Tafuta

Papa Francisko. Utambulisho na vipaumbele vyake: Utu, heshima na haki msingi za binadamu; dhana ya sinodi katika maisha na utume wa Kanisa, Haki na amani duniani. Papa Francisko. Utambulisho na vipaumbele vyake: Utu, heshima na haki msingi za binadamu; dhana ya sinodi katika maisha na utume wa Kanisa, Haki na amani duniani. 

Papa Francisko: Utambulisho na vipaumbele katika utume wake!

Papa Francisko kwa watu wengi duniani anaonekana kuwa ni chemchemi ya faraja na matumaini; mtetezi wa maskini na wanyonge; kiongozi mwenye Ibada ya pekee kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa; ni kiongozi anayeheshimu na kuthamini dhamana, utu na heshima ya wanawake katika maisha na utume wa Kanisa; akazia "dhana ya Sinodi" katika maisha na utume wa Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko kwa watu wengi duniani anaonekana kuwa ni chemchemi ya faraja na matumaini; mtetezi wa maskini na wanyonge; kiongozi mwenye Ibada ya pekee kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa; ni kiongozi anayeheshimu na kuthamini dhamana, utu na heshima ya wanawake katika maisha na utume wa Kanisa. Haya ni kati ya mambo mazito yaliyogusiwa na Kardinali Marc Armand Ouellet, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Maaskofu katika mahojiano maalum na Gazeti la L’Osservatore Romano.

Anasema, dhamana, wajibu, changamoto na matatizo wanayokabiliana nayo wanawake Amerika ya Kusini ndicho kilichokuwa kiini cha mkutano wa Tume ya Kipapa kwa ajili ya Amerika ya Kusini kilichofanyika hapa mjini Vatican kuanzia tarehe 6-9 Machi 2018 kwa kuwashirikisha wanawake, ili kujadili mustakabali wao kwa sasa na kwa siku za usoni. Mkutano huu uliongozwa na kauli mbiu “Mwanamke, mhimili wa ujenzi wa Kanisa na Jamii Amerika ya Kusini”. Hii ni changamoto iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati alipokutana na kuzungumza na wajumbe wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Amerika ya Kusini huko Bogotà wakati wa hija yake ya kitume! 

Papa aliwakumbusha kwamba, matumaini ya Amerika ya Kusini yanafumbatwa katika sura ya mwanamke. Mkutano huu ulifanyika katika mazingira ya uhuru kamili kwa kuwapatia wanawake kuelezea: matatizo, changamoto na fursa zilizoko mbele yao katika maisha na utume wa Kanisa Amerika ya Kusini. Injili ya Kristo iwe ni mwongozo rejea katika majadiliano ya kuwajengea uwezo wanawake kwani Kristo Yesu aliwajali na kuwathamini sana wanawake, akawapatia uhuru wa kushiriki katika maisha na utume wake, kiasi ya kuwa ni mashuhuda wa Fumbo la Ufufuko, kiini cha imani na maisha ya Kanisa. Alijali na kuthamini utu na heshima yao kama binadamu.

Kardinali Marc Ouellet anaendelea kufafanua kwamba, katika miaka ya hivi karibuni, Kanisa limeendelea kuwashirikisha wanawake katika maisha na utume wake, kwa kutumia karama na mapaji waliyokirimiwa na Mwenyezi Mungu. Lakini, katika kipindi cha miaka 50 iliyopita, kumekuwepo na mchango mkubwa unaotolewa na wanawake katika medani mbali mbali za maisha. Kumbe, Jamii iendelee kuwekeza elimu makini kwa wanawake, ili waendelee kuchangia mchakato wa ustawi, maendeleo na ustawi wa wengi.

Kanisa linaendelea pia kuwekeza zaidi huko Amerika ya Kusini kwa kutambua na kuthamini wingi wa Wakristo; utajiri mkubwa wa: lugha, tamaduni na imani ya watu, licha ya kuandamwa na baa la umaskini, lakini ni watu wanaotambua kwamba, wanayo nafasi ya pekee katika jamii; maisha na utume wa Kanisa. Ni waamini wenye Ibada maalum kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa kama inavyoshuhudiwa na Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake kwa kujikita katika: ufukara, amani na utunzaji bora wa mazingira, karama na utajiri kutoka kwa Mtakatifu Francisko wa Assisi bila kusahau malezi na majiundo yake ya Kiyesuit. Kanisa Amerika ya Kusini ni rasilimali, ni jamii yenye ujumbe wa kinabii kwa watu wa Mataifa. Hiki ni kipindi cha neema na baraka kwa Kanisa Amerika ya Kusini.

