Cerca

Vatican News
IWCC na Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini wanakazia umuhimu wa Elimu ya Amani Duniani miongoni mwa waamini wa dini mbali mbali. WCC na Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini wanakazia umuhimu wa Elimu ya Amani Duniani miongoni mwa waamini wa dini mbali mbali.  (AFP or licensors)

WCC: Umuhimu wa elimu ya amani duniani kwa waamini wote!

Katika majadiliano yao, viongozi wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni, WCC na Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini wameendelea kuboresha “Hati ya Elimu ya Amani Duniani katika Dini Mbali mbali”. Huu ni mradi unaotekelezwa kwa pamoja baina ya taasisi hizi mbili, ambazo zimekuwa zikishirikiana tangu mwaka 1977.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ujumbe wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni, WCC, hivi karibuni umekutana na viongozi wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini, kama sehemu ya utamaduni na desturi ya kukutana walau kila mwaka, ili kubadilishana mawazo, uzoefu na mang’amuzi katika medani mbali mbali za maisha, tayari kuibua mbinu mkakati unaopaswa kufanyiwa kazi katika kipindi cha mwaka 2019. Katika majadiliano yao, viongozi hawa wameendelea kuboresha “Hati ya Elimu ya Amani Duniani katika Dini Mbali mbali”. Huu ni mradi unaotekelezwa kwa pamoja baina ya taasisi hizi mbili, ambazo zimekuwa zikishirikiana tangu mwaka 1977.

Matunda ya ushirikiano huu ni pamoja na mradi wa “Sala ya dini mbali mbali” iliyotolewa kunako mwaka 1994. Tafakari kuhusu Ndoa ya Mseto iliyotolewa kunako mwaka 1997. Kati ya mazingira mapya mengi yanayodai uangalifu na bidii ya kiuchungaji ya Kanisa inatosha kukumbuka: ndoa za mseto (hii ni ndoa kati ya watu wa madhehebu au dini tofauti). Taasisi hizi mbili kunako mwaka 2011 zikafanya tafakari ya pamoja kuhusu “Ushuhuda wa Wakristo katika ulimwengu wenye dini nyingi” na mwaka 2011wakachapisha “Ushauri wa mwenendo wa maisha. Viongozi wa taasisi hizi wameridhika na ushirikiano uliopo kati yao na kwamba, wameonesha nia ya kutaka kuendeleza umoja na ushirikiano huu mintarafu mchakato wa majadiliano ya kidini!

Mama Kanisa daima amekuwa mstari wa mbele kuwafunda walimwengu kuhusu umuhimu wa kuchuchumilia na kuambata amani katika maisha yao, kama chachu muhimu sana katika maendeleo ya watu kiroho na kimwili. Waamini na wapenda amani duniani wanayo dhamana kubwa kuhakikisha kwamba, wanaendelea kuwafunda vijana wa kizazi kipya kuhusu umuhimu wa amani katika maisha bila kuchoka kwani amani inawezekana kabisa ikiwa kama binadamu watapania. Haki asilia na kanuni maadili zinapaswa kuzingatiwa na wote, ili kweli amani iweze kutawala katika mioyo ya watu.

Ikiwa kama kanuni hizi msingi zingefuatwa na kuzingatiwa Jumuiya ya Kimataifa isingeshuhudia wala kuendelea kushuhudia mauaji ya kimbari sehemu mbali mbali za dunia na kwamba, dunia kwa sasa inaanza kuonja cheche za Vita kuu ya tatu ya dunia. Hii inatokana na ukweli kwamba, rasilimali na utajiri wa mali asili, uchu wa mali na madaraka, udini na utaifa ni mambo ambayo yameendelea kuwa ni chanzo kikuu cha vita na matokeo yake ni makundi makubwa ya wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi kuendelea kuteseka kwa kutafuta hifadhi na usalama wa maisha.

Mafundisho Jamii ya Kanisa ni mwaliko kwa waamini kuchuchumilia: haki msingi za binadamu, amani, ustawi na maendeleo fungamani kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshima ya binadamu. Majadiliano ya kidini yanalenga kujenga na kudumisha amani, umoja, upendo na mshikamano kati ya walimwengu. Maadhimisho ya Siku ya Kuombea amani duniani, kila tarehe mosi, Januari yaliyoanzishwa na Mwenyeheri Paulo VI ni changamoto endelevu kwa waamini kusali kwa ajili ya kuombea amani na Jumuiya ya Kimataifa kuendelea kujikita katuika mchakato wa kudumisha utamaduni wa amani.

Majiundo makini ya amani yanapaswa kujikita katika dhana ya majadiliano katika ukweli na uwazi pamoja na upatanisho kama anavyokaza kusema Mtakatifu Paulo VI. Mtakatifu Yohane Paulo II alifanikiwa kuwakutanisha viongozi wa dini mbali mbali ili kusali kwa ajili ya kuombea amani huko Assisi tarehe 26 Oktoba, 1986. Papa mstaafu Benedikto XVI alikazia umuhimu wa vijana kufundwa utamaduni wa haki na amani na kwamba, majadiliano ya kidugu ni muhimu sana katika kukuza haki, amani na mshikamano wa kidugu. Huu ndio mwelekeo unaopewa msukumo wa pekee hata na Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Katika nyakati hizi, Mama Kanisa anapenda kuwahamasisha waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema kuwekeza katika utamaduni wa amani kwa kuwa na lugha inayowagusa vijana wa kizazi kipya kama chachu ya maendeleo endelevu. Utamaduni wa amani utoe kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshima ya binadamu; haki msingi za binadamu na vipaumbele vyake: kiroho na kimwili. Kila mtu ajisikie kwamba, anapenda na kupendwa na watu. Majiundo ya utamaduni wa amani yajikite pia kwenye mitandao ya kijami inayotumiwa kwa kiasi kikubwa na vijana wa kizazi kipya. Watu wajifunze kupenda na kuheshimu tofauti zao; uhuru wa mtu kutoa mawazo yake sanjari na kujenga utamaduni wa kusikilizana.

Baraza la Makanisa Ulimwenguni
12 January 2019, 15:53