Cerca

Vatican News
Nembo ya Siku ya Umisionari wa Utoto Mtakatifu 2019 Nembo ya Siku ya Umisionari wa Utoto Mtakatifu 2019 

Papa:Epifania pia ni Siku ya utoto Mtakatifu wa kujipyaisha matendo ya umisionari!

Tarehe 6 Januari 2019, Baba Mtakatifu anakumbusha Sikukuu ya Tokeo la Bwana kwamba, pia ni Siku ya Utoto Mtakatifu. Amesema hayo mara baada ya tafakari ya Sala ya Malaika wa Bwana. Tukio hili la siku linawataka watoto na vijana wengi wajipyaishe katika juhudi kubwa ya kueneza Injili; kuwa na uchaguzi na mtindo wa maisha binafsi katika umri wao

Sr. Angela Rwezaula - Vatican

Sikukuu ya Tokeo la Bwana yaani Epifania au Tokeo la Bwana ni siku ambayo inakumbusha siku ile Mamajusi kutoka mashiriki ya mbali waliongozwa na Nyota kuu hadi katika mji wa  Bethlehemu. Kwa mujibu wa maandishi matakatifu ya Biblia inathibitisha kuwa yote hiyo ilikuwa ni ishara kutoka mbinguni.  Hiyo ni Nyota isiyo ya kawaida iliwavutia Mamajusi ambao walikuwa ni wataalam na wasomi wa mambo ya nyakati na hata katika chimba chimba maandishi matakatifu kuhusu nyota na mwishowe nyota hiyo iliwaongoza hadi kwa mtoto mchanga Yesu.

Katika Injili ya mathayo (Mathayo 2:1-12) nyota hiyo ilikuwa ishara kutoka mbinguni kwa maana nyingine tunaweza kusema nyota hiyo ilikuwa sehemu ya mpango wa Mungu ili kuonyesha kwamba Baba alimheshimu na kumkubali mtoto Yesu kuwa Mwana wake mpendwa. Mara ngapi tumeimba nyota ya kule mbinguni inaangaza. Na kumbe nyota ndiyo hiyo iliyowaongoza Mamajusi hadi kumwona mtoto mchanga. Katika kuadhimisha Onesho la Bwana yaani Epifania, sambamba na Siku ya watoto wamisionari kwa mwaka 2019 (au kwa maana nyingine utoto Mtakatifu) wameongoza na kauli mbiu “ ishi na sambaza Neno. Siku hii imekuwa sasa ya utamaduni wa kila tarehe 6 Januari,katika Sikukuu ya Epifania ya Bwana  kuadhimisha pia  Siku ya Kimisionari kwa watoto na vijana ambayo inajulikana "Siku ya Utoto Mtakatifu".

Siku ya Utoto Mtakatifu uandaliwa na Sekretarieti ya Kipapa

Siku hiyo inaandaliwa na Sekretarieti ya Kipapa ya matendo ya Utoto Mtakatifu, yaani umisionari wa watoto ambao kwa mwaka huu wamepewa jukumu la kutafakari kwa kina katika kuliishi neno na baadaye kuliweka katika matendo hasa kueneza Neno. Kwa kawaida nchi nyingi duniani pia kama nchini Italia, watoto wanajinyima zawadi zao ndogo kama fedha wakiziweka kama sada kwenye makopo yao na kutunza kwa lengo la kutoa zawadi hiyo siku ya Sikukuu ya Epifania ya Bwana, kwa ajili ya watoto  wengine wahitaji mahali popote ambapo kama parokia inakuwa imechagua kuelekeza sadaka hiyo au ufadhili huo. Hii ni njia mojawapo kwa namna ya pekee ya kuwasaidia watoto waishi na uzoefu wa kwanza wa mchakato katika hatua za kimisionari. Njia hii inawafanya watoto waishi na uzoefu tayari wakiwa wadogo kujinyima, kujisadaka kwa ajili ya watoto wengine ambao wanahitaji zaidi yao!

Kutazama ishara ya Mamajusi waliotangulia

Kwa kutazama watu ambao walianza  taratibu hatua hadi kufika pangoni na kumsujudu Yesu mtoto ni jambo la kutafakari na kujiuliza kwa kina na matumaini ya tukio hili katika mioyo yetu, kwa maana waliona ishara, nyota  na wakaanza hatua ya safari yao kutafuta na hatimaye waliona. Watu wengi duniani leo hii wanaishi katika kutafuta na matarajio! Na wengine, bila kufanya hivyo na hata bila ya kujibidisha. Kanisa linashughuli ya kuwa ishara, ya kuwa nyota na ili kwa taratibu kuweza kuwafikisha kaka dada kwake Yesu Kristo. Tendo hili  linawezekana tu, kuanzia katika familia ambayo inafundisha watoto kumtafuta Yesu, kuanza hatua ya taratibu kwa kuongozwa na nyota; nyota ya matendo hai ya sala na matendo hai ya kusaidiana kindugu, kuhurumiana kindugu na kupendana.

Ndiyo njia na mwafaka wa kuanziaha siku ya Utoto mtakatifu ili kuanza kueneza Injili kwa kila mtoto na kijana hadi kufikia utu uzima. Kwa hakika siku ya Utoto Mtakatifu, inafanyika katika mabara yote matano ili kujipyaisha katika wajibu wao wa kimisionari. Inawagusa kwa namna ya pekee watoto  wote duniani ambao kwa njia ya sala na sadaka yao, wanawasaidia watoto wenzao wanaoteseka kila kukicha katika mazingira magumu ya maisha na mara nyingi hatarishi ambao kwa dhati wanahitaji ushuhuda wa kindugu na mshikamano.

 

07 January 2019, 11:11