Tafuta

Vatican News
Utume wa familia unafumbatwa katika haki na huruma ya Mungu! Utume wa familia unafumbatwa katika haki na huruma ya Mungu!  (Vatican Media)

Ndoa na Familia: Kumbatieni haki na huruma ya Mungu!

Wanandoa ni watu wanaopaswa kusikilizwa kwa makini kwa njia ya msaada wa Roho Mtakatifu ili kuweka mambo bayana mintarafu haki na huruma ya Mungu; uzuri na utakatifu wa maisha ya ndoa ya Kikristo. Wakristo katika hija ya maisha yao, wajitahidi daima kutafuta na kutekeleza mapenzi ya Mungu na wasikubali kumezwa na malimwengu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumanne, tarehe 29 Januari 2019 amezindua rasmi mwaka wa Mahakama Kuu ya Rufaa ya Kipapa “Rota Romana”. Baba Mtakatifu katika hotuba yake, amekazia: umoja na uaminifu; mpango mkakati wa utume wa maisha ya ndoa na familia; umoja, ukarimu na upendo aminifu kwa watu wa ndoa, kwani Kanisa linataka kujielekeza zaidi kwa ajili ya kudumisha imani, afya na ustawi wa watu wa ndoa na familia.

Monsinyo Pio Vito Pinto, Dekano wa Mahakama Kuu ya Rufaa ya Kipapa, katika hotuba yake kwa ajili ya kumkaribisha Baba Mtakatifu, amependa kumhakikishia kwamba, wao ni walezi na wawajibikaji makini katika malezi ya dhamiri nyofu ya Wakristo, kwa kuwasaidia na hatimaye kuamua juu ya hatima ya ndoa zenye mgogoro. Mahakama hii inawajibika pia kuwasaidia viongozi wa Kanisa katika utekelezaji wa dhamana na majukumu yao ya kitume, kwa kuwa karibu zaidi na wanandoa watarajiwa katika hija ya malezi na majiundo yao ya awali na endelevu, kwa kutambua kwamba, wao ni nguzo muhimu ya maisha ya Kikristo!

Monsinyo Pio Vito Pinto amekazia umuhimu wa familia kama chemchemi ya miito mitakatifu ndani ya Kanisa, changamoto na mwaliko kwa wanandoa na familia kuwa ni mashuhuda na vyombo vya Injili ya uhai, upendo na huduma. Ili familia ziweze kutekeleza dhamana na wajibu wake barabara, zinapaswa kuwa na ajira za kudumu, ili waweze kulipwa ujira wa haki na hivyo kudumisha utu na heshima yao.  Monsinyo Pio Vito Pinto amesikitishwa na tabia ya baadhi ya vyombo vya mawasiliano ya jamii kushupalia kashfa za maisha ya ndoa na familia na hivyo kusahau: uzuri, utakatifu na udumifu wa watu wa ndoa katika maisha yao. Hii ndiyo habari kwamba, wanandoa wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu!

Askofu mkuu Edgar Pèna Parra, Katibu mkuu msaidizi wa Vatican, ndiye aliyeadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kufungua Mwaka wa Mahakama Kuu ya Rufaa ya Kipapa, kwa kukazia umuhimu wa kuweka uwiano mzuri kati ya haki na huruma ya Mungu. Wadau katika Mahakama hii, watambue kwamba, licha ya nyaraka mbali mbali wanazokutana nazo kila siku katika utume wao, lakini nyuma yake kuna watu wa ndoa ambao wametikiswa katika utu na undani wao. Wanandoa ni watu wanaopaswa kusikilizwa kwa makini kwa njia ya msaada wa Roho Mtakatifu ili kuweka mambo  bayana mintarafu haki na huruma ya Mungu; uzuri na utakatifu wa maisha ya ndoa ya Kikristo. Wakristo katika hija ya maisha yao, wajitahidi daima kutafuta na kutekeleza mapenzi ya Mungu na wasikubali kumezwa na malimwengu.

Kwa kufikiri, kuishi na kutenda kwa namna hii, kutawasaidia waamini kusonga mbele, licha ya matatizo na changamoto mbali mbali wanazoweza kukumbana nazo katika maisha. Fadhila ya unyenyekevu na maisha ya sala ziwe ni nyenzo msingi kwa wafanyakazi wa Mahakama kuu ya Rufaa ya Kipapa, kwani, katika utume wao wanashiriki katika utekelezaji wa fumbo la wokovu. Haki inapaswa kuritubishwa na taalimumgu, yaani ufahamu zaidi wa Fumbo la Mungu katika maisha ya mwanadamu. Ukuu wa Fumbo la Umwilisho, uwasaidie na kuwawajibisha kutafakari wajibu wao kama sehemu ya mchakato wa utambuzi wa Kristo na wokovu wa mwanadamu. Kama Bikira Maria, wawe tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutekeleza mapenzi ya Mungu. Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa awalinde na kuwasimamia katika utume wao, ili waweze kuupenda na hatimaye, kulitumikia Kanisa kwa ari na moyo mkuu.

Ndoa na familia
30 January 2019, 16:19