Siku ya Ukoma Duniani 2019: Mapambano dhidi ya ubaguzi, unyanyapaa na maamuzi mbele! Siku ya Ukoma Duniani 2019: Mapambano dhidi ya ubaguzi, unyanyapaa na maamuzi mbele! 

Ujumbe kwa Siku ya Ukoma Duniani kwa Mwaka 2019

Mapambano ya kutokomeza ubaguzi, unyanyapaa pamoja na maamuzi mbele dhidi ya wagonjwa wa Ukoma duniani ni njia makini ya kuonesha mshikamano na wagonjwa pamoja na waathirika wa Ukoma. Ni watu wanaopaswa kupendwa, na kupewa tiba muafaka. Ndani ya Kanisa kuna mifano hai ya watakatifu kama Damian de Veuster waliojisadaka kwa ajili ya huduma kwa wagonjwa hao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Siku ya Ukoma Duniani ilianzishwa kunako mwaka 1954 na inaadhimishwa na Jumuiya ya Kimataifa kila mwaka, Jumapili ya mwisho wa mwezi Januari na kwa mwaka 2019, siku hii imeadhimisha hapo tarehe 27 Januari 2019. Kardinali Peter Kodwo Appiah Turkson, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu katika ujumbe wake kwa Siku ya Ukoma Duniani anawataka viongozi wa Kanisa pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, wanapambana kufa na kupona hadi kutokomeza ubaguzi, unyanyapaa pamoja na maamuzi mbele dhidi ya wagonjwa wa Ukoma duniani.

Takwimu zinaonesha kwamba, kila mwaka zaidi ya watu 200, 000 wanapata maambukizi mapya ya ugonjwa wa Ukoma na kwamba, hii ni sawa na asilimia 94% katika nchi 13 duniani. Kanisa katika maisha na utume wake, linamwangalia Kristo Yesu alivyoonesha upendo na ukarimu kwa wagonjwa wa Ukoma, akawatakasa na kuwarejeshea tena hadhi na utu wao kama wana wa Mungu. Hii ndiyo changamoto inayoendelea kutolewa na Baba Mtakatifu Francisko kwa kuwataka watu wa Mungu kuonesha mshikamano wa upendo na huruma kwa wagonjwa wa Ukoma.

Mapambano ya kutokomeza ubaguzi, unyanyapaa pamoja na maamuzi mbele dhidi ya wagonjwa wa Ukoma duniani ni njia makini ya kuonesha mshikamano na wagonjwa pamoja na waathirika wa Ukoma. Ni watu wanaopaswa kupendwa, kuheshimiwa, kuthaminiwa na kupewa tiba muafaka. Ndani ya Kanisa kuna mifano hai ya watakatifu kama Damian de Veuster waliojisadaka kwa ajili ya huduma kwa wagonjwa wa Ukoma, akiwaonesha watu jinsi hata ya kuganga na kuponya ukoma wa maisha yao ya kiroho!

Baba Mtakatifu anawataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kujenga na kudumisha utamaduni wa watu kukutana na kusaidiana kwa hali na mali, kama ilivyokuwa hata kwa Mtakatifu Francisko wa Assisi aliyemwona Kristo Yesu, miongoni mwa wagonjwa wa Ukoma. Umoja na mshikamano na wadau mbali mbali ni muhimu sana katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukoma duniani! Huu ni ugonjwa unaoweza kudhibitiwa kwa tiba na elimu makini kwa jamii.Jumuiya za waamini na watu wenye mapenzi mema zisimame kidete kupambana kikamilifu na tabia ya ubaguzi, kwa kuhakikisha kwamba, watu wanahudumia: kiroho na kimwili. Wagonjwa wa Ukoma waoneshwe upendo, mshikamano na utu wao kuheshimiwa na wote. Mama Kanisa anawashukuru na kuwapongeza wale wote wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa wagonjwa wa Ukoma sehemu mbali mbali za dunia.

Siku ya Ukoma 2019
31 January 2019, 15:08