Cerca

Vatican News
Kardinali Parolin: Vijana ni jeuri na amana katika maisha na utume wa Kanisa! Kardinali Parolin: Vijana ni jeuri na amana katika maisha na utume wa Kanisa! 

Siku ya Vijana Duniani: Vijana ni jeuri na rasilimali ya Kanisa!

Lengo ni kujenga na kudumisha sanaa na utamaduni wa kukutana, kujadiliana, kusikilizana, kusindikizana na hatimaye, kufanya mang’amuzi yatakayotekelezwa katika maisha na utume wa Kanisa mintarafu sera na mikakati ya shughuli za kichungaji. Siku ya Vijana Duniani ni fursa inayojikita katika ushuhuda, uzoefu, mang’amuzi sanjari na ujenzi wa ujirani mwema kati ya vijana na Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani huko Panama kuanzia tarehe 22 - 27 Januari 2019 yanaongozwa na kauli mbiu “Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; iwe kwangu kama ulivyosema”. Lk. 1:38. Baba Mtakatifu Francisko anawahamasisha vijana kutoa ushuhuda wa tamaduni za Makanisa yao mahalia wakati wa maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani, kwani lengo ni kuhakikisha kwamba, Kanisa linasimama kidete kulinda na kudumisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kanisa linataka kujielekeza katika mchakato wa ujenzi wa ulimwengu unaosimikwa katika misingi ya umoja, usawa, udugu na mshikamano wa kweli!

Baba Mtakatifu Francisko, kwa mara ya tatu sasa anashiriki katika maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani, changamoto kwa Kanisa ni kuendelea kuwahamasisha vijana kutembea kwa pamoja na Kristo Yesu, kama ilivyokuwa kwa wafuasi wa Emau. Lengo ni kujenga na kudumisha sanaa na utamaduni wa kukutana, kujadiliana, kusikilizana, kusindikizana na hatimaye, kufanya mang’amuzi yatakayotekelezwa katika maisha na utume wa Kanisa mintarafu sera na mikakati ya shughuli za kichungaji. Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani ni fursa inayojikita katika ushuhuda, uzoefu, mang’amuzi sanjari na ujenzi wa ujirani mwema kati ya vijana na Kanisa katika ujumla wake.

Huu ni mwendelezo wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana kwa mwaka 2018, mwaliko wa kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili kwa watu wa Mataifa. Katika mahojiano maalum na Vatican News, Kardinali Pietro Parolin, katibu mkuu wa Vatican anasema, vijana ni amana na utajiri wa Kanisa. Ni kundi linalopaswa kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa. Ndiyo maana Hati ya Mababa wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana imejikita katika mawazo ya Injili yanayowaonesha wale wafuasi wa Emau, waliokuwa wanaandamana na Yesu; Yakafunguliwa macho yao nao wakamtambua; Wakatoka kwa haraka kwenda kutangaza kwamba, Kristo Yesu aliyeteswa na kufa Msalabani, amefufuka kwa wafu!

Hii ndiyo changamoto inayopaswa kumwilishwa katika maisha na utume wa Makanisa mahalia;  kwa kujenga na kuimarisha umoja na mafungamano na vijana; kwa kuandamana na kukaa na vijana, ili kuwasaidia kung’amua maisha yao; kutafsiri matukio mbali mbali katika mwanga wa Injili na hatimaye, kufanya maamuzi magumu ambayo watapaswa kuyatekeleza haraka, kwa kushirikishana mang’amuzi yao baada ya kukutana na Kristo Mfufuka kama ilivyokuwa kwa wafuasi wa Emau.

