Tafuta

Vatican News
SEDAC Amerika ya Kati ni chombo na jukwaa la maisha na utume wa Makanisa mahalia! SEDAC Amerika ya Kati ni chombo na jukwaa la maisha na utume wa Makanisa mahalia! 

SEDAC Amerika ya Kati: Chombo na jukwaa la utume wa Kanisa!

SEDAC iko tayari kupokea ujumbe wa Baba Mtakatifu kama chachu na mwanga wa matumaini katika safari yao ya shughuli za kichungaji katika kipindi hiki kigumu cha historia ambacho kinatawaliwa kwa kiasi kikubwa na vita, rushwa na ufisadi; uksoefu wa haki na usawa kati ya watu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Askofu mkuu José Luis Escobar Alas, Rais wa Sekretarieti ya Mabaraza ya Maaskofu Katoliki, Amerika ya Kati, SEDAC, katika hotuba yake, amemkaribisha Baba Mtakatifu Francisko huko Amerika ya Kati, chimbuko la watakatifu wengi ndani ya Kanisa. Hawa ni waaamini waliojisadaka na kuyamimina maisha yao kwa ajili ya imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. SEDAC inampongeza Baba Mtakatifu kwa kuipatia heshima ya kuweza kuadhimisha Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani nchini Panama.

SEDAC imetumia fursa hii kuonesha kwa mara nyingine tena imani, utii, mshikamano pamoja na kuunga mkono utekelezaji wa kazi ya Mungu kwa Kanisa na ulimwengu katika ujumla wake! SEDAC iko tayari kupokea ujumbe wa Baba Mtakatifu kama chachu na mwanga wa matumaini katika safari yao ya shughuli za kichungaji katika kipindi hiki kigumu cha historia ambacho kinatawaliwa kwa kiasi kikubwa na vita, rushwa na ufisadi; ukosefu wa haki na usawa kati ya watu.

SEDAC imegusia pia wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji; maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Dhamana na wajibu wa viongozi wa Kanisa ni kuhakikisha kwamba, wanajitosa kimasomaso kwa kusimama kidete: kuwalinda, kuwasindikiza na kuwasaidia kwa kuiga mfano wa huduma kama ulivyoshuhudiwa na Mtakatifu Oscar Arnulfo Romero Galdamez. SEDAC imechukua fursa hii kumshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kumtangaza Askofu mkuu Oscar Romero kuwa Mtakatifu.

Sekretarieti SADAC
25 January 2019, 14:19