Baba Mtakatifu anaendelea kumwilisha matunda ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican katika maisha na utume wa Kanisa, kwa kukazia umuhimu wa watu wa Mungu kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa. Hiki ni kiini cha “dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa”. Baba Mtakatifu anakazia ukuhani wa waamini wote; umuhimu wa waamini kushiriki kikamilifu Sakramenti za Kanisa; umuhimu wa majadiliano ya kidini na kiekumene; ari na mwamko wa kimisionari pamoja na umuhimu wa waamini walei kuwa ni chachu ya utakatifu kwa njia ya ushuhuda wa maisha, kielelezo cha imani tendaji!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, maskini ni amana na utajiri wa Kanisa, hawa ni walengwa wa kwanza wa mchakato mzima wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Umoja, upendo na mshikamano wa dhati ni mambo msingi katika utangazaji na ushuhuda wa Injili ya upendo kwa watu wa Mataifa. Mambo yanayopaswa kuzingatiwa ni: Ufahamu wa Neno la Mungu; umuhimu wa toba na wongofu wa ndani; ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Haya ni mambo msingi katika mchakato mzima wa uinjilishaji mpya kwa wakati huu!

Dhana ya Sinodi ni wazo lililotolewa na Mwenyeheri Paulo VI, linaloihusisha Familia ya Mungu katika ujumla wake. Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya kumbu kumbu ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa maadhimisho ya Sinodi ndani ya Kanisa Katoliki, alilitaka Kanisa kuanza kumwilisha dhana hii katika maisha ya Makanisa mahalia; Mabaraza ya Maaskofu; Mashirikisho ya Kanda hadi kufikia Kanisa la Kiulimwengu. Katika kipindi cha miaka miwili, Kanisa limepyaisha dhana ya Sinodi kwa kuwa na mbinu mpya iliyowashirikisha Mababa wengi wa Sinodi kwa kutoa nafasi zaidi kwa makundi madogo madogo, yajulikanayo kitaaluma kama “Circuli minori”.

Kardinali Marc Ouellet anakazia umuhimu wa  Sinodi kwani zitawasaidia waamini kuchota utajiri wa amana na nyaraka mbali mbali zinazotolewa na Kanisa kwa ajili ya kuboresha maisha na utume wa maisha yao na kuendelea kujikita katika: Shule ya Neno, Sakramenti na Ukarimu mintarafu uhalisia wa maisha yao. Maadhimisho ya Sinodi yanaweza kuwa ni nafasi kwa Makanisa mahalia kusoma alama za nyakati na kujibu changamoto za shughuli za kichungaji kwa umoja na mshikamano dhati. Kimsingi, “dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa” ndio mwelekeo mpya wa mchakato wa maisha na utume wa Kanisa!

Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka Mtakatifu wa Huruma ya Mungu alisema,  Imani ya Kikristo inapata muhtasari wake katika huruma ya Mungu ambayo ni hai, inaonekana na imefikia hitimisho lake kwa Kristo Yesu, kielelezo cha upendo wa Mungu, anayetaka kila mwanadamu akombolewe, Agano ambalo limefungwa kwa njia ya Damu Azizi ya Yesu na kwamba, huruma ya Mungu inaweza kuwafikia watu wote wanaoikimbilia.

Huruma ya Mungu anakaza kusema Baba Mtakatifu iko wazi kama malango matakatifu yanayogusa moyo wa Mungu anayependa na kufanya subira ili kuwapokea na kuwakumbatia tena wale waliotenda dhambi na kukimbia mbali na uwepo wake. Huruma ya Baba inaweza kuwafikia watu kwa kuwa na dhamiri nyofu; kusikiliza Neno la Mungu linaloongoa moyo wa mtu; kwa kukutana na watu wenye huruma; kwa kuguswa na mang’amuzi ya maisha yanayosimulia kuhusu madonda ya ndani; dhambi, msamaha na huruma ya Mungu. Baba Mtakatifu anafafanua zaidi kwamba, njia ya wazi na iliyonyooka inayomhakikishia mwamini maondoleo na msamaha wa dhambi ni Yesu Kristo mwenye mamlaka ya kusamehe dhambi; utume ambao amelikabidhi Kanisa.

Sifa za Askofu: Shuhuda wa Kristo Mfufuka; Mitume wa huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu; Waalimu wa manga’amuzi ya maisha; watangazaji na mashuhuda wa Injili ya furaha. Baba Mtakatifu Francisko anasema, pengine inafaa kwa Kanisa kuchunguza sifa hizi kwa wale wanaotarajiwa kuteuliwa kuwa Maaskofu kabla ya kusonga mbele na uchunguzi wa mambo mengine. Lakini, kimsingi Askofu anapaswa kuwa mtu mnyenyekevu, mpole na ambaye yuko tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu.

Kardinali Marc Ouellet anahitimisha mahojiano haya kwa kusema, huu ni mwongozo unaoobubujika kutoka katika Neno la Mungu na ambao unapaswa kufuatwa kwa ukamilifu. Maaskofu wenye sifa na karama kama hizi, ndio wenye uwezo wa kuratibisha maisha na utume wa Kanisa kwa ubora zaidi! Kinachotakiwa mbele ya Mungu ni unyenyekevu na moyo wa huduma; umahiri wa kuhubiri ni nyongeza tu. Kardinali Marc Ouellet anasema, Kanisa linainjilisha kwa njia ya ushuhuda wa furaha ya Injili inayobubujika kutoka kwa Kristo Mfufuka. Askofu, kimsingi anapaswa kuwa kweli ni mtu wa Mungu, kwa njia ya uwepo wake wa kibaba, kwa ajili ya huduma kwa wote pasi na ubaguzi!

Kardinali Marc Ouellet
16 January 2019, 09:26