Tafuta

Vatican News
Kardinali Kevin Joseph Farrell,anasema vijana wanataka kujadiliana na kusikilizwa! Kardinali Kevin Joseph Farrell,anasema vijana wanataka kujadiliana na kusikilizwa! 

Panama 2019: Vijana wanataka kujadiliana na kusikilizwa!

Hadi sasa takwimu zinaonesha kwamba, vijana waliojiandikisha rasmi ni 500, 000 kutoka katika nchi 135. Idadi ya watu wa kujitolea katika huduma ni 30, 000; Makardinali na Maaskofu ni 400, Mapadre ni 2, 000. Gharama ya maandalizi yote haya ni dola milioni 54 za Kimarekani. Maadhimisho yanatarajia kuingiza kiasi cha dola milioni 250 pamoja na kuongeza idadi ya watalii nchini humo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani, ni fursa kwa Mama Kanisa kukuza na kudumisha utume wake miongoni mwa vijana wa kizazi kipya: kwa kujenga sanaa na utamaduni wa: kuwasikiliza, kuwasindikiza na kuwasaidia kufanya maamuzi magumu katika maisha yao kadiri ya mwanga wa Injili ya Kristo na Mafundisho Jamii ya Kanisa. Kwa mwaka huu 2019, mkazo wa pekee ni kwa ajili ya vijana kutoka Amerika ya Kusini, wanaokabiliana na changamoto mbali mbali katika maisha na utume wao. Nchi nyingi Amerika ya Kusini kwa sasa zinakabiliana na hali ngumu ya maisha: kisiasa, kiuchumi na hata kijamii.

Vijana wanataka kuanza kuandika ukurasa mpya wa maisha na utume wao ndani ya jamii na wanataka wapewe rasilimali na mtaji wa mambo msingi, tayari kuchangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Vijana wanataka kulindwa na kutunzwa; kueleweka na kupendwa! Vijana wengi kutoka Amerika ya Kusini ni watu wenye ujasiri na uwezo wa kujifunza kikamilifu na kuzama katika tunu msingi za maisha ya imani, kwa kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu asili ya wema na utakatifu wote!

Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani ni nafasi ya kusikiliza kwa makini ujumbe wa Neno la Mungu, tayari kuumwilisha katika uhalisia wa maisha na vipaumbele vya watu. Hapa kuna haja ya kuheshimiana, kuthaminiana na kusaidiana kama binadamu, kwa kufyekelea mbali ubinafsi na uchoyo. Hata vijana kutoka katika nchi maskini zaidi duniani wanashiriki kwani wamewezeshwa na mfuko wa mshikamano kwani hili ni tukio muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa.

Kardinali Kevin Joseph Farrell, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha anafafanua kwa kina na mapana kuhusu maadhimisho ya Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2019 huko Panama ambayo yanaongozwa na kauli mbiu “Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; iwe kwangu kama ulivyosema”. Lk. 1:38. Tayari makundi makubwa ya vijana yamewasili na idadi hii inatarajiwa kuongezeka maradufu hasa wakati wa matukio makubwa ya “Njia ya Msalaba, Mkesha na Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kufunga maadhimisho haya”.

Hadi sasa takwimu zinaonesha kwamba, vijana waliojiandikisha rasmi ni 500, 000 kutoka katika nchi 135. Idadi ya watu wa kujitolea katika huduma ni 30, 000; Makardinali na Maaskofu ni 400, Mapadre ni 2, 000. Gharama ya maandalizi yote haya ni dola milioni 54 za Kimarekani. Maadhimisho yanatarajia kuingiza kiasi cha dola milioni 250 pamoja na kuongeza idadi ya watalii nchini Panama. Idadi hii inatarajiwa kuongezeka maradufu wakati wowote. Hadi sasa kundi kubwa la wawakilishi ni kutoka Poland na takwimu zinaonesha kwamba, hata wawakilishi kutoka Bara la Afrika wamo, “ingawa hawavumi sana. Angola inawakilishwa na vijana 200, Msumbiji vijana 40 na Cape Verde ni vijana 30 kwa zile takwimu tulizonazo kwa sasa. Vijana kutoka Amerika ya Kusini wamejisadaka ili kuhudhuria tukio hili, ingawa wanakabiliwa na hali tete katika nchi zao.

Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka huu 2019 ni sehemu ya mchakato wa maisha na utume wa Kanisa. Ni mwendelezo wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Vijana iliyohitimishwa mwaka 2018 na baadaye Mwezi Oktoba 2019 kutaadhimishwa Sinodiya Maaskofu Ukanda wa Amazonia. Lengo la Sinodi hii ni kuibua mbinu mkakati wa shughuli za kichungaji zitakazokidhi mahitaji ya uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili; utamadunisho kwa kuhakikisha kwamba, tunu msingi za kiinjili zinamwilishwa katika tamaduni, mila na desturi za watu wa Amazonia pamoja na kuzisafisha zile zinazosigana na kupingana na Habari Njema ya Wokovu! Ni Sinodi itakayojikita katika mchakato wa kukuza na kudumisha haki msingi za binadamu kama njia ya kuenzi utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Kardinali Farrell, anaendelea kufafanua kwamba, maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani yametanguliwa na semina kuhusu utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote pamoja na maadhimisho ya Siku ya Vijana Wazawa Amerika ya Kusini.Papa Francisko katika ujumbe wake, anawahamasisha Vijana kutoa shuhuda za tamaduni za Makanisa yao mahalia wakati wa maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani, kwani lengo ni kuhakikisha kwamba, Kanisa linasimama kidete kulinda na kudumisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, daima Kanisa nikijielekeza katika mchakato wa ujenzi wa ulimwengu unaosimikwa katika usawa na utu.

Vijana wametafakari yote haya, ili kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani, usawa, udugu, mshikamano na utulivu kama nyenzo msingi na vikolezo vya maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu. Katika mambo yote haya, vijana wanahamasishwa na Baba Mtakatifu kukimbilia daima ulinzi na tunza ya Bikira Maria katika maisha yao. Mtakatifu Yohane Paulo II, muasisi wa maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani ameliachia Kanisa urithi mkubwa katika maisha na utume wake. Vijana wanahamasishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, wanachangia kwa hali na mali katika mchakato wa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, kama sehemu ya mabadiliko katika ulimwengu mamboleo.

Kardinali Kevin Joseph Farrell, anakaza kusema, kuanzia tarehe 18-22 Juni 2019 kutafanyika Jukwaa la Vijana Kimataifa. Huu ni mwendelezo wa tafakari ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Vijana kwa kumpatia nafasi Roho Mtakatifu kuendelea kuwatumia vijana katika maisha na utume wa Kanisa. Hii itakuwa ni fursa ya kufanya mang’amuzi ya kijumuiya, kwa kuendelea kujikita katika dhana ya Sinodi na ari ya kimisionari. Viongozi wa Kanisa wanaweza kutoa mwongozo wa kanuni maadili na utu wema, lakini pia wanapaswa kujenga na kudumisha sanaa na utamaduni wa kuwasikiliza vijana, changamoto pevu inayotolewa na Baba Mtakatifu Francisko.

Dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa ndio mtindo unaopewa kipaumbele cha pekee na Baba Mtakatifu: kutoka katika maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Vijana, hadi Panama kwa Siku ya Vijana Duniani na hatimaye, Sinodi kwa ajili ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia! Huu ni mwaliko wa ujasiri unaopaswa kuvaliwa njuga katika maisha na utume wa Kanisa!

Siku ya Vijana Duniani 2019
23 January 2019, 09:45