadre wanaotoka nchini China na wengine baada ya miaka wanarudi nyumbani. Kwa maana hiyo Askofu Mkuu Shan – chuan alithibitisha kwa vyombo vya habari kuwa Kanisa la Taiwan ni picha inayowakilisha ulimwengu mzima, kwa sababu wanayo mashirika ya kitawa ya kike na kiume. Kwa pamoja wanashirikiana katika shughuli mbalimbali za utume na pia serikali haiwaingilii kati katika shughuli za ona kwa maana nyingine ni kuthibitisha kuwa uhusiano wao wote wa kidini ni wa amani.

05 January 2019, 12:05