Papa Francisko, Jumatatu tarehe 21 Januari 2019 amekutana na kuzungumza na Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed Ali Papa Francisko, Jumatatu tarehe 21 Januari 2019 amekutana na kuzungumza na Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed Ali 

Papa akutana na Waziri mkuu wa Ethiopia Bw. Abiy Ahmed Ali

Baba Mtakatifu amepongeza juhudi zinazoendelea kutekelezwa na Serikali ya Bwana Abiy Ahmed Ali katika kukuza na kudumisha mchakato wa upatanisho wa kitaifa, ustawi na maendeleo fungamani ya watu wa Mungu nchini Ethiopia. Katika muktadha huu, viongozi hawa wamegusia pia mchango wa Ukristo katika historia ya Ethiopia pamoja na kuzipongeza taasisi za Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu jioni, tarehe 21 Januari 2019, amekutana na kuzungumza na Bwana Abiy Ahmed Ali, Waziri Mkuu wa Ethiopia, ambaye baadaye alipata nafasi ya kukutana na kuzungumza pia na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa ameandamana na Monsinyo Antoine Camilleri, Katibu mkuu Msaidizi wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican.

Katika mazungumzo baina ya viongozi hawa wawili, wamekazia umuhimu wa uhusiano mzuri wa kidiplomasia uliopo kati ya Vatican na Ethiopia. Baba Mtakatifu amepongeza juhudi zinazoendelea kutekelezwa na Serikali ya Bwana Abiy Ahmed Ali katika kukuza na kudumisha mchakato wa upatanisho wa kitaifa, ustawi na maendeleo fungamani ya watu wa Mungu nchini Ethiopia. Katika muktadha huu, viongozi hawa wamegusia pia mchango wa Ukristo katika historia ya Ethiopia pamoja na kuzipongeza taasisi za Kanisa Katoliki katika kuchangia ustawi na maendeleo ya wananchi wa Ethiopia hususan katika sekta ya elimu na afya.

Baba Mtakatifu na mgeni wake, katika mazungumzo yao, wamejikita pia katika hali ya ukanda wa Afrika na kwa namna ya pekee, umuhimu wa nchi za Kiafrika kutafuta suluhu ya amani katika vita, migogoro na kinzani zinaendelea kulimeng’enyua Bara la Afrika na kwamba, kipaumbele kwa sasa kiwe ni kwa ajili ya maendeleo endelevu na fungamani: kisiasa na kiuchumi Barani Afrika. Baba Mtakatifu ameipongeza Ethiopia katika jitihada zake za kuleta amani na upatanisho kwenye Nchi za Pembe ya Afrika, hasa baada ya Ethiopia na Eritrea kutiliana sahihi mkataba wa amani!

Ziara ya Waziri Mkuu wa Ethiopia mjini Vatican imekuwa na umuhimu wa pekee sana, baada ya miaka ishirini ya vita ya wenyewe kwa wenyewe ambayo imesababisha maafa na majanga makubwa kwa maisha ya watu na mali zao, tarehe 18 Septemba 2018, Ethiopia na Eritrea vitaliana sahihi mkataba wa amani, tukio ambalo hivi karibuni, Baba Mtakatifu Francisko amelikumbuka kwa heshika kubwa, katika hotuba yake kwa mabalozi na wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa mjini Vatican.

Baba Mtakatifu anaendelea kuwahimiza watu wa Mungu nchini Ethiopia na Eritrea kujikita katika mchakato wa haki, amani na maridhiano, kama cheche za matumaini mapya kwa Nchi za Pembe ya Afrika na Afrika katika ujumla wake. Kunako mwaka 2014, wakati wa hija ya kitume ya Maaskofu wa Ethiopia na Eritrea, Baba Mtakatifu Francisko aliwahimiza kuwekeza katika miradi ya kijamii na kiuchumi ili kupambana na umaskini wa hali na kipato. Kwani eneo hili limekuwa linakumbukwa na ukame pamoja na baa la njaa, hali ambayo inanyanyasa na kusigina utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Injili ya huduma ya upendo, iwe ni faraja kwa familia ya Mungu katika eneo la Pembe ya Afrika. Ukosefu wa fursa za ajira, wimbi kubwa la watoto yatima waliowapoteza wazazi wao kutokana na vita, njaa na umaskini wamekuwa daima mbele ya macho ya Baba Mtakatifu Francisko anaikumbuka familia ya Mungu iliyoko kwenye Pembe ya Afrika. Vita, umaskini na hali ngumu ya maisha ni kati ya changamoto zinazopelekea vijana wengi kuthubutu kuhatarisha maisha yao jangwani na kwenye Bahari ya Mediterrania, ili kutafuta, usalama, hifadhi na maisha bora zaidi. Lakini, kwa bahati mbaya, leo hii, Bahari ya Mediterrania imegeuka kuwa ni kaburi la maisha na matumaini ya watu wengi kutoka Afrika! Katika mazingira kama haya, Kanisa nchini Ethiopia linapaswa kuwa ni chombo cha haki, amani na maridhiano kati ya watu!

Papa: waziri Mkuu wa Ethiopia
22 January 2019, 09:06