Cerca

Vatican News
Siku ya Vijana Duniani 2019: Ilani ya Vijana kwa Viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa. Siku ya Vijana Duniani 2019: Ilani ya Vijana kwa Viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa. 

Panama: Ilani ya Vijana kwa Viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa

Vijana wanaoshiriki katika maadhimisho ya Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani kwa mwaka 2019 huko Panama, katika Ilani ya Siku ya Maadhimisho ya Vijana Duniani, wanawaomba viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kuzingatia mambo makuu matano kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi!Mazingira, Usalama wa wahamiaji, maji safi na salama; sera za uchumi shirikishi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia, wanaoshiriki katika maadhimisho ya Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani kwa mwaka 2019 huko Panama, katika Ilani ya Siku ya Maadhimisho ya Vijana Duniani, wanawaomba viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kuzingatia mambo makuu matano kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi! Mambo haya ni. Mosi, umuhimu wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Vijana wanataka Jumuiya ya Kimataifa kutekeleza kwa dhati kabisa maazimio ya Mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabia nchi COP24, uliofanyika huko Katowice, nchini Poland ili kupunguza hewa ya ukaa na ongezeko la joto duniani linalohitishia maisha, usalama, ustawi na maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu!

Jambo la pili ni “Mkataba wa Kimataifa wa Usalama wa Wahamiaji 2018” “Global Compact 2018”, unaolenga kuratibu na kuboresha mchakato wa wahamiaji na wakimbizi duniani, ili kulinda na kudumisha haki msingi, utu na heshima yao. Unakazia umuhimu wa jamii kusikiliza na kujibu kilio cha wakimbizi na wahamiaji duniani; kwa kukusanya maoni; kwa kupunguza gharama za kuwahudumia wahamiaji, kudumisha usalama na kuendeleza mchakato wa maboresho ya maisha yao. Mkataba huu unapania pamoja na mambo mengine: kuboresha ulinzi na usalama; haki msingi za binadamu pamoja na kupatiwa huduma ya msaada wa kisheria pale haki zao zinapovunjwa.

Jambo la tatu ni upatikanaji wa maji safi na salama ifikapo mwaka 2030. Maji ni sehemu ya haki msingi za binadamu na inaendelea kuwa ni changamoto kubwa kwa Jumuiya ya Kimataifa. Ikiwa kama suala zima la maji halitashughulikiwa kikamilifu, kwa siku za usoni, linaweza kuwa ni chanzo kikuu cha kinzani na migogoro ya kimataifa. Maji safi na salama ni muhimu sana katika mchakato mzima wa maboresho ya afya ya binadamu, ustawi na maendeleo yake.Maji yanaendelea kuwa ni sehemu muhimu ya agenda za Jumuiya ya Kimataifa hasa katika masuala ya kiuchumi, kisiasa na kijamii. Lakini, maji yanapaswa kutambulika kwanza kabisa kuwa ni sehemu ya haki msingi za binadamu na kamwe isigeuzwe kuwa biashara inayoweza kumilikiwa na kuendeshwa na makampuni binafsi.

Jambo la nne ni utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Athari za mabadiliko ya tabianchi ni kazi ya mikono ya wanadamu, kumbe, kuna haja ya kutunza vyanzo vya maji, ili kupata maji safi na salama kwa ajili ya afya bora; watu wajifunze kuhifadhi taka, ili kuepuka na uchafuzi mkubwa wa mazingira ambao ni chanzo kikuu cha umaskini, magonjwa na baa la njaa duniani.

Jambo la tano ni sera na mfumo wa uchumi shirikishi. Vijana wanakaza kusema,  Maendeleo endelevu na fungamani yazingatie kanuni maadili, utu na heshima ya binadamu, ili kutokomeza umaskini wa kupindukia; kukuza na kuimarisha uchumi unaofumbatwa katika: haki na usawa. Uchumi shirikishi unapania kukabiliana na changamoto za biashara na maendeleo ya mahusiano ya fedha na teknolojia kimataifa. Ufanisi wa mambo yote haya unajikita katika toba na wongofu wa kiekolojia kwa kujikita katika elimu na malezi endelevu katika ngazi mbali mbali za maisha ya binadamu!

Vijana wanapaswa kukuza na kudumisha mwelekeo wa kiekolojia mintarafu imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, ili hatimaye, kusherehekea kazi ya uumbaji na ukombozi. Vijana wanapaswa pia kuwa na wongofu wa ulaji ili kuondokana na ulaji wa kupindukia ambao kwa sasa umekuwa ni sehemu ya magonjwa yanayomwandama mwanadamu. Sera na mikakati ya maendeleo fungamani ielekezwe zaidi katika maendeleo ya teknolojia rafiki kwa mazingira, pamoja na kulinda haki msingi za wananchi mahalia!

Panama: Ilani ya Vijana 2019
24 January 2019, 13:47