Tafuta

Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani 2019: Panama imegeuka kuwa ni Madhabahu ya Sala, Neno la Mungu na Majiundo makini ya vijana! Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani 2019: Panama imegeuka kuwa ni Madhabahu ya Sala, Neno la Mungu na Majiundo makini ya vijana! 

PANAMA: Madhabahu ya Sala na Neno la Mungu kwa vijana!

Panama imegeuka kuwa ni Hekalu la sala na tafakari ya Neno la Mungu; mahali pa kukuza na kudumisha tunu msingi za maisha ya Kikristo na Kiutu; ni muda wa kushuhudia na kumwilisha Injili ya upendo na mshikamano wa dhati miongoni mwa vijana wa kizazi kipya. Ni wakati muafaka wa kujifunza kutoka katika shule ya Bikira Maria, tayari kujisadaka katika huduma ya upendo kwa maskini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Askofu mkuu Josè Domingo Ulloa Mendieta wa Jimbo kuu la Panama, Mwenyeji wa maadhimisho ya Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2019 anasema, kwa sasa Panama imegeuka kuwa ni Hekalu la sala na tafakari ya Neno la Mungu; mahali pa kukuza na kudumisha tunu msingi za maisha ya Kikristo na Kiutu; ni muda wa kushuhudia na kumwilisha Injili ya upendo na mshikamano wa dhati miongoni mwa vijana wa kizazi kipya. Ni wakati muafaka wa kujifunza kutoka katika shule ya Bikira Maria, tayari kujisadaka katika huduma ya upendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Baraza la Maaskofu Katoliki Panama linamshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kulipatia nafasi ya kugeuza Panama, kuwa ni makao makuu ya vijana wa kizazi kipya kuanzia tarehe 22-27 Januari 2019. Kwa njia ya Ibada kwa Bikira Maria, vijana wamepyaisha tena imani, matumaini na mapendo kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Hawa ni wale vijana ambao wamesiginwa sana na umaskini wa maisha ya kiroho na kimwili; ni vijana ambao wamekuwa wakitangaza tanga kama wakimbizi na wahamiaji ili kutafuta: hifadhi, usalama na maisha bora zaidi ughaibuni.

Uwepo wa Baba Mtakatifu Francisko ni ushuhuda wenye mvuto na mashiko, kwani anataka kuwajenga na kuwaimarisha katika imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Kwa hakika anasema Askofu mkuu Josè Domingo Ulloa Mendieta kutakuwepo na mabadiliko makubwa baada ya maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani. Huu ni muda muafaka wa uinjilishaji wa kina unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Ni wakati wa kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili miongoni mwa vijana wa kizazi kipya.

Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani, yawe ni chachu kwa vijana kujitoa na kujisadaka kwa ajili ya huduma ya uinjilishaji kwa vijana wenzao wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi; wawe ni vyombo vya Injili ya faraja kwa wale wote waliokata tamaa katika maisha. Huu ni wakati kwa vijana kuhakikisha kwamba, wanatumia vyema mitandao ya kijamii kufikisha ujumbe wa Baba Mtakatifu sehemu mbali mbali za dunia, lakini kwanza, kwa kujenga mahusiano na mafungamano ya dhati na Mwenyezi Mungu, Kristo, Kanisa na vijana wenzao.

Vijana wako tayari kusikiliza ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko, ili waweze kutoka kimasomaso kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili. Kanisa linataka kutoka kifua mbele kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu sanjari na kukita mizizi yake katika mambo msingi ya maisha na utume wa Kanisa. Kanisa linataka kutangaza na kushuhudua huruma na upendo wa Mungu kwa watu wa Mataifa, kwa kuwashirikisha vijana katika maisha na utume wake!

Panama Mji Mkuu wa Vijana 2019
23 January 2019, 10:19