Cerca

Vatican News
Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Vijana 2018: Tarehe 18-22 Juni 2019 Jukwaa la Vijana Kimataifa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Vijana 2018: Tarehe 18-22 Juni 2019 Jukwaa la Vijana Kimataifa  (Vatican Media)

Sinodi ya Maaskofu 2018: Jukwaa la Vijana Kimataifa, Juni 2019

Kuanzia tarehe 18-22 Juni 2019 kutafanyika Jukwaa la Vijana Kimataifa. Huu ni mwendelezo wa tafakari ya Sinodi ya Maaskofu ya Maaskofu kwa ajili ya Vijana kwa kumpatia nafasi Roho Mtakatifu kuendelea kuwatumia vijana katika maisha na utume wa Kanisa. Hii itakuwa ni fursa ya kufanya mang’amuzi ya kijumuiya, kwa kuendelea kujikita katika dhana ya Sinodi na ari ya kimisionari.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Hati ya Mababa wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Vijana kwa Mwaka 2018 imegawanyika katika sehemu kuu tatu ambazo  zimejikita katika mawazo ya Injili yanayowaonesha wale wafuasi wa Emau, waliokuwa wanaandamana na Yesu. Yakafunguliwa macho yao nao wakamtambua; Wakatoka kwa haraka kwenda kutangaza kwamba, Kristo Yesu aliyeteswa na kufa Msalabani, amefufuka. Hii ndiyo changamoto ambayo Mababa wa Sinodi wanayataka Makanisa mahalia kuimwilisha katika maisha na utume wa Kanisa miongoni mwa vijana, daima yakijitahidi kujenga na kuimarisha umoja na mafungamano na vijana, kwa kuandamana na kukaa na vijana, ili kuwasaidia kung’amua maisha yao.

Pili ni kutafsiri matukio mbali mbali katika mwanga wa Maandiko Matakatifu na; Tatu ni kufanya maamuzi magumu ambayo vijana watapaswa kuyatekeleza haraka, kwa kushirikishana mang’amuzi yao baada ya kukutana na Kristo Mfufuka kama ilivyokuwa kwa wanafunzi wa Emau. Ni katika mwanga wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana kwa mwaka 2018 sanjari na maadhimisho ya Siku ya XXXIV ya Duniani kwa mwaka 2019 huko Panama, Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha linatangaza kwamba, Mwezi Juni, 2019 kutafanyika Jukwaa la Vijana Kimataifa. Huu ni mwendelezo wa tafakari ya Sinodi ya Maaskofu iliyoongozwa na kauli mbiu “Vijana, Imani na Mang’amuzi ya miito”.

Baba Mtakatifu Francisko katika Katiba ya Kitume “Episcopalis communio” yaani “ Umoja wa Maaskofu katika Sinodi za Maaskofu, anakazia maadhimisho ya Sinodi kuwa ni chombo cha kukuza na kudumisha: majadiliano, umoja na ushirikiano kati ya urika wa Maaskofu na Khalifa wa Mtakatifu Petro; Sinodi kama chombo cha uinjilishaji unaojikita katika sanaa na utamaduni wa Kanisa kusikiliza kwa makini maoni ya familia ya Mungu. Kumbe, maadhimisho ya Sinodi yanapaswa kuwa na awamu ya kwanza ya maandalizi, kuadhimishwa na hatimaye, hitimisho lake ambalo ni muhtasari wa maazimio yanayopaswa kuidhinishwa na Kanisa mahalia, Mabaraza ya Maaskofu au Baraza la Kipapa lililokabidhiwa dhamana hii.

Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha linapenda kuyahamasisha Makanisa mahalia kuhakikisha kwamba, yanawahusisha vijana katika maisha na utume wa Kanisa, ili kuwajengea uwezo wa kupambana na changamoto mamboleo; kwa njia ya vyama na mashirika kwa ajili ya maisha na utume wa vijana kitaifa na kimataifa. Kilele cha ushirikishwaji wa vijana katika maisha na utume wa Kanisa ni Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani yanayopitia hatua mbali mbali za maandalizi na hatimaye maadhimisho yake. Kuanzia tarehe 18-22 Juni 2019 kutafanyika Jukwaa la Vijana Kimataifa. Huu ni mwendelezo wa tafakari ya Sinodi ya Maaskofu ya Maaskofu kwa ajili ya Vijana kwa kumpatia nafasi Roho Mtakatifu kuendelea kuwatumia vijana katika maisha na utume wa Kanisa.

Hii itakuwa ni fursa ya kufanya mang’amuzi ya kijumuiya, kwa kuendelea kujikita katika dhana ya Sinodi, ari na mwamko wa kimisionari katika maisha na utume wa Kanisa. Jukwaa hili litawashirikisha wajumbe kutoka Mabaraza ya Maaskofu Katoliki; vyama na mashirika makuu ya utume wa vijana kimataifa bila kuwasahau “vijana wa sinodi” kama walivyokuwa wanajulikana wakati wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu. Hii ni nafasi ya vijana kushirikisha uzoefu na mang’amuzi yao sanjari na kusikiliza ushauri kutoka kwa wataalamu wa sayansi ya maisha na utume wa vijana ndani na nje ya Kanisa. Itakuwa ni fursa ya kuweza kuchambua katika ngazi ya kimataifa jinsi ambavyo vijana sehemu mbali mbali ya dunia, wameweza kupokea Hati ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Vijana kwa mwaka 2018.

Hii itakuwa ni fursa ya kupitia tena Mapendekezo ya vijana kwa Mababa wa Sinodi ya vijana 2018 yaliyowekwa katika Hati ya Utangulizi wa Maadhimisho ya Sinodi ya Vijana ambayo yalikuwa ni sehemu ya mchakato wa mambo msingi ambayo Mama Kanisa anapaswa kuyazingatia ili hatimaye, kuangalia jinsi ambavyo atasaidia kuwaongoza, kuwainua na kuwaimarisha vijana katika maisha yao. Hati hii ni muhtasari wa changamoto za vijana kutoka katika mabara, dini na tamaduni mbali mbali duniani, inayoonesha mambo msingi yanayopaswa kuzingatiwa na Mama Kanisa. Mwishoni mwa maadhimisho ya Jukwaa hili, kutaundwa ofisi ya uwakilishi wa vijana kimataifa!

Jukwaa la Vijana Kimataifa
10 January 2019, 16:44