Tafuta

Mpango Mkakati wa Mwezi Oktoba 2019: Sala, Ushuhuda, Majiundo makini na endelevu sanjari na huduma ya upendo Mpango Mkakati wa Mwezi Oktoba 2019: Sala, Ushuhuda, Majiundo makini na endelevu sanjari na huduma ya upendo 

Mpango Mkakati Mwezi Oktoba 2019: Neno, Katekesi, Ushuhuda!

Papa anataka waamini wajitahidi kukutana na Kristo Yesu kwa njia ya Ekaristi Takatifu, Neno la Mungu na Sala. Pili ni ushuhuda wa wamisionari watakatifu, wafiadini na waungama imani, kielelezo makini cha uwepo endelevu wa Kanisa sehemu mbali mbali za dunia. Tatu ni majiundo makini ya kimisionari kwa kujikita katika: Biblia, Katekesi, Tasaufi na Taalimungu. Nne ni huduma ya upendo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mwezi Oktoba 2019 Kanisa litakuwa linaadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu Papa Benedikto XV alipochapisha Waraka wa Kitume"Maximum Illud" yaani “Kuhusu Shughuli za Kimisionari.” Papa Benedikto XV katika Waraka huu, alifungua rasmi ukurasa mpya wa maisha na utume wa Kanisa mintarafu shughuli za kimisionari, kwa kulitaka Kanisa kuanzisha mchakato wa majiundo na malezi kwa ajili ya kuyategemeza Makanisa mahalia kwa rasilimali watu, yaani wahudumu wa Injili!

Mpango Mkakati wa Mwezi Oktoba 2019 unaongozwa na kauli mbiu “Mmebatizwa na kutumwa: Kanisa la Kristo katika utume”.  Kanisa linataka kuendeleza wito na utume wake wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia, agizo kutoka kwa Kristo mwenyewe kwa wafuasi wake. Maadhimisho haya ni muda wa: sala, katekesi, tafakari na matendo ya huruma! Ni wakati kwa waamini walei kutambua haki, dhamana na wajibu wao katika maisha na utume kwa Kanisa. Hii ni fursa ya kuwahimiza waamini kujiwekea sera na mikakati ya kuyategemeza Makanisa mahalia: kwa njia ya rasilimali watu, vitu na fedha, ili Kanisa liendelee kutangaza Injili ya huruma na upendo hadi miisho ya dunia!

Baba Mtakatifu Francisko analitaka Kanisa kujikita zaidi katika utekelezaji wa mambo makuu manne: Mosi, waamini wajitahidi kukutana na Kristo Yesu kwa njia ya Ekaristi Takatifu, Neno la Mungu na Sala. Pili ni ushuhuda wa wamisionari watakatifu, wafiadini na waungama imani, kielelezo makini cha uwepo endelevu wa Kanisa sehemu mbali mbali za dunia. Tatu ni majiundo makini, endelevu na fungamani ya kimisionari kwa kujikita katika: Biblia, Katekesi, Tasaufi na Taalimungu. Nne ni huduma ya upendo kama kielelezo cha imani tendaji!

Huu ni ufafanuzi uliotolewa na Askofu mkuu Giovanni Pietro Dal Toso, Katibu Mwambata wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu na Rais wa Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa, wakati wa maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumbu kumbu ya Mwenyeheri Paolo Manna, kila mwaka ifikapo tarehe 16 Januari. Huyu ni muasisi wa tasaufi wa uragibishaji  wa ari na mwamko wa kimisionari miongoni mwa wa Wakristo ili kutambua: ukuhani, ufalme na unabii wao. Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa yamechapisha mwongozo unaopatikana kwenye mtandao kwa anuani ifuatayo: http://www.october2019.va/ .

Hapa waamini wanaweza kujipatia maelezo ya kina kama yalivyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati anatangaza maadhimisho ya Mpango Mkakati wa Mwezi Oktoba 2019. Mwongozo huu usaidie kuleta ari na mwamko mpya katika maisha na utume wa kimisionari kwa kujikita katika sala inayomwilishwa katika ushuhuda wa imani tendaji. Waamini wahamasike kuchangia shughuli za kimisionari ndani na nje ya mazingira yao. Hapa msingi mkubwa ni waamini kukutana na Kristo Yesu katika maisha ya sala na tafakari ya kina ya Neno la Mungu; maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa bila kusahau ushuhuda makini ambao umetolewa na watakatifu, wafiadini pamoja na waungama imanui. Kwa ufupi, Mpango Mkakati wa Mwezi Oktoba, uliotengwa maalum kukuza na kudumisha ari na mwamko wa kimisionari ndani ya Kanisa unafumbatwa katika mambo makuu yafuatayo: Biblia, Katekesi, Tasaufi na Ukarimu wa Kimisionari.

Mwezi Oktoba 2019
19 January 2019, 10:55