Cerca

Vatican News
Sherehe ya Tokeo la Bwana: Siku ya Utoto Mtakatifu: Lengo ni kukuza ari na mwamko wa kimisionari miongoni mwa watoto wadogo. Sherehe ya Tokeo la Bwana: Siku ya Utoto Mtakatifu: Lengo ni kukuza ari na mwamko wa kimisionari miongoni mwa watoto wadogo.  (Vatican Media)

Siku ya Utoto Mtakatifu: Malezi na ari ya kimisionari kwa watoto

Kama ilivyo kwa Wakristo wengine wote, hata watoto kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, wanashiriki: Ukuhani, Ufalme na Unabii wa Kristo Yesu, na hivyo, wanahamasishwa kumtangaza na kumshuhudia katika maisha na mazingira yao. Huu ndio mkazo unaotolewa pia katika Mpango Mkakati wa Mwezi Oktoba 2019 unaongozwa na kauli mbiu “Mmebatizwa na kutumwa”.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Katika Sherehe ya Epifania yaani Tokeo la Bwana, inayoadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 6 Januari, Mama Kanisa pia anaadhimisha Siku ya Utoto Mtakatifu, iliyoanzishwa na Papa Pius XII, kunako mwaka 1950, aliyetaka waamini kutoa kipaumbele cha kwanza kwa malezi ya watoto wao kama Kristo Yesu, alivyowapatia nafasi ya pekee, katika maisha na utume wake. Watoto wanapaswa kujifunza na hatimaye, kujenga utamaduni wa: umoja, upendo na mshikamano, kwa kujaliana, kusaidiana na kusali pamoja; mambo msingi katika malezi na makuzi yao kwa sasa na kwa siku za usoni!

Hii ni changamoto na mwaliko kwa wazazi na walezi kuwajengea watoto wao ari na moyo wa kimissionari tangu sasa, ili kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa watoto wenzao sehemu mbali mbali za dunia. Hawa ni watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi, watoto yatima; watoto wanaokumbana na magonjwa, njaa, ujinga na baa la umaskini. Hata katika umaskini wao, watoto wanaweza kuchangia ustawi na maendeleo ya watoto wenzao sehemu mbali mbali za dunia! Huu ndio mshikamano wa watoto katika huduma ya Injili ya upendo!

Huu ni mwaliko unaotolewa na Sr. Roberta Tremarelli, Katibu mkuu wa Shirika la Kipapa la Utoto Mtakatifu, katika maadhimisho ya Siku ya Utoto Mtakatifu sanjari na Sherehe ya Tokeo la Bwana. Anasema, kama ilivyo kwa Wakristo wengine wote, hata watoto kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, wanashiriki: Ukuhani, Ufalme na Unabii wa Kristo Yesu, na hivyo, wanahamasishwa kumtangaza na kumshuhudia katika maisha na mazingira yao. Huu ndio mkazo unaotolewa pia na Mama Kanisa kama sehemu muhimu ya utekelezaji wa  Mpango Mkakati wa Mwezi Oktoba 2019 unaongozwa na kauli mbiu “Mmebatizwa na kutumwa”.

Kanisa linaendeleza wito na utume wake wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia, agizo kutoka kwa Kristo mwenyewe kwa wafuasi wake. Hiki ni kipindi maalum sana kwa maisha na utume wa Kanisa sehemu mbali mbali za dunia. Huu ni muda wa kutangaza furaha ya Injili kwa watu wa Mataifa; Kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa kwa ari na ushiriki mkamilifu na hatimaye, Kushuhudia imani inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili.

Sr. Roberta Tremarelli anakaza kusema, hata watoto nao wanapaswa kufuata nyayo za Mamajusi kutoka Mashariki walioongozwa na nyota kwenda kumtafuta Kristo Mfalme aliyezaliwa mjini Bethlhememu, walipomwona, wakamsujudia na kumpatia zawadi. Na kama ilivyokuwa kwa wachungaji kule kondeni, wakatoka kwenda kutangaza matendo makuu ya Mungu katika maisha ya mwanadamu!  Mshikamano wa upendo, umewawezesha watoto kutoka sehemu mbali mbali za dunia kuguswa na mahangaiko ya watoto wenzao kiasi cha kujinyima na kuchangia kwa ajili ya ustawi na maendeleo yao!

Sr. Roberta Tremarelli anasikitika kusema, leo hii, haki msingi za watoto sehemu mbali mbali za dunia zinaendelea kuvunjwa, kiasi kwamba, watoto wananyanyaswa na kudhulumiwa; wanapokwa haki yao ya utoto kwa kufanyishwa kazi za suluba; kwa kusumbuliwa na: umaskini, magonjwa, ujinga, baa la njaa na utapiamlo wa kutisha; kwa vita na majanga mbali mbali yanayoendelea kumwandama mwanadamu! Watoto hata katika changamoto zote hizi, bado wanaweza kusaidiwa kukuza na kudumisha ari na moyo wa kimissionari, kwa kujenga utamaduni wa upendo na mshikamano. Kwa njia hii watoto wamesaidia kulinda Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo kwa kuwapatia watoto wenzao mahitaji msingi kama vile: chakula, elimu, makazi na huduma bora ya afya. Shirika la Utoto Mtakatifu lililoanzishwa kunako mwaka 1843 na Askofu Toussaint de Forbin Janson wa Jimbo Katoliki la Nancy lililoko nchini Ufaransa.

Mwaka 2019, Shirika la Utoto Mtakatifu linaadhimisha kumbu kumbu ya miaka 176 tangu kuanzishwa kwake. Makanisa mahalia sehemu mbali mbali za dunia wamewakabidhi wanawake wakatoliki kuwa ni wasimamizi na walezi wa Shirika la Utoto Mtakatifu, dhamana na wajibu wanaopaswa kuutekeleza kwa ari na moyo mkuu, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa malezi na makuzi ya watoto kimisionari!

Utoto Mtakatifu

 

07 January 2019, 08:14