Kardinali Parolin anakaza kusema, kwa ufupi sana, Mababa wa Sinodi wamekazia umuhimu wa sanaa na utamaduni wa kusikiliza sanjari na kuwasindikiza vijana, ili waweze kukutana katika hija ya maisha yao na Kristo Mfufuka anayetaka kupyaisha maisha na utume wao hapa duniani. Vijana ni chachu ya mabadiliko kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria, wanapaswa kukubali na kushiriki kikamilifu katika mpango wa Mungu! Bikira Maria ni kielelezo makini cha usikivu na utekelezaji wa mapenzi ya Mungu katika maisha yake. Vijana nao kwa nguvu ya Roho Mtakatifu inayotenda kazi ndani mwao, wanaweza kuleta mabadiliko makubwa katika ulimwengu mamboleo! Lakini si kwa vita, fujo na vurugu, bali kwa kutekeleza mpango wa Mungu kila siku ya maisha yao! Vijana wawe tayari kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa Mungu na jirani zao, kama alivyofanya Bikira Maria, kwa kukubali kuwa ni Mama wa Mungu na Kanisa.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, katika ulimwengu wa utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine, waathirika wakuu ni vijana na hasa zaidi vijana wazawa. Kumbe, vijana wanapaswa kuwa na utambuzi makini kwamba, wao ni sehemu ya watu wao, mwaliko ni kusimama kidete kupinga utamaduni usiojali wala kuthamini utu na heshima ya wengine. Vijana wathubutu kuzamisha mizizi ya tamaduni zao katika maisha, huku wakiwa na matumaini kwa maisha ya mbeleni yenye msingi thabiti!

Kardinali Parolin anakaza kusema, vijana wapende na kuheshimu mila, desturi na tamaduni zao njema, ili waweze kukua, kukomaa na kuchanua katika utakatifu wa maisha! Umefika wakati wa kujikita zaidi katika mchakato wa utamadunisho, kwa kuwajengea wazawa uwezo wa kushirikisha karama, mila, desturi na tamaduni zao njema sehemu ya utajiri wa maisha na utume wa Kanisa. Vijana wadumishe umoja na mshikamano, tayari kupambana na changamoto za maisha ya ujana!

Amerika ya Kusini ni kati ya maeneo ambayo yanakabiliwa na hali ngumu ya kiuchumi, kisiasa na kijamii. Kuna wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji; vita na kinzani za kijamii. Hapa ni chimbuko la biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya mambo yanayosigina utu, heshima na haki msingi za binadamu! Kumbe, uwepo wa Baba Mtakatifu Francisko unapania kuwajengea imani, matumaini na mapendo, tayari kupyaisha maisha na wito wao kwa mwanga wa Injili; kwa kuheshimu na kuthamini utu na haki msingi za binadamu. “Vijana kamwe wasikate tamaa wala kukubali kupigishwa magoti na furaha za mpito” bali wasimame kidete kupambana na changamoto za maisha, ili kuwa na matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake wa Siku ya Kuombea Amani Duniani kwa mwaka 2019, anakazia: Injili ya amani kama sehemu ya utume wa Kanisa; Changamoto za siasa safi; Upendo na fadhila za kiutu kwa ajili ya siasa inayohudumia haki msingi na amani; vilema vya wanasiasa; umuhimu wa siasa safi inayowashirikisha vijana na kujengeana imani; pamoja na kukataa kishawishi cha vita na mbinu mkakati wa vitisho, kwa kuwekeza katika mradi mkubwa wa amani. Katika muktadha huu, vijana wanapaswa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa uinjilishaji miongoni mwa vijana wenzao.

Kardinali Parolin anasema, hili liwe ni lengo madhubuti kwa vijana sehemu mbali mbali za dunia. Wajitahidi kuinjilisha kwa njia ya ushuhuda wa maisha unaopenyeza mizizi yake na kujikita katika tamaduni, mila na desturi za vijana wenzao. Vijana wakifikia hatua hii, kwa hakika, lengo la maadhimisho ya Siku za Vijana Duniani, litakuwa limepiga hatua kubwa zaidi! Yaani hadi Kanisa linapata furaha ya kuinjilisha vijana wa kizazi kipya!

Kardinali Parolin: Panama 2019
22 January 2019, 10